MO Dewji Foundation kushirikiana na Tulia Trust kujenga vyoo katika Hospitali ya Rungwe Katika kuendeleza huduma zake kwa jamii, Taasisi ya MO Dewji imeungana kwa pamoja na Taasisi ya Tulia Trust inayomilikiwa na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson kujenga vyoo katika Hospitali ya Rungwe iliyopo mkoani Mbeya. Akizungumza kuhusu ushirikiano huo katika mashindano ya kukimbia ya Tulia Marathon, Mratibu Miradi wa Taasisi wa MO Dewji, Catherine Decker amesema taasisi yao imeamua kushirikiana na Dk. Tulia ili kusaidia kuboresha sekta ya afya ya nchini ambayo kwa sasa bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Catherine alisema Taasisi ya MO Dewji imejikita zaidi katika kusaidia sekta ya elimu, afya na huduma za kijamii na hivyo ushirikiano na Tulia Trust ni mzuri kwao na umekuja ikiwa ni miezi miwili imepita tangu walipotoa msaada mwingine katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya SekouToure iliyopo Mwanza na kama taasisi wana miradi nyingi wamepanga kuifanya ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano.
Mratibu Miradi wa Taasisi wa MO Dewji, Catherine Decker akizungumza kuhusu ushirikiano wa MO Dewji Foundation na Tulia Trust kujenga vyoo katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya Rungwe.
“Huduma za afya ya uzazi zimekua ni changamoto katika sekta ya afya nchini, hivyo taasisi yetu imekusudia kutoa misaada ili kuziboresha na sasa safari yetu imetuleta mkoani Mbeya, ambapo tuna muunga mkono Mheshimiwa Naibu Spika kuchimba vyoo katika hospitali ya Rungwe kwenye wodi za kina mama wajawazito, “Wanawake ni msingi wa maendeleo katika jamii zetu, tafiti zinaonyesha kuwa kufanya kazi na wanawake, kunawapa nafasi ya kuongeza kipato chao, kwani ni njia bora katika kuchangia maendeleo chanya kwa jamii,” alisema Catherine na kuongeza. “Lakini ili tuwaheshimu wanawake tunapaswa kuhakikisha kuwa wanapata huduma za afya ya uzazi, ikiwemo vifaa bora pamoja na mazingira safi ili kuboresha usalama wa afya zao. Kwa kufanya hivi itachangia kuboresha sekta ya afya katika jamii zetu, jambo ambalo tuna litazamia kama taasisi.” Kwa upande wa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania na mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dk. Tulia Ackson aliishukuru Taasisi ya Mo Dewji kwa udhamini huo ambao umeambatana na mashindano ya kukimbia ya Tulia Marathon na malengo ya kuanzisha mashindano hayo ni kukusanya pesa ili kusaidia kuboresha sekta ya elimu na afya.
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania na mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dk. Tulia Ackson akizungumza kuhusu ushirikiano wa MO Dewji Foundation na Tulia Trust kujenga vyoo katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya Rungwe.
“Tulikuwa na malengo maalumu ila kikubwa ni kuimarisha afya na elimu, hospitali ya Rungwe kwa sasa wodi ya kina mama ina choo kimoja na sisi kama Tulia Trust kwa kushirikiana na wadhamini wetu [Mo Dewji Foundation] tumepata fedha ambazo tutajenga vyoo kwa ajili ya hiyo wodi ya kina mama na mabafu pia, “Na hicho ndicho kinachotofautisha marathon hii ya kwetu na hizo zingine, hii tulikuwa na mpango maalumu wa kukusanya fedha ili tuweze kuboresha miundombinu ya elimu na afya na huu ni mwanzo tu mwakani tutafanya mambo mengi zaidi,” alisema Dk. Tulia.
No comments:
Post a Comment