Utalii : Ngorongoro Kitovu cha Utalii Kinachowavutia Watu Mashuhuri Duniani - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Monday, 24 April 2017

Utalii : Ngorongoro Kitovu cha Utalii Kinachowavutia Watu Mashuhuri Duniani


Na Jumia Travel Tanzania
Inaonekana mwaka 2017 umeanza vizuri katika sekta ya utalii nchini Tanzania kutokana na watu kadhaa mashuhuri kuzuru vivutio vyake. Sehemu ambazo zimeonekana kuwavutia watu wengi zaidi ni hifadhi ya mbuga ya Serengeti na bonde la Ngorongoro.

Alianza mwigizaji maarufu wa filamu kutokea Hollywood nchini Marekani, Will Smith na mkewe Jada Pinkett-Smith. Mwanzoni mwa mwezi Machi walitua nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kujivinjari katika mbuga ya Serengeti. Wakiwa huko familia ya Smith walikutana na msanii mwingine kutokea huko huko Marekani, lakini huyu yeye ni mwanamitindo na mrembo, Chanel Iman.

Haikupita muda mrefu sana tangu watu hao mashuhuri kuwepo nchini, kwani siku chache zilizopita aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Taifa la Israel, Bw. Ehud Barak naye alitembelea mbuga ya Serengeti pamoja na Ngorongoro.


Hii ni ishara nzuri kwa sekta ya utalii nchini ambapo kupitia watu hawa maarufu wengine nao wanapata taarifa na kuhamasika kutembelea pia.

Lakini lazima tujiulize ni kwa nini Ngorongoro huwavutia watu zaidi na kuwafanya kufunga safari kuja Tanzania na sio sehemu zingine? Jumia Travel imekukusanyia vitu ambavyo vinapatikana katika eneo hilo la urithi wa dunia ambalo hakuna mtu atakayesimuliwa na kutotaka kulitembelea:

Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro. Kama ulikuwa haufahamu bonde la Ngorongoro ni shimo kubwa lililotokana na mlipuko wa volkeno ambalo halijai maji wala kubomoka duniani. Eneo hili ambalo limetangazwa kuwa ni urithi wa dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO); lina urefu wa kilometa 20, kina cha mita 600 na ukubwa wa kilometa za mraba 300.

Vifuatavyo ni vivutio vinavyopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro:

Binadamu na Wanyama kuishi pamoja. Kwa zaidi ya miaka 200 iliyopita watu wa kabila la Wamasai walifika eneo hili na kuishi hapo. Maisha yao ya jadi yamewafanya waweze kuishi pamoja na mifugo yao kwa amani na utulivu kabisa bila ya kuwabugudhi wanyamapori. Mpaka hivi sasa kuna wafugaji wa Kimasai takribani 42,000 wakiishi katika hifadhi pamoja na mifugo yao kama vile ng’ombe, punda, mbuzi na kondoo. Kipindi cha mvua hutoka eneo hili na kuelekea maeneo ya tambarare ambapo kiangazi kikifika hujisogeza maeneo ya karibu ya mlima na misitu iliyopo. Wamasai huruhusiwa kuingiza mifugo yao kwa ajili ya kuilisha na kuinywesha lakini si kufanya shughuli za kilimo; lakini maeneo mengine ya hifadhi wanaruhusiwa kurandaranda.

Bonde la Volkeno na Wanyamapori. Bonde la Ngorongoro lilitokana na mlipuko wa volkeno takribani miaka milioni 3 iliyopita ambapo ni kubwa, lisilobomoka wala kutojaa maji. Lilitangazwa na UNESCO kuwa ni urithi wa dunia mwaka 1979 na ni eneo pekee ambalo binadamu, mifugo na wanyama wanaishi kwa pamoja kwa amani na utulivu kabisa. Unaweza kukuta kuna wakati ng’ombe wa Wamasai wanachunga pamoja na pundamilia katika mbuga za Ngorongoro.

