Matukio : Waziri Mkuu Awaasa Watumishi Wanaofanyakazi Viwandani - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


31 Jul 2017

Matukio : Waziri Mkuu Awaasa Watumishi Wanaofanyakazi Viwandani





WAZIRI MKUU Mhe. Kassim Majaliwa amewasihi Watanzania wanaofanya kazi katika viwanda mbalimbali nchini kufanya kazi kwa bidii na kuwa waaminifu.
Amesema Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda hivyo ni vema watakaopata fursa ya ajira katika viwanda hivyo kuwa waadilifu.
Ameyasema hayo Jumapili, Julai 30, 2017 wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha gesi cha Ikama kilichoko wilayani Rungwe.
Waziri Mkuu amesema wakati Serikali ikiendelea kuwakaribisha wawekezaji nchini, wananchi walioajiriwa kwenye maeneo hayo wawe waaminifu.

“Mnatakiwa muwe waaminifu, msibebe kitu chochote ndani ya kiwanda bila ya ridhaa ya wamiliki kwa kuwa mtaonyesha taswira mbaya kwa wawekezaji.”
Amesema uaminifu wao ndio utawezesha Watanzania wengi kupata ajira kwenye viwanda hivyo ambavyo vimejengwa katika maeneo yao.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na kampuni ya TOL Gases, Mhandisi Harold Temu alisema kiwanda kinauwezo wa kuzalisha tani 46 kwa siku.

Alisema gesi inayozalishwa kiwandani hapo ni ya Carbon Dioxide ambayo inauzwa nchini na nchi jirani za Zambia, Malawi, Zimbabwe na Congo.

Mhandisi Temu alisema wateja wakubwa wa gesi hiyo ni viwanda vya kutengenezea soda, bia na pia hutumika katika kuhifadhia chakula na kwenye vifaa vya kuzimia moto.

Mapema Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kuchakata majani ya chai cha Katumba, ambapo alisema Serikali inaimarisha Ushirika wa zao hili ili wakulima waweze kupata tija.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa umma wa wilaya ya Rungwe Julai 30, 2017. Kulia ni Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson na kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa kiwanda cha gesi cha TOL Gases Limited kilichopo katika kijiji cha Ikama wilayani Rungwe Baada ya kuwasili kiwandani hapo Julai 30, 2017 Kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana viongozi wa kiwanda cha chai cha Katumba wilayani Rungwe alipowasili kiwandani hapo kukagua shuguli za kiwanda hicho Julai 30, 2017.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda cha chai cha Katumba wilayani Rungwe Julai 30, 2017. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla na kushoto ni Meneja Uzalishaji wa kiwanda hicho, Bw. Ramadhani Kampasili.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akitazama chai iliyosindikwa na kufungashwa tayari kwa kuuzwa wakati alipotembelea kwianda cha chai cha Katumba wilayani Rungwe Julai 30, 2017.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Tukuyu Wilayani Rungwe baada ya kutembelea kiwanda cha Chai cha Katumba Julai 30, 2017.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Ufundi, Bw. McJohn Mbiri (kulia Kwake) kuhusu mitambo ya kuzalisha gesi ya hewa ya ukaa wakati alipotembelea kiwanda cha TOL Limited kilichopo katika kijiji cha Ikama wilayani Rungwe Julai 30, 2017. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na wazee wa kijiji cha Busokelo baada ya kuwasili kwenye uwanja wa michezo wa Kandete katika jimbo la Busokelo kuhutubia mkutano wa hadhara Julai 30, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia ngoma ya asili ya Kimyakyusa iitwayo "Ndigala" baada ya kuwasili kwenye uwanja wa michezo wa Kandete katika jimbo la Busokelo mkoani Mbeya kuhutubia mkutano wa hadhara
Sehemu ya watumishi wa umma wa wilaya ya Rungwe wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipozungumza nao Julai 30, 2017.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad