Matukio : Waziri Lwenge atakiwa Kuhakikisha Maji Yanapatikana kisarawe - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 22 June 2017

Matukio : Waziri Lwenge atakiwa Kuhakikisha Maji Yanapatikana kisarawe


Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.


Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge pamoja na watendaji wake kuhakikisha Mji wa Kisarawe uliopo mkoani Pwani unapata huduma ya maji safi na salama.


Rais Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo jana mkoani Pwani wakati akizindua Mradi wa upanuzi wa Mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa Mabomba Makuu kutoka Mlandizi kwenda Jijini Dar es Salaam.


Mh. Magufuli amesema kuwa Mkoa wa Pwani umefanya kazi kubwa ya kutunza miundombinu ya maji ambayo imewezesha kuhudumia wananchi wa Dar es Salaam hivyo ni haki kwa wananchi wa Mkoa huo kufaidika na maji wanayoyatunza kwa muda mrefu.


“Ninafahamu Mji wa Kibaha kwa sasa hauna shida ya maji, shida iliyopo ni kuzidi kwa presha ya maji ambayo sio tatizo la DAWASA wala DAWASCO hivyo ili kutatua tatizo hilo ni jukumu la Wizara husika na watendaji wake kujipanga na wahandisi wa maji kuunganisha bomba kutoka Wilaya ya Kibaha hadi Kisarawe ambapo kuna changamoto ya maji safi na salama,” alisema Rais Magufuli.


Akiongelea utunzaji wa miundombinu ya maji, Rais Dkt. Magufuli amewataka watendaji wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhakikisha wanashughulikia maji yanayopotea kwa kurekebisha miundombinu ambayo imeharibika na kuweka miundo mbinu mipya inayoweza kuhimili wingi wa maji.


Aidha, Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya India kwa kutoa trilioni 1.3 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji kwa Miji 16 nchini ambayo ikikamilika itawezesha wananchi wengi kupata maji safi na salama hivyo amewaahidi kudumisha ushirikiano uliopo katika sekta ya maji baina ya nchi hizo mbili.


Kwa upande wake Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema kuwa Mradi huo ni sehemu ya miradi mikubwa saba ya kimkakati inayoendelea kupanuliwa ikiwemo ya upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini, Ruvu Juu, Uchimbaji visima virefu, Ujenzi wa bwawa la Kidunda, upanuzi wa mtandao wa usambazaji maji, mradi wa kupunguza upotevu wa maji na uboreshaji wa mfumo wa majitaka.


“Mradi huu umejengwa na fedha za mkopo jumla ya shilingi bilioni 87 kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim ambapo umesaidia pia kujenga nyumba 17 za wafanyakazi katika eneo la mradi,” alisema Mhandisi Lwenge.


Mhandisi Lwenge amefafanua kuwa baada ya upanuzi huo mashine zinauwezo wa kuvuta maji kati ya lita milioni 182 - 196 kwa siku hivyo hadi kufikia mwezi Machi, 2016 wananchi 742,611 wa mkoani Pwani wanapata maji safi na salama.


Nae Balozi wa India nchini Tanzania, Sandeep Arya amesema kuwa uhusiano wa sekta ya maji kati ya Tanzania na India ulianza miaka 35 iliyopita na maji ndiyo sekta ya kipaumbele inayounganisha Tanzania na India hivyo uhusiano baina ya nchi hizo ni wa kindugu.


“Uamuzi wa kutoa mkopo wa shilingi Trilioni 1.1 kwa ajili ya mradi wa usambazaji maji katika Miji 17 nchini Tanzania unaendelea kudhihirisha ushirikiano wetu,” alisema Balozi Arya.


Uzalishaji wa sasa wa mitambo yote unafikisha jumla ya lita Milioni 502 kwa siku ambazo ni majumuisho ya maji ya Ruvu Juu lita milioni 196, Ruvu chini lita milioni 270 pamoja na mtambo mdogo wa Mtoni unaozalisha kiasi kidogo kwa siku.


Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dkt. John Pombe Magufuli

No comments:

Post a Comment