Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Giidabuday akizungumza Dar es Salaam jana kuhuzu masuala mbalimbali ya mchezo huo. Kushoti na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya RT, Tullo Chambo na kulia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Wachezaji ya RT, Mwandu Jilala.
Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya taifa ya riadha yatafanyika Mkuza, Kibaha mkoani Pwani kwa siku mbili kuanzia Julai 22 na kushirikisha wanariadha kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, mashindano hayo awali yalitakiwa kufanyika mwezi uliopita, lakini yalisogezwa mbele ili kupisha mashindano ya shule za Sekondari na Msingi ya Umisseta na Umitashumta inayofanyika Mwanza.
Gidabuday alisema kuwa hatua ya kusoeza mbele mashindano hayo ya taifa ni kuwezesha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kushiriki ili kuinua vipaji vyao.
Aliitaka mikoa yote kufanya maandalizi ya maana ili kueleka timu iliyoiva vizuri kwa ajili ya kutoa ushindani katika mashindano hayo ya taifa yatakayofanyika kwenye viwanja vya shule za Filbert Bayi.
Aidha, Gidabuday alisema kuwa benchi la ufundi la timu ya taifa ya vijana watakaoshiriki mashindano ya dunia kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 18 limeanguliwa na sasa timu hiyo itakuwa chini ya kocha mkuu Rehema Killo badala ya Robert Kalihaye.
Alisema kuwa Killo atasaidiwa na Yohana Misese wakati meneja wa timu hiyo atakuwa Christian Katembo, ambao wanachukua nafasi ya Mwinga Mwanjala na Peter Mwita. Mwanjala ameteuliwa kuwa kocha wa wachezaji wa riadha watakaoshiriki mashindano ya Michezo ya Jumuiya ya Madola ya Vijana itakayofanyika Bahamas baadae mwezi ujao.
Mbali na riadha, Tanzania katika michezo hiyo ya Madola itashirikisha pia mchezo wa kuogelea ambao nao utakuwa na wachezaji wawili.
Wakati huohuo, Gidabuday amesema kuwa RT haihusiki na kuvurundwa kwa mchezo wa riadha katika Michezo ya Shule za Sekondari nchini (Umisseta) inayoendelea jijini Mwanza, kwani hawakushirikishwa kwa lolote.
Alisema kuwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) liliwatumia barua ya mualiko RT ikiwa imechelewa, hivyo hawajapeleka wataalam wao katika michezo hiyo, ambayo itafuatiwa na ile ya shule za msingi (Umitashumta).
No comments:
Post a Comment