Jana tarehe 28 Agosti, 2017 Katibu Mkuu wa Shirikisho la Jumuiya za Wanafunzi watanzania wanaosoma katika Jamhuri ya watu wa China (TASAFIC) Bw. Remidius Mwema Emmmanuel alikutana na kufanya mazungumzo na Naibu waziri wa Vijana, Kazi na Ajira Nchini Tanzania Mhe. Anthony Mavunde.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ofisini kwake mjini Dodoma, pamoja na mambo mengine yalilenga ufahamu juu ya nafasi ya vijana wa kitanzania wanaohitimu masomo yao nje ya nchi hususani China namna ambavyo wanaweza kunufaika na kutumia vema fursa mbalimbali za kiuchumi kwa manufaa ya Taifa pindi wanaporejea nchini baada ya kuhitimu masomo yao. Hata hivyo Mhe.
Mavunde alipokea maelezo mafupi juu ya mkakati wa Shirikisho (TASAFIC) kwa Vijana wa Kitanzania pindi wanapohitimu wanavyoweza kuwa chachu ya mabadiliko na kuchangamkia fursa zilizopo nchini kwa kutumia Uzoefu na taaluma wanayoipata nje ya nchi. Kwa upande wake Mhe. Mavunde alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na TASAFIC na kuongeza kuwa Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko tayari na inaendelea kuwaunga mkono Vijana wote wanaoonyesha uthubutu wa kujikwamua kiuchumi.
Akizungumzia Upande wa kilimo, alisema baadhi ya Vijana wamekuwa na mitizamo ya kutojihusisha na Kilimo, Lakini hii inatokana na wengi wao kujaribu kilimo kwa kutozingatia kanuni na misingi bora ya Kilimo na kuona jambo hilo haliwezekani.
"Serikali sasa tuna mikakati ambayo tuna hakika itasaidia kuondoa dhana hizo na kuwafanya vijana wengi kupenda kilimo, ikiwa ni pamoja na Kutoa Elimu zaidi na kuwatumia vijana waliofanikiwa ili waweze kuaelimisha wenzao. Mfano tunao vijana wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) wanaitwa SUGECO, Serikali iliwapatia udhamini wa fedha kupitia Benki ya CRDB, wakafanya kilimo na sasa wamekuwa ni taasisi kubwa na wameanza kusaidia vijana wenzao kupitia mafunzo na misaada mbalimbali.
Lakini wapo vijana Mkoani Mbeya, Ruvuma na Mikoa mingine ambao wamepata mafanikio makubwa. Jambo la msingi ni vijana kubadili mitizamo, tunayo Benki yetu ya maendeleo ya kilimo, Mifuko ya pembejeo, Mifuko ya uwezeshwaji wananchi na mfuko wa maendeleo ya Vijana hiyo ni hatua mojawapo lakini bado Serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha vijana kupitia vikundi rasmi wanajenga utayari wa kujihusisha na kilimo, hata kilimo cha muda mfupi (Mboga mboga) ambacho pia kimeleta manufaa makubwa kwa makundi ya Vijana.
Sasa ni waombe mtambue kwamba nynyi TASAFIC kupitia watanzania wote wanaosoma China Taifa linawategemea na ni matarajio yetu kwamba Taaluma zenu zitatumika kikamilifu kubadilisha kundi kubwa la vijana pale mtakaporejea nchini " Alisema Mhe .Mavunde Akitoa shukrani kwa Naibu waziri huyo, Bw. Remidius kwa niaba ya TASAFIC amesema TASAFIC Itaendelea kutumia Fikra,Taaluma,mawazo na kutoa maoni mbalimbali yenye lengo la kuleta tija kwa Taifa.
“Mhe .Naibu waziri nakuhakikishia kwamba TASAFIC itaendelea kuwajibika na kuwatumikia watanzania wote wanaosoma Jamhuri ya watu wa China chini ya ungalizi wa Ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini China na nitafikisha ujumbe kwa wasomi hao,Ikiwa ni pamoja na kuielezea vyema na kuwakumbusha fursa njema na mikakati ya Serikali iliyopo kwa wasomi hao pindi watakapohitimu Masomo yao na kurejea nchini (Tanzania).
Ingawa Miongoni mwa wahitimu kutoka Chuo Kikuu Cha Kilimo Nchini China kwa mwaka 2017 baada ya kurejea nchini tayari wameonyesha nia kuanzisha Shamba maalum la Mfano kulima zao la Muhogo, aidha Tunacho chama cha Jumuiya ya Watanzania ambao waliowahi kusoma China (CAAT) ambao pia wameendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha taaluma,Uzoefu na Maarifa ya watanzania wote waliosoma China yanatumika kikamilifu kwa manufaa ya Taifa,” Alisema Katibu Mkuu Remidius Emmanuel
No comments:
Post a Comment