Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na
mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Zambia Edgar Lungu (aliyekaa) leo Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Lungu akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa
Jamhuri wa TanzaniaDkt. John Pombe Joseph Magufuli (aliyekaa) leo Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Dkt.
Augustine Mahiga (kushoto) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia
wakisaini makubaliano ya kuwa na Mashauriano ya Kidiplomasia leo Ikulu
Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Dkt.
Augustine Mahiga (kushoto) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia
wakionyesha mikataba ya makubaliano ya kuwa na Mashauriano ya
Kidiplomasia iliyotiwa saini leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
akisalimiana na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania Mhe. Profesa
Sospeter Muhongo mara baada ya kumaliza mazungumzo na waandishi wa
habari akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Zambia Edgar Lungu (nyuma
mwenye tai nyekundu) leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
akisalimiana na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Tanzania Balozi John
Kijazi mara baada ya kumaliza mazungumzo na waandishi wa habari akiwa
na mgeni wake Rais wa Zambia Edgar Lungu (hayupo pichani) leo Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na
mgeni wake Rais wa Zambia Edgar Lungu (mwenye tai nyekundu) wakiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania na Zambia
leo Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha zote na: Frank Shija – MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe.
Edgar Chagwa Lungu leo tarehe 28 Novemba, 2016 wamekubaliana kuchukua hatua za
haraka na madhubuti kuboresha utendaji kazi wa reli ya TAZARA na bomba la
mafuta la TAZAMA ili miradi hiyo miwili ilete manufaa yaliyokusudiwa kwa
wananchi Tanzania na Zambia.
Marais hao
wametangaza kuchukua hatua hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam katika mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika muda mfupi baada viongozi hao kufanya
mazungumzo rasmi ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku 3 ya Rais Lungu iliyoanza
jana hapa nchini kwa mwaliko wa Rais Magufuli.
Katika mkutano huo
uliorushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya redio, tevisheni na mitandao
ya kijamii Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na kuzorota kwa utendaji
kazi wa reli ya TAZARA ambao umeshuka kutoka usafirishaji wa tani 5,000,000 za
mizigo mwaka 1976 hadi kufikia usafirishaji wa tani 128,000 kwa mwaka hivi
sasa, huku utendaji kazi wa bomba la mafuta la TAZAMA nao ukiporomoka kutoka
uwezo wake wa kusafirisha tani 1,100,000 za mafuta hadi kufikia tani 600,000 kwa
mwaka hivi sasa.
Marais hao
wamekubaliana kuwakutanisha wanasheria wakuu wa Serikali za nchi zote mbili
haraka iwezekanavyo kwa lengo la kufanya marekebisho ya kisheria kwa maeneo
yote yaliyoonesha kuwa kikwazo na pia kupanga upya menejimenti za TAZARA na
TAZAMA ili ziweze kuendesha vyombo hivyo kibiashara na kwa manufaa
yaliyokusudiwa wakati vilipoanzishwa na Waasisi wa mataifa haya mawili yaani
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mhe. Dkt. Kenneth Kaunda
wa Zambia.
"Tumekubaliana
ni lazima tubadilike na tubadilike kwa haraka, vikwazo vinavyotokana na sheria
viondolewe na manejimenti ya TAZARA ipangwe upya, na mimi nataka kusema kwa
uwazi, ukiwauliza TAZARA watakwambia tatizo ni mtaji lakini ukweli ni kwamba
tatizo ni menejimenti, ingekuwa tatizo ni mtaji, ule uliokuwepo mwaka 1976 umekwenda
wapi? maana sasa hivi TAZARA ina vichwa 14 tu vya kuendeshea treni na ina
upungufu mkubwa wa mabehewa" amesema Rais
Magufuli.
Kwa upande wake
Rais Lungu amesisitiza kuwa katika kuimarisha TAZARA wamekubaliana kuweka
pembeni siasa na kuirejesha TAZARA katika hali yake ya kibiashara kwa
kuhakikisha inafanya kazi ya kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo
iendayo kusini mwa Tanzania na nchini Zambia.
Mhe. Lungu
ameongeza kuwa pamoja na kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA, Zambia
inatarajia kunufaika na gesi iliyogunduliwa kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania
na pia inajipanga kutumia vizuri fursa ya kufunguka kwa ukanda wa maendeleo wa
Mtwara (Mtwara Corridor) na mpango wa
ujenzi wa reli ya kati ambapo ukanda wa Kaskazini mwa Zambia una mawasiliano ya
karibu na bonde la ziwa Tanganyika.
"Mhe. Rais
Magufuli una muda wa kutosha katika uongozi wako na mimi nina muda wa kutosha
pia, kwa hiyo kwa pamoja tunaweza kuimarisha maeneo yote ya kuinua biashara na
uwekezaji kati ya nchi zetu mbili ikiwemo kuimarisha TAZARA na TAZAMA kwa
manufaa ya wananchi wetu" amesisitiza Rais
Lungu.
Kuhusu hali ya biashara
kati ya