Mahakamani : Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yatarajiwa kutoa uamuzi dhidi ya maombi ya Serikali ya Marekani ya kuwataka raia watatu wa Tanzania waodaiwa kuhusika na dawa za kulevya - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


12 Apr 2017

Mahakamani : Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yatarajiwa kutoa uamuzi dhidi ya maombi ya Serikali ya Marekani ya kuwataka raia watatu wa Tanzania waodaiwa kuhusika na dawa za kulevya


Na Karama Kenyunko

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho inatarajia kutoa uamuzi dhidi ya maombi ya Serikali ya Marekani ya kuwataka raia watatu wa Tanzania wanaodaiwa kujihusisha na dawa za kulevya kama waende nchini humo kusikiliza tuhuma hizo ama la.

Wajibu maombi ambao wanatuhumiwa nchini humo ni mfanyabiashara bilionea, Ally Khatib Hajj maarufu kama Shkuba, mfanyabiashara Idd Mafuru na Lwitiko Emmanuel Adam maarufu Tiko.

Katika maombi hayo, serikali inaiomba mahakama itoe amri ya kuwakamata na kuwazuia watuhumiwa hao ambao ni wajibu maombi ianzishe utaratibu wa kuwasafirisha kwenda nchini humo. Uchunguzi unaonyesha kuwa mshtakiwa Shkuba, na wenzake walihusika kwenye njama za kusambaza zaidi ya kilo moja ya dawa za kulevya aina ya Heroine ambazo zimezuiliwa nchini humo.


Wajibu maombi ambao wanatuhumiwa nchini Marekani ambao ni mfanyabiashara bilionea, Ally Khatib Hajj maarufu kama Shkuba (fulana nyekundu), mfanyabiashara Idd Mafuru (wa pili kulia) na Lwitiko Emmanuel Adam maarufu Tiko (kulia) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.


Maombi ya Marekani, yaliyosikilizwa mbale ya hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha, yaliwasilishwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe kupitia, Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki.

Wajibu maombi wanatetewa na jopo la Mawakili watatu, wakiwemo Edson Ndusyepo, Majura Magafu na Adinan Chitare.

Wakati wa usikilizwaji Kakolaki alieleza kuwa Waziri wa sheria wakati huo Mwakyembe alipelekewa maombi ya kutakiwa kwa wajibu maombi hao ambapo Aprili 4, mwaka huu mahakama ilitoa amri ya kukamatwa kwao na Aprili 6 walikamatwa na jana walifikishwa mahakamani hapo ambapo maombi hayo yaliwasilishwa.

Kakolaki ameendelea kudai kuwa maombi ya kuwasafirisha wajibu maombi ni halali kwani kumekuwa na mahusiano ya Tanzania kubadilishana wahalifu na nchi za Ulaya tangu enzi za ukoloni wakati Tanzania inaitwa Tanganyika.

Wakili Kakolaki alibainisha kuwa mwaka 1965 Tanzania iliingia makubaliano na Marekani kwa kubadilishana wahalifu ikiwa ni muendelezo wa kile kilichoanzishwa na watawala wa kikoloni.

Alidai kuwa kutokana na makubaliano hayo, maombi ya Marekani kuwasafirisha wahalifu hao yako kisheria kwa sababu maombi hayo yameelezwa vizuri katika kiapo cha Richard Magnes ambaye ni Wakili msaidizi wa Marekani wa Jimbo la Southern Texas kilichoapwa mbele ya Hakimu Mkazi wa jimbo hilo Nans A. Johnson.

Katika kiapo hicho inaonyesha kuwa katika uchunguzi uliofanyika unaonyesha kuwa mshtakiwa Hassan ama Shkuba anahusika kwenye njama za kusambaza zaidi ya Kilo moja ya dawa za kilevya aina ya Heroine ambazo zinazuiliwa kwa mujibu wa sheria za Marekani.

Inadaiwa kuwa Machi 23, mwaka jana, maofisa wanaofungua mashtaka Marekani (Grand Jury) walifungua kesi dhidi ya Shkuba kwa makosa ya kukiuka sheria za nchi.

Katika kiapo cha wakala, ambacho kimeapwa na Mathew Marcus imeelezwa kuwa watu mbali mbali walikamatwa na mmoja wao alipokamatwa alitoa pipi kwa za dawa za kulevya na alimtaja Shkuba kuwa ndiye aliyemtuma kusafirisha hizo dawa.

Alidai kuwa uchunguzi umebainisha kuwa dawa hizo zilikuwa zikiingia Tanzania kwa kutumia meli kwenye mwambao wa bahari ya Tanzania kwa kutumia maelekezo ya Shkuba na pia Mmoja kati ya wasambazaji alieleza kuwa alifanya safari yake kuja Tanzania lakini kabla ya kufika alikutana na Shkuba Dubai ambapo alilipwa dola 50,000 kama malipo ya awali ya Mzigo wa kilo 100 za Heroine ambazo baadae alizileta Tanzania na kupokelewa na Shkuba.

Kuhusu mjibu maombi wa pili, Iddi Mafuru, Kakolaki alimedai katika uchunguzi uliofanyika ulibaini Mfuru alisafirisha Kilo moja ya Heroin kwenda nchini Marekani, kupitia kiongozi wa taasisi ya dawa hizo nchini Tanzania inayoongozwa na Shkuba.

Aidha Kakolaki ameongeza kuwa kuhusu mjibu maombi Lwitiko, upelelezi unaonyesha alihusika na usafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia ya meli.

Katika maelezo hayo amebainisha kuwa Tiko ni mwananachama wa Taasisi ya Dawa za kulevya ambapo amekuwa akifanya shughuli hizo kwa njia ya kificho.

Hata hivyo, mawakili wa upande wa utetezi ukiongozwa na Magafu, waliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali maombi hayo na kuwaachia huru washitakiwa kwa kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kwamba washitakiwa walijihusisha na biashara hiyo nchini Marekani.

Alisema kuwa, mahakama inatakiwa kujiridhisha kwa usahihi kama kweli watuhumiwa wamejihusisha na biashara hiyo kabla ya kuwasafiurisha ughaibuni. Aliongeza kuwa kiapo kilicholetwa mahakamani hapo kinamapungufu hivyo kama mahakama itakubali kuwasafirisha watuhumiwa marekani basi ni vema wakajua ni kwa kosa gani.

Aidha aliongeza kuwa nchi ya Tanzania inawajibu wa kuwalinda raia wake wote sasa kama wakipelekwa huko bila ya kujua makosa yanayowakabili watakuwa wanahatarisha usalama wao.

Baada ya Hakimu Mkeha kusikilza hoja za pande zote mbili ameahirisha kesi hiyo hadi kesho(leo) kwa ajili ya uamuzi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad