Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Alli Karume akipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na SSRA kutoka kwa Afisa Uhusiano wa Mamlaka Bw. Sabato Kosuri alipotembelea banda hilo wakati wa maadhimisho ya siku ya Bahari Duniani yaliyofanyika mkoani Kigoma.
Na. Zawadi Msalla.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Alli Karume ameitaka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kusimamia kwa ukaribu michango ya Wanachama kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili itumike kwa malengo yaliyokusudiwa kwa mujibu wa Sheria zilizoanzisha mifuko hiyo.
Wito huo umetolewa jana mjini Kigoma na Waziri Karume alipotembelea banda la SSRA kwenye maonesho ya wiki ya Bahari duniani yanayoendelea kwenye viwanja vya shule ya msingi Mlole Mkoani humo.
Waziri Karume alisema SSRA inawajibu mkubwa wa kumlinda mwanachama wake ili kuhakikisha hapati matatizo pale anapotakiwa kupata mafao yake.Pia alisisitiza kuwa Itakuwa ni jambo la kuumiza sana inapotokea mwanachama mwenye matumaini ya kupata mafao yake atakapoambiwa mfuko umefilisika na hivyo mafao anayoyatarajia hawezi kuyapata.
Aidha Mhe. Karume aliipongeza SSRA kwa elimu wanayoendelea kuitoa kwa jamii juu ya umuhimu wa kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na jinsi wanavyo simamia maboresho mbalimbali yanayoendelea katika sekta hiyo.
Hata hivyo alisema bado SSRA inawajibu mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii ili kushawishi wananchi kuona umuhimu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwani wapo wananchi wengi wasio fahamu umuhimu wa mifuko hiyo na wengi wao hupata shida inapofikia kipindi cha uzeeni.
Awali akitoa maelezo ya shughuli za SSRA Afisa Uhusiano na Uhamasishaji wa Mamlaka hiyo Bw. Sabato Kosuri alimhakikishia Mhe. Waziri usalama wa michango ya wanachama kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Bw.Kosuri alisema tayari SSRA imeweka miundombinu imara ya kusimamia eneo hilo ikiwa ni pamoja na miongozo ya uwekezaji pamoja na kaguzi za mara kwa mara ili kuhakikisha mifuko inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria kanuni na taratibu na hivyo kuwahakikishia usalama wachangiaji wote kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii iliundwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135 (Toleo la 2015) kwa lengo la kusimamia na kudhibiti Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa manufaa ya Wanachama na Taifa kwa ujumla. Mamlaka ilianza kazi rasmi mwishoni mwa Mwaka 2010.
Mamlaka ina jukumu la msingi la kuhakikisha kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inakuwa endelevu, inaendeshwa kwa kufuata kanuni, taratibu na kisheria, wanachama wanapata taarifa za Mifuko/michango yao, na mafao yaliyobora.
No comments:
Post a Comment