Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii) Bi. Sihaba Nkinga akiongea wakati wa mahafali ya watoto waliokimbia kukeketwa na kujiunga katika kituo Watoto waliokimbia Kukeketwa cha ATFGM-Massanga
NA HASSAN SILAYO-MAELEZO
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bi. Sihaba Nkinga amekemea vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike nchini na kuahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria wale watakaobainika.
Akiongea wakati wa Mahafali ya watoto 46 waliokimbia kukeketwa na kujiunga na Kituo cha kulea watoto hao cha ATFGM Kilichopo Masanga Tarime Vijijini Bi.Sihaba alisema kuwa suala la ukeketaji ni kinyume na sheria za nchi na haki za binadamu na ni suala lenye madhara kwa maisha ya watoto.
“Hatukubaliani na suala hili kwani linarudisha maendeleo ya nchi yetu,suala hili pia linachangia kurudisha fikra za vijana wetu na kubatilisha ndoto za vijana wetu, tunao muda wa kujirekebisha na kama tulikuwa tunaendelea basi turudi nyuma”Alisema Bi. Sihaba.
Katibu Mkuu huyo amesema kuwa jamii inayo wajibu wa kulinda na kuendeleza mila zenye kuleta maendeleo na kuacha kulinda na kukumbatia mila zinathoathiri maisha ya binadamu kwani sio suala sahihi kwani mila nyingine zinagharimu maisha ya vijana wetu.
Akizungumza katika mahafali hayo Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Glorious Luoga amewakemea wazazi watakaothubutu kuwakeketa wasichana wanaotoka katika kituo hicho baada ya mafunzo na wale watakao watakaowatahiri watoto wa kiume kwa mara ya pili baada ya kufanyiwa tohara salama hospitalini.
“Niwaeleze wazazi na walezi, wapo wanaowalazimisha kuwafanyia tohara ya pili watoto wa kiume baada ya kufanyiwa tohara salama, atakayegundulika kufanya tukio hilo tutamshughulikia kwa kumchukulia hatua kali za kisheria ili aone uchungu anaoupata mtoto wakati wanawatahiri kwa mara ya pili” Alisema Mhe. Luoga.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bi. Lydia Bupilipili amewasihi wazazi kuacha tabia ya ukeketaji na kuwapeleka watoto shule ili waweze kutimiza malengo yao kwani kila mtoto ana talanta aliyopangiwa na mungu hivyo kufanya hivyo kuwakeketa na kuwazuia kwenda shule ni kukatisha malengo yao.
Mkurugenzi wa Kituo cha Kulea Watoto waliokimbia Kukeketwa cha (ATFGM-Massanga) Sister Stella Mgaya ameshukuru juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na uongozi wa wilaya ya Tarime kukabiliana na tatizo hilo na kuendelea kuomba wadau kujitokeza kuwaendeleza watoto wanaohitimu kituoni hapo.
“Tunashukuru jitihada za Wilaya ya Tarime wamekuwa nasi bega kwa bega ila tunaomba wadau wengine ikiwemo serikali kwani baada ya mafunzo watoto hawa wamekuwa wakitengwa na familia zao na kuacha kuwapa mahitaji ya msingi hivyo kulazimu kituo kugharamia masomo japo sio kwa kiwango cha kuridhisha” Alisema Sister Mgaya.
Wakisoma Risala kwa mgeni rasmi muwakilishi wa wahitimu hao Magreth Daniel ameiomba serikali kuendelea kuwasaidia hasa baada ya mafunzo na kuepuka kutengwa na familia pia kuendelea kuwachukulia hatua za kisheria wazazi,walezi na mangariba wanaojishughulisha na vitendo vya ukeketaji.
Kituo cha Kulea Watoto waliokimbia Kukeketwa cha ATFGM-Massanga kwa mwaka jana kimepokea watoto 300 kutoka katika maeneo ya Tarime,Rorya,Bunda, Loliondo na baadhi kutoka nchi jirani ya Kenya.
No comments:
Post a Comment