Masalia ya Kale ya Binadamu wa Mwanzo. Ngorongoro ndimo linapopatikana bonde la Olduvai ambalo kwa mujibu wa wanahistoria yanapatikana masalia ya binadamu wa mwanzo kuishi duniani. Hapa ndipo wanaikolojia maarufu Dkt. Louis na mkewe Mary Leakey walipata masalia ya kale likiwemo fuvu la mtu wa kale zaidi, Zinjanthropus, ambaye alipata kuishi miaka milioni 1.75 iliyopita. Utafiti wao uliweza kuvumbua mabadiliko ya taratibu ya ukubwa wa ubongo na zana zao za mawe walizokuwa wanazitumia.

Vivutio vingine. Mbali na vivutio vilivotajwa hapo juu pia kuna vitu vingine chungu nzima vya kuvutia watu wanavyoweza kuvifurahia kuviona.

Ziwa Ndutu na Masek; maziwa haya hujaa kutokana na maji yanayotiririka kutokea milimani, na maji yake hayafai kwa matumizi ya binadamu kutokana na chumvi nyingi iliyonayo.


Oldonyo Lengai; hili ni jina la lugha ya Kimasai likiwa na maana ya ‘Mlima wa Mungu,’ unapatikana nje kidogo ya hifadhi ya Ngorongoro. Ni mlima pekee wenye volkeno hai ambapo ilishawahi kulipuka mwaka 2006 na siku za hivi karibuni mwezi Julai mwaka 2007.

Mchanga Unaohama; safu ya mchanga mweusi umetakana na majivu ya mlima wa volkeno wa Oldonyo Lengai, umekuwa ukisukumwa taratibu kuelekea upande wa Magharibi wa hifadhi kwa kiwango cha mita 17 kwa mwaka. Una kimo cha mita 9 na mzingo wenye urefu wa mita 100, unapatikana Kaskazini mwa bonde la Olduvai.




Bonde la Olkarien; eneo hili nalo ni muhimu katika hifadhi kwani hutoa hifadhi kwa ndege tai aina ya Ruppell Griffon. Msimu mzuri wa kutembelea eneo hili ni miezi ya Machi mpaka Aprili ambapo tai huzaliana. Wanyama huja eneo hili pale panapokuwa na malisho ya kutosha.


Kutazama ndege aina ya Flamingo na wengineo wa kila aina. Ndege aina ya Flamingo wanaonekana sana katika maziwa yanayopatikana ndani ya hifadhi. Mbali na ndege hao pia kuna aina mbalimbali za ndege ambao wanaweza kuonekana katika misimu tofauti ya majira ya mwaka hususani miezi ya mvua.

Safari ya Kuizunguka Hifadhi. Utakuwa hujaifaidi Ngorongoro kama haujavizungukia vivutio mbalimbali vinavyopatikana ndani yake. Kwa kuwatumia waongozaji wa mbuga, hakikisha kwamba unatembelea sehemu kama vile bonde la Olmoti kuelekea nyanda za Embakai, shuka chini kuelekea Bonde la Ufa, pandisha Kaskazini kwenye nyanda za hifadhi ya misitu na kisha eneo la tambarare la Mashariki kuzunga miamba ya Nassera, milima ya Goli na bonde la Olkarien.

Kwa hakika hii ni Edeni ya sasa kama watu wengi wanavyopenda kuiita kutokana na maajabu iliyonayo pamoja na historia ya binadamu wa mwanzo kuishi mule. Sasa kama watu wanasafiri kutoka kila pembe ya dunia kuja kulitembelea eneo hili kwa nini na wewe mtanzania usitenge muda na kupanga kufanya hivyo? Haihitaji kuwa milionea kutembelea eneo hili, kunafikika kwa urahisi na hata malazi ni nafuu pia kwani Jumia Travel wamekurahisishia hilo.

No comments:

Post a Comment