Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewapongeza Wajasiriamali wa Tanzania kwa ushiriki wao katika Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST.
Dkt. Mwakyembe ametoa pongezi hizo leo mjini Kampala nchini Uganda katika viwanja vya Mashujaa Kololo alipotembelea kujionea namna tamasha hilo lilivyopokelewa na wadau wake walioiwakilisha Tanzania wakiwemo wajasiriamali toka vikundi mbalimbali, vikundi vya ngoma, vikundi vya sanaa ya maigizo pamoja na baadhi ya wasanii.
Katika tamasha hilo, Dkt. Mwakyembe pia alipata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya wajasiriamali hao pamoja na kuongea nao huku akijionea bidhaa mbalimbali zinazouzwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jambo ambalo limemfurahisha sana hususani kwa upande wa watu kutoka Tanzania kwakuwa wamejaza mabanda yao kwa bidhaa kadha wa kadha.
“Tamasha hili linaonyesha utajiri mkubwa wa sanaa, utamaduni pamoja na bidhaa tulizonazo kama nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na hapa tumekutana kwasababu tunabadilishana mawazo na kuonyeshana bidhaa mbalimbali za nchi zetu”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha, katika ziara hiyo, Dkt. Mwakyembe amewatoa wasiwasi wajasiriamali hao kuhusu suala la upatikanaji wa masoko huku akiwaahidi kuwatafutia fursa ya kuwapeleka wajasiriamali hao pamoja na bidhaa zao Bungeni mjini Dodoma ili ziweze kupata soko kwa urahisi kupitia wabunge.
“Niwatoe wasiwasi wajasiriamali wote wa Tanzania mliohudhuria hapa, nitahakikisha kuwa pindi tunaporudi nyumbani nitatafuta wasaa wa kulishawishi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili nyie mpate nafasi ya kuleta bidhaa zenu katika viwanja vya Bunge ili basi Wabunge wapate kujua haswa vitu vizuri mlivyonavyo nah ii itawasaidia kuviuza kwa urahisi zaidi na kujipatia vipato vyenu”, aliongeza Dkt. Mwakyembe.
Sambamba na hilo, Dkt, Mwakyembe amewahakikishia wajasiriamali hao kuhusu suala la kujitangaza kupitia vyombo vya habari akisema kwamba, atajitahidi kutoa ushawishi kwa vyombo vya habari nchini ili viweze kuwapatia muda wa kuwatangaza wajasiriamali hao ili wapate kujulikana ikiwemo shughuli wazifanyazo.
“Nitahakikisha kuwa siku mnapopewa nafasi ya kuja viwanja vya Bunge basi mnapata muda wa kutosha katika vyombo vya habari ili mpate kujulikana, hivyo kila mmoja wenu naamini atapewa nafasi ya kufanya mahojiano kwa kujieleza shughuli azifanyazo na mahali anapopatikana na hii itawasaidia kupata masoko zaidi toka kwa watu mbalimbali”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wao wajasiriamali hao wameshukuru Waziri Mwakyembe kwa juhudi alizowafanyia hususani za kuhakikisha kwamba wanahudhuria kwa kiwango kikubwa katika tamasha hilo, lakini pia ahadi aliyowapa ya kuwapeleka Bungeni ili wakatangaze bidhaa zao na kuwatangaza katika vyombo vya habari nchini.
Tamasha la JAMAFEST lilianzishwa mwaka 2013 nchini Rwanda na baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kwa mwaka huu tamasha hilo linafanyika mjini Kampala nchini Uganda ambapo pia tamasha hili linatarajiwa kufanyika tena katika moja ya nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2019.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akiangalia ngoma ya kiutamaduni iliyokuwa ikipigwa na Kikundi cha Sanaa na Utamaduni Tanzania (TaSUBA) katika banda lao wakati wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika mjini Kampala, Uganda 13 Septemba, 2017.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akimsikiliza mjasiriamali wa Tanzania kuhusu baadhi ya bidhaa zilizopo katika banda lao wakati wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika mjini Kampala, Uganda 13 Septemba, 2017.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akipokea zawadi ya shati toka kwa mjasiriamali wa Tanzania mara alipotembelea banda lao wakati wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika mjini Kampala, Uganda 13 Septemba, 2017.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (mwenye tai nyekundu) akiangalia moja ya ubunifu wa picha iliyochongwa na mjasiriamali wa Tanzania wakati wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika mjini Kampala, Uganda 13 Septemba, 2017.PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.
No comments:
Post a Comment