Filamu : Dkt. Harrison Mwakyembe aahidi kuwatokomeza Waharamia wa Kazi za Filamu kwa maslahi ya Wasanii na Taifa. - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


12 Oct 2017

Filamu : Dkt. Harrison Mwakyembe aahidi kuwatokomeza Waharamia wa Kazi za Filamu kwa maslahi ya Wasanii na Taifa.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameahidi kuhakikisha kwamba suala la uharamia wa kazi za filamu za Watanzania nchini unakomeshwa mara moja kwa kuwasaka wahusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria.

Kauli hiyo ameitoa Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Wamiliki wa Majumba ya Kuonyeshea Sinema ambapo moja ya changamoto kubwa aliyotajiwa na wamiliki hao ni suala la uharamia wa kazi za sanaa jambo ambalo linawakwamisha wamiliki hao kutokana na ukweli kwamba baadhi ya watu wasio waaminifu wamekuwa wakivujisha filamu mpya kwa kuziuza kiholela mitaani na wengine wakihuisha filamu hizo katika mitandao ya kijamii jambo linalosabibisha hasara kubwa kwa wasanii na wamiliki wa majumba ya sinema.

Mhe. Mwakyembe amesikitishwa na vitendo vya baadhi ya watu hao wanaojihusisha na uharamia wa kazi za filamu za Watanzania huku akiapa kuwashughulikia popote walipo watu hao ili kuhakikisha kuwa Wasanii wananufaika na kazi zao na pia Wamiliki wa Majengo ya Sinema wananufaika pia kwa kuonyesha kazi za wasanii hao kwa utaratibu ambao hautomuumiza msanii mwenye kazi yake.

“Najua baadhi ya Wamiliki wa Majumba ya Sinema mnapata hasara, na hata baadhi ya Wasanii pia, suala hili linanikera sana na kamwe haikubaliki hata kidogo, tutahakikisha kwamba watu wa namna hii wanatoweka katika tasnia yetu, tutawasaka popote walipo na kuwapeleka kwenye vyombo vya Sheria kwani Serikali hii sio ye mchezo na watu wa namna hii”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Ameongeza kuwa, yeye kama Waziri mwenye dhamana na Wizara hiyo atahakikisha kwamba hamasa ya kutosha inatolewa kwa Watanzania ili wawe na utamaduni wa kuangalia sinema zinazotengenezwa nchini katika Majumba ya Sinema yaliyopo nchini.

Aidha, Dkt. Mwakyembe amewapongeza Wasanii nchini kwa kutoa kazi nyingi huku akiwataka kuhakikisha kwamba ubora unazingatiwa na maadili yanazingatiwa kwa ajili ya jamii na pia amewashauri Wamiliki wa Majumba hayo kutenga siku maalum ambayo itakuwa ikitumika kuonyesha Sinema za Kiswahili zenye maadili na kuzitaka sinema hizo kupewa muda wa kutangazwa katika vyombo vya habari nchini ili wananchi wengi wapate kuzijua na kuweza kutembelea majumba hayo kwa ajili ya kuzitazama.

“Mi nadhani na sisi Tanzania tukianzisha utamaduni wa kwamba siku Fulani ni siku ya kuonyesha Sinema za Kiswahili tu, hii itaweka historia nchini lakini iwe picha nzuri tu na tuzitangaze filamu hizo na sisi kama Wizara tuna haja ya kuongea na baadhi ya vituo vya televisheni, magazeti pamoja na redio kuzitangaza filamu hizo kwani hii itasaidia kuinua soko la filamu nchini. Bodi ya Filamu Tanzania hakikisheni kwamba pindi itakapoamuliwa kuwa siku fulani ni siku ya kuonyesha filamu za Kiswahili basi muone haja ya kuzipunguzia tozo baadhi ya filamu hizo zitakazokuwa zikionyeshwa lakini tu mpaka hapo itakapoamuriwa”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Juliana Shonza amewapongeza Wasanii wa Tanzania kwa kujitoa kwao katika kuonyesha vipaji vyao katika kuhakikisha kwamba vipaji hivyo vinaitangaza Tanzania Kimataifa.

“Nafurahi kuona kuwa Filamu za Watanzania zinafanya vizuri na Tanzania tuna Waigizaji wanaofanya vizuri kwahiyo naamini kwamba mkiitumia vizuri hiyo fursa ya uigizaji mtakuwa mnaitendea haki nchini yetu na kuinua vipaji vyenu lakini pia mtakuwa mmeitangaza Tanzania Kimataifa”, alisema Mhe. Shonza.

Mhe. Waziri Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa ameongozana na Naibu wake Mhe. Juliana Shonza kwa pamoja wamekuwa wakikutana na wadau mbalimbali wa kisekta ikiwa ni sehemu ya utaratibu waliojiwekea lengo likiwa kutambua changamoto zao na namna ya kuzitatua kwa manufaa ya Taifa.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) pamoja na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Juliana Shonza (katikati) wakiwa katika moja ya Jumba la Kuonyeshea Sinema lililopo Jijini Dar es Salaam wakati walipokutana na Wamiliki wa majengo hayo na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu filamu na uonyeshaji wake 11 Oktoba, 2017. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara hiyo, Bibi Leah Kihimbi.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) pamoja na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Juliana Shonza (katikati) wakiwa katika moja ya Jumba la Kuonyeshea Sinema lililopo Jijini Dar es Salaam wakati walipokutana na Wamiliki wa majengo hayo na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu filamu na uonyeshaji wake 11 Oktoba, 2017. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara hiyo, Bibi Leah Kihimbi.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wa pili kulia) pamoja na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Juliana Shonza (kushoto) wakiangalia moja ya kifaa kikubwa kitumikacho kuonyeshea sinema maarufu kama Projekta wakati walipokutana na Wamiliki wa Majumba hayo na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu filamu na uonyeshaji wake 11 Oktoba, 2017.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wa pili kulia) pamoja na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Juliana Shonza (kushoto) wakiangalia moja ya kifaa kikubwa kitumikacho kuonyeshea sinema maarufu kama Projekta wakati walipokutana na Wamiliki wa Majumba hayo na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu filamu na uonyeshaji wake 11 Oktoba, 2017.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) pamoja na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Juliana Shonza (katikati) wakiwa wameongozana na baadhi ya Wamiliki wa Majumba ya Kuonyeshea Sinema wakati walipokutana na Wamiliki wa majengo hayo na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu filamu na uonyeshaji wake 11 Oktoba, 2017.(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad