Matukio : Dkt. Kalemani amtaka Mkandarasi REA kuajiri wazalendo - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 6 April 2017

Matukio : Dkt. Kalemani amtaka Mkandarasi REA kuajiri wazalendo



Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kulia), akifunua kitambaa kilichofunika Jiwe la Msingi, kuashiria uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), kwa Mkoa wa Shinyanga. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Negezi, Wilaya ya Kishapu (hawako pichani), wakati wa uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), kwa Mkoa wa Shinyanga. Uzinduzi huo ulifanyika hivi karibuni.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, akiwatunza na kujumuika kucheza ngoma pamoja na moja ya vikundi vya burudani kutoka Shinyanga, kilichokuwa kikitumbuiza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), kwa Mkoa wa Shinyanga hivi karibuni.


Na Veronica Simba – Shinyanga


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, amemtaka Mkandarasi kutoka Kampuni ya M/s OK Electronics and Electric Limited, atakayetekeleza kazi ya kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa Mkoa wa Shinyanga, kuhakikisha anaajiri wananchi wenye sifa kutoka maeneo hayo badala ya kuleta wafanyakazi kutoka mbali.


Alitoa maagizo hayo hivi karibuni katika Kijiji cha Negezi, wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa Mkoa huo.


“Tumia wataalam/vibarua vijana kutoka maeneo haya. Hatutapenda uajiri watu kutoka mbali wakati wafanyakazi wenye sifa wako hapahapa,” alisema Naibu Waziri. Aidha, Dkt. Kalemani, alimwagiza Mkandarasi huyo kuhakikisha anawalipa vibarua mara moja kila wanapokamilisha kazi husika. “Hakuna kulaza malipo kwa sababu sisi tunakulipa vizuri.”


Sambamba na maagizo hayo, Dkt Kalemani, aliutaka uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo, kujipanga na kumsimamia Mkandarasi husika ili kuhakikisha anafanya kazi masaa 24 kwa siku. Alisisitiza kuwa, Ofisa yeyote atakayelegalega kumsimamia Mkandarasi husika kadri inavyotakiwa. Atawajibishwa kwa kuondolewa katika nafasi yake.


Naibu Waziri pia, aliwaelekeza TANESCO kuhakikisha wanawafuata wateja na kuwapatia huduma mahala walipo badala ya kusubiri wateja wawafuate katika Ofisi zao, ambazo ni chache na ziko mbali na makazi ya wananchi wengi hususan walioko vijijini.


Kufuatia maelekezo hayo; aliuomba uongozi wa Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Shinyanga, kuanzisha vituo maalum ambavyo vitatumiwa na Maofisa wa TANESCO kuwahudumia wateja walioko katika maeneo yao.


“Hatuwezi kusubiri kujenga Ofisi, shughuli ambayo itachukua muda mrefu, wakati wananchi wanahitaji umeme,” alisisitiza. Kuhusu suala la wakandarasi binafsi, ambao hufanya kazi ya kutandaza nyaya za umeme katika nyumba za wananchi mbalimbali na kuwatoza kiasi kikubwa cha fedha; Naibu Waziri alitaka tabia hiyo ikome mara moja.


Alitoa maelekezo kuwa ni marufuku kwa Mkandarasi binafsi, kufunga nyaya kwenye nyumba ya mteja yeyote bila kwanza kupata idhini kutoka TANESCO.


Naibu Waziri, aliagiza majina ya wakandarasi binafsi ambao wataidhinishwa na TANESCO kufanya kazi ya kufunga nyaya za umeme kwa wateja, yabandikwe katika Ofisi husika ili wananchi waweze kuwatambua na pia iwe rahisi kuratibu gharama za kazi hiyo, hivyo kuwaepusha wananchi na utapeli kwa kulipishwa gharama kubwa isivyostahili.


Aidha, aliwashauri viongozi wa Halmashauri na Serikali za Vijiji, kutenga hela katika bajeti zao, kwa ajili ya kuunganisha umeme kwenye Taasisi mbalimbali muhimu zikiwemo Shule na Vituo vya Afya. Alikumbusha kwamba, kazi ya kuweka umeme kwenye nyumba na taasisi mbalimbali ni ya wahusika wenyewe, siyo Serikali.


Vilevile, Dkt Kalemani aliwataka wananchi kuwa na ufahamu wa gharama za kuunganishiwa umeme kupitia Mradi wa REA, ambazo alizitaja kuwa ni shilingi 27,000 tu. “Ole wake atakayepandisha gharama hizo kwa maslahi binafsi, atakiona cha moto.”


Aliwahimiza wananchi ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za kufungiwa nyaya za umeme, kuomba kufungiwa kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji kutandaza nyaya katika nyumba yote na ambacho kinaweza kufungwa katika nyumba isiyozidi vyumba vinne.


Uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu (REA III) kwa Mkoa wa Shinyanga; kama ilivyokuwa katika Mikoa mingine ambayo Mradi huo umekwishazinduliwa; ulienda sambamba na kumtambulisha kwa viongozi na wananchi, Mkandarasi atakayetekeleza kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment