WATAALAMU na wanazuoni wamekubaliana haja ya kupitia mpango wa maendeleo endelevu wa viwanda, SIDP (1996-2020), ili kwenda na wakati kwa kubadili kilimo na kuiweka nchi katika njia bora ya kufikia uchumi wa viwanda. Kauli hiyo imetamkwa kwa namna tofauti na wataalamu hao ambao wamekutana jijini hapa kuangalia uhusiano uliopo kati ya viwanda, mabadiliko ya tabia nchi na kilimo; na ni namna gani sera ya viwanda inaweza kupitiwa upya kuakisi mahusiano haya. Warsha hiyo iliyoandaliwa na ESRF na CUTS International imelenga katika kuelezea umuhimu wa kuangalia mahusiano ya sera ya maendeleo ya viwanda na mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa chakula na biashara. Wakijadili mada mbalimbali zilizowasilishwa katika semina hiyo iliyofanyika ESRF, wataalam hao walitambua umuhimu wa pekee wa kupitia upya sera hiyo ili iweze kuonesha muunganiko fasaha uliopo kati ya viwanda, kilimo na biashara; na hatua/mikakati ipi iwepo kukinga adhma hii ya viwanda dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi. Wamesema kwamba kwa kuunganisha sera ya maendeleo endelevu ya viwanda na uchakataji wa bidhaa za kilimo na kilimo chenyewe kunaleta mwanya wa kuweka msingi imara katika mchakato wa maendeleo na hasa viwanda. Pia, kwa kuwa na sera madhubuti, nchi itaweza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya Viwanda, hususani viwanda vinavyotegemea maligafi za sekta ya kilimo.
Mkuu wa Idara ya Utafiti na Machapisho wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Fortunata Makene akitoa neno la ukaribisho kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Tausi Kida wakati wa mkutano wa awamu ya pili ya kuangalia Tabia nchi, Uboreshaji kilimo, na mahusiano yake na biashara kwa jumuiya ya Afrika Mashariki (PACT EAC2), uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.[/caption] Katika mkutano huo ilikubalika haja ya kuwa na mikakati ya utetezi kwa kuangalia tafiti zitakazofanywa juu ya kinachojiri katika maendeleo kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa chakula na biashara. Zaidi ya yote, pia wadau waliona kuna haja kubwa ya kuwa na tafiti itayoweza kuonesha ni kwa kiasi gani sera ya SIDP (1996-2020) imeweza kuchangia katika ukuaji wa viwanda Tanzania, na changamato zipi imekumbana nazo ambazo zinapaswa kutatuliwa na kuanishwa wakati wa mapitio ya sera hii. Akiwasilisha hoja yake ndugu Solomon Baregu, Mtafiti wa ESRF na Meneja wa Mradi wa PACT EAC 2, amesema kwa kuangalia hali halisi ya sasa ipo haja kwa wataalamu kutambua changamoto zinazojitokeza katika maendeleo endelevu ya viwanda na kukiangalia kilimo kama msingi wa uimarishaji wa viwanda. Aidha alisema kwamba kwa kuangalia hali ya sasa ipo haja kubwa ya kubadili kilimo cha Tanzania ili kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha viwanda kwa kuvipatia mali ghafi ya kutosha na yenye ubora. Alisema ni vyema kuelewa uhusiano uliopo katika sera za maendeleo ya viwanda na kilimo ili kuwa na mpango mahsusi wa utetezi kwa lengo la kuimarisha viwanda. Katika mkutano huo washiriki pia walipitia mambo mbalimbali na hatua zinazochukuliwa kupitia sera ya mpango wa maendeleo wa viwanda unaomalizika 2020.
Alisema kwa taifa la Tanzania ili lisonge mbele ni vyema masuala muhimu katika SIDP yakaangaliwa ili kutekeleza mipango ya maendeleo ya viwanda kwa kuhusisha na uchakataji wa mazao ya kilimo. Aidha alisema katika utafiti utakaosaidia kuboresha SIDP majukumu ya biashara ya kimataifa katika maendeleo ya viwanda na tabia nchi haviwezi kudharaulika. Alisema utafiti utakaofanywa utasaidia kuongeza ‘nyama’ zaidi katika mikakati ya maendeleo kwa kufanya utetezi kwenye mabadiliko ya tabia nchi, biashara na usalama wa chakula kwa kufanya mabadiliko makubwa katika uchakataji bidhaa za kilimo kwa kutambua pia makubaliano ya kimataifa ambayo Tanzania ni mshiriki, hususani UNFCCC na WTO.

No comments:
Post a Comment