Matukio : Ziara ya Rais Dk. Magufuli Imeonesha Mwelekeo wa Tanzania Tunayoitaka - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


8 Mar 2017

Matukio : Ziara ya Rais Dk. Magufuli Imeonesha Mwelekeo wa Tanzania Tunayoitaka



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

Na Hassan Silayo-MAELEZO


Kuanzia 02 Machi, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alianza ziara ya kikazi ya siku 4 katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara iliyolenga kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.


Ziara hiyo kwa kiasi kikubwa imeonesha dira na mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano hasa katika utekelezaji wa miradi inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali Imani,kabila na itikadi za vyama vyao vya siasa.


Siku ya kwanza ya ziara yake Rais Dkt. Magufuli aliweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Tanzania Goodwill Ceramic Tiles Ltd. kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani ambacho ni kikubwa Afrika Mashariki na Kati kilichogharimu Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza.

Akiongea katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika kiwanda chenye uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku Rais Magufuli alifurahishwa na teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae inayotumiwa na kiwanda hicho na kuhoji kama kuna haja ya serikali kuendelea kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi.


Rais Magufuli alisema kuwa “Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi".


Akiwa njiani kuelekea Mikoa ya Lindi na Mtwara Rais Magufuli alizungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi wa tatu na kupiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.


Aidha, Rais Dkt. Magufuli anawataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha katika kipindi hiki mvua zinaponyesha huku akiweka bayana kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.

Akioneshwa kutoridhishwa na utekeleaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi alipotembelea ujenzi wa mradi wa maji wa Ng'apa Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe 17 Machi, 2015 Rais Magufuli aliagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India Bw. Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo kampuni hiyo itakapokamilisha mradi huo unaotarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.


Katika kuthibitisha amedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda Rais Dkt. Magufuli aliitaka Wizara ya Nishati na Madini Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inafikisha gesi katika kiwanda hicho haraka iwezekanavyo lengo likiwa kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na ukosefu wa gesi ambavyo vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji kusimama mara kwa mara.

Aidha, Dkt. Magufuli aliitaka Wizara hiyo kuhakikisha wanamega eneo lenye makaa ya mawe katika eneo la Ngaka lililopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma na kuipatia kampuni ya Dangote ili iweze kuzalisha yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji kilichopo Mkoani Mtwara.


Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Alhaji Aliko Dangote tangu kianze kuuza saruji bei ya bidhaa hiyo sokoni imeshuka kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja wa kilo 50 hadi kufikia Shilingi 10,000/- na ununuzi wa magari 580 yatasaidia kusafirisha saruji nchi nzima kwa gharama nafuu ambayo watanzania wengi wataimudu.


Wakati akikamilisha Ziara yake Mhe. Dkt. Rais Magufuli alifanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mjini Mtwara ambapo alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inasukuma maendeleo ya Nchi kwa nguvu kubwa kwa manufaa ya wananchi.


Rais Magufuli alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutilia mkazo juhudi za uendelezaji wa bandari ya Mtwara, ujenzi wa barabara, uimarishaji wa miundombinu ya nishati ya umeme, ujenzi wa viwanda vikubwa na usimamizi mzuri wa shughuli za kilimo ambavyo vitasaidia kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu.


Aidha, Rais Dkt. Magufuli alioneshwa kusikitishwa na Mkoa wa Mtwara kufanya vibaya kielimu na kuwataka kuweka msisitizo katika elimu kwani juhudi za Serikali kuwapelekea maendeleo hazitakuwa na maana kama wananchi watakuwa hawana elimu.


Ziara hiyo ya Rais Dkt. Magufuli imeonesha mwelekeo wa Tanzania tunayoitaka hasa katika maeneo ya usimamizi wa miradi na utekelezaji wake kwa maslahi ya umma.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad