Na Dixon Busagaga wa
Globu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini.
Watu zaidi ya 400 wakazi wa mji wa Kahama na viunga vyake wamejitokeza kupima VVU wakati wa mashindano ya Mahusiano Cup ambayo huusisha michezo ya mpira wa miguu na mpira wa pete.
Mashindano hayo ambayo huandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji wa madini ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi yalizinduliwa tarehe moja desemba, yakiwa na lengo la kuhamasisha Jamii kupima afya zao na kuimarisha uhusiano baina ya wenyeji na Mgodi wa Buzwagi.
Akizungumza wakati wa Kuhitimisha fainali za michezo hiyo pamoja na kampeni ya upimaji VVU katika uwanja wa mpira wa Kahama Mji, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama Timothy Ndanya amesema wao kama uongozi wa wilaya ya Kahama wanafarijika na jitihada zinazofanywa na Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi katika harakati za kuhakikisha Jamii inajua afya zao kwa kupima afya na kupanga maisha yao vizuri.
Ameongeza pia jitihada hizo zimekuwa zikionekana kupitia katika sekta ya michezo na hii imekuwa ikijidhihirisha kupitia programu mbalimbali za michezo ambazo zimekuwa zikiendeshwa na Kampuni ya Acacia.
Akizungumzia Mashindano ya Mahusiano Cup ya mwaka huu ambayo yamehusisha timu nyingi zaidi ukilinganisha na miaka iliyopita, Katibu Tawala huyo amesema mashindano ya mwaka huu yamesaidia kuonyesha vipaji vingi vya wanamichezo ambao hapo awali hawakuwa na fursa ya kuweza kuonyesha uwezo wao kupitia michezo.
“Kwetu sisi mmeturahisishia na kwa sababu viongozi wa vyama vya michezo wako wako hapa, hapana shaka watakuwa wamevitambua vipaji ambavyo vimekuwa vikionyeshwa kwa muda wote wa mashindano haya na watatafuta namna nzuri ya kuviendeleza pamoja na kutengeneza timu imara ya halmashauri ya Kahama Mji ambayo itakuwa ikituwakilisha katika michezo mbalimbali” Alisema Timoth.
Kwa Upande wake kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi, George Mkanza amesema michezo ya mwaka huu imekuwa ya mafanikio makubwa sana na kwamba Malengo yake yamefikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Mwaka huu Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi tulikuwa na dhamira ya kuwafikia wakazi wengi wa Kahma kwa njia ya michezo ili kuwapatia elimu juu ya ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kuimarisha Mahusiano yetu na wenyeji wa Kahama, ndio maana utaona mwaka huu michezo hii imefanyika nje ya eneo la kata ya Mwendakulima na kuhusisha timu za tarafa yote ya Kahama Mji” Alisema Mkanza.
Akizungumzia takwimu za upimaji VVU kwa kipindi cha wiki moja ambacho Mashindano hayo ya Mahusiano Cup yalikuwa yakiendelea, Kaimu Meneja Mkuu huyo wa Mgodi wa Buzwagi, amesema jumla ya watu 420 walijitokeza kupima VVU ambapo kati ya hao Wanawake walikuwa 89 sawa na asilimia 21.1% na wanaume 321 sawa na asilimia 76.4%. Ambapo kati ya wote waliopima watu 11 walikutwa na maambukizi sawa na asilimia 2.6%, Wanawake 5 sawa na asilimia 1.19% na wanaume 6 sawa na asilimia 1.42%
Michezo ya Mahusiano Cup ya mwaka 2016 ilifanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Kahama na Uwanja wa Shule ya Msingi Mwendakulima ambapo jumla ya timu kumi na nne za mpira wa mguu zilishiri na timu sita za mpira wa pete.
Timu zilizoshiriki Mpira wa Mguu:- ni kata ya Nyihogo, Nyahanga, Busoka, Kahama Mjini, Zongomela, Malunga, Mhungula, Majengo, Mwendakulima, Ngogwa, Nyasubi, Mhongolo, Wendele, Pamoja na timu ya Mgodi wa Buzwagi, na kwa upande wa Mpira wa Pete:- timu za Kata za Kahama Mjini , Mhungula, Mwendakulima, Mhongolo, Ngogwa na Zongomela zilishiriki mashindano hayo.
Katika michezo hiyo zaidi ya wanamichezo 400 walijitokeza kushiriki ambapo timu za Kahama Mji pamoja na Mhungula ndizo zilizofanikiwa kuingia fainali, ambapo katika mchezo wa fainali timu ya Mhungula iliibuka kidedea kwa kuibamiza timu ya Kahama mji jumla ya goli tatu kwa mbili na kujinyakulia Kombe pamoja na Shilingi milioni moja huku mshindi wa pili timu ya Kahama Mji kuondoka na kitita cha shilingi laki saba na nusu pamoja na kikombe.
Kwa upande wa timu za mpira wa pete zilizofanikiwa kuingia fainali zilikuwa ni timu za Kahama Mji na timu za Zongomela ambapo timu ya Kahama Mji iliibuka Mshindi baada ya kuwafunga wenzao wa kata ya Zongomela jumla ya vikapu 47 dhidi ya 22 na Hivyo kuwafanya timu ya Kahama Mji kuwa Washindi wa Mahusiano Cup kwa upande wa timu za netball kwa Mwaka 2016 na kujinyakulia Kombe pamoja na Shilingi milioni moja huku mshindi wa pili timu ya Zongomela ikiondoka na kitita cha shilingi laki saba na nusu pamoja na kikombe.
Katika mashindano hayo hiyo timu ya Mgodi wa Buzwagi ilishika nafasi ya tatu na kujinyakulia shilingi laki tano kwa upande wa mpira wa miguu na timu ya Netball kutoka kata ya Mwendakuliam ilikuwa mshindi wa tatu kwa upande wa mpira wa pete na kuondoka pia na shilingi laki tano. Huku timu zingine zote zikiambulia kifuta jasho cha shilingi elfu sabini kila timu.
Kabla ya kufanyika kwa fainali hizo mapema asubuhi kampuni hiyo ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi iliandaa pia Bonanza maalumu la Michezo lililowahusisha wadau mbalimbali kutoka ndani ya mji wa Kahama Bonanza lililohusisha michezo kama vile kuvuta kamba, kufukuza kuku na mpira wa miguu.























