Baadhi ya wabunge wa mabunge ya Uingereza wakiwa katika kikao na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt, Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (wa tatu kushoto), akiongoza majadiliano na Ujumbe wa Wabunge watano pamoja na maafisa kadhaa kutoka nchini Uingereza, walipomtembela na kufanya naye mazungumzo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto), akisisitiza jambo alipokutana na kufanya mazungungumzo na wabunge kutoka nchini Uingereza waliomtembelea Jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Kaimu Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mamelta Mutagwaba.
Baadhi ya Ujumbe kutoka Tanzania walioshiriki mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na baadhi ya Wabunge kutoka nchini Uingereza, Jijini Dar es Salaam (kulia ni Mkurugenzi wa masuala ya Sheria Bi. Susana Mkapa akifuatiwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bw. Paul Sangawe.
Kamisha wa Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Mgonya Benedicto (kushoto) na Msajili wa Hazina, Dkt. Oswald Mashindano, wakifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na wageni wake, Wabunge wa Mabunge ya Uingereza (Baraza la Mamwinyi na Bunge la Wawakilishi).
Kiongozi wa Wabunge wa Bunge la Uingereza waliotembelea nchini na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), Mhe. David Linden, akizungumza namna nchi hiyo inavyosaidia masuala mbalimbali nchini ikiwemo Elimu na lishe.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akizungumza na Wabunge kutoka Nchini Uingereza waliomtembelea katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na kuipongeza nchi hiyo kwa kuisadia Tanzania katika masuala mbalimbali, amesisitiza ushirikiano wa nchi hizo mbili ujikite zaidi katika masuala ya biashara na uwekezaji.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kushoto) na Kiongozi wa Ujumbe wa Wabunge kutoka Uingereza, Mhe. David Linden (katikati) na Wabunge wengine kutoka Uingereza, Maafisa Waandamizi kutoka Tanzania, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa Mkutano katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati)akijadili jambo na baadhi ya maafisa walioambatana na Wabunge wa Bunge la Uingereza baada ya kumalizika kwa Mkutano kati yao ulioangazia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Elimu, lishe, na Matumizi adili ya rasilimali fedha, Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Tanzania imetoa rai kwa Serikali ya Uingereza kubadili mfumo wa uhusiano wake kwa kujikita zaidi katika masuala ya biashara na uwekezaji badala ya kutoa misaada ya kawaida ili nchi iweze kukuza uchumi wake kwa haraka zaidi.
Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wabunge kutoka mabunge ya uingereza (Baraza la Mamwinyi na Bunge la Wawakilishi).
Dokta Mpango amesema kuwa kiwango cha mtaji ambacho Serikali ya Uingereza imewekeza nchini hadi sasa ni Paundi bilioni 2.5 lakini kwa upande wa biashara kati ya nchi hizo mbili, hali si nzuri.
"Mwaka 2015 Tanzania iliuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 22.5 na kununua bidhaa kutoka Uingereza zenye thamani ya Dola milioni 150, kiwango ambacho ni kidogo sana na tunahitaji kufanya biashara zaidi" Alisisitiza Dkt. Mpango.
Alielezea hatua mbalimbali ambazo Serikali inazichukua kuimarisha uchumi wa viwanda na kuelezea changamoto kubwa ikiwa na namna ya kuendeleza kilimo kwa ajili ya kupata malighafi za viwanda na kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuwa kilimo ndicho kinaajiri idadi kubwa ya Watanzania.
Dkt. Mpango alitoa wito kwa Serikali ya Uingereza kuwekeza zaidi katika viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa mbalimbali ikiwemo kujenga viwanda vya kutengeneza matrekta na zana nyingine za kilimo, kusindika bidhaa za mazao ya wakulima pamoja na kuwekeza katika sekta za kuongeza thamani ya madini na nishati ya umeme.
Dokta Mpango aliwaeleza Wabunge hao kwamba hivi sasa Serikali imepiga hatua kubwa kiuchumi na kuishukuru Uingereza kwa mchango mkubwa inaoutoa kusaidia Elimu, Lishe, Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma na afya kwa upande wa lishe, uwekezaji ambao kwa pamoja umefikia zaidi ya paundi milioni 180.
Kwa upande wake, kiongozi wa Wabunge watano waliomtembelea Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa David Linden, amesema wamefurahishwa na namna Tanzania inavyopiga hatua kubwa kimaendeleo na kudhibiti vitendo vya rushwa.
Amesema kuwa wameridhishwa na kiwango cha miradi wanayoifadhili katika sekta ya elimu na afya hususan masuala ya lishe kwa watoto na kwamba nchi yao itaendelea kuisaidia Tanzania ili iweze kufikia malengo yake kiuchumi na kijamii
Wabunge hao wapo nchini tangu Jumapili iliyopita na wanatembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza.
No comments:
Post a Comment