Naibu
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura
akikabidhi bendera kwa nahodha wa timu ya Taifa ya Kuogelea, Hilal Hemed
Hilal
Timu
ya Taifa ya mchezo wa kuogelea, imetamba kufanya vyema katika
mashindano ya Dunia yaliyopangwa kuanza Desemba 6 mjini Windsor, Canada.
Tanzania
itawakilishwa na jumla ya wogeleaji sita ambao wamepatikana kutokana na
michujo mbalimbali ikiwa pamoja na mashindano ya Taifa yaliyofanyika
mwezi Machi mwaka huu kwenye bwawa la kuogelea la Hopac.
Waogeleaji
hao ni Hilal Hilal ambaye ni nahodha, Adil Bharma, Denis Mhini na
Joseph Sumari ambao ni wanaume ambapo kwa wanawake ni pamoja na
muogeleaji namba moja nchini, Sonia Tumiotto na Catherine Mason.
Akizungumza
leo, Hilal alisema kuwa wamejiandaa vizuri chini ya kocha wao, John
Belela na morali ipo juu kutokana na mafanikio waliyopata hivi karibuni
katika mashindano ya kanda ya tatu yaliyofanyika Kigali, Rwanda na
Tanzania kushika nafasi ya kwanza.
Hilal alisema kuwa lengo lao ni kupigia taifa lao na wanaamini watafanya vyema na hasa baada ya kuwaongeza wigo wa waogeleaji.
"Tumejiandaa
kufanya vizuri, kama mjuavyo kwenye mashindano ya Afrika ya kanda ya
tatu Tanzania ndiyo ilikuwa bingwa, tulipata medali 99, ushindani huu
tutakwenda kuuendeleza Canada," alisema Hilal.
Waogeleaji
hao leo walikabidhiwa Bendera ya Taifa na Naibu Waziri wa Habari,
Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura katika hafla fupi
iliyofanyika Wizarani na kuhudhuliwa na Balozi wa Italia hapa nchini,
Roberto Mengoni sambamba na mwakilishi wa kampuni ya kutengeneza vifaa
vya Michezo ya Errea yenye makao makuu nchini Italia.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Naibu Waziri Wambura aliwataka waogeleaji hao
kupambana huku akimuomba Balozi Roberto na kampuni ya Errea kuendelea
kuisapoti Tanzania.
"Ushirikiano
wenu isiishie kwa timu yetu teule ya kuogelea, tunaomba muendelee
kutusapoti hata kwenye miundo mbinu kwa kujenga mabwawa ya kuogelea hapa
nchini na ikiwezekana hata kufungua viwanda vya vifaa vya Michezo,"
alisema Naibu Waziri huku Balozi Roberto akiahidi kushirikiana nao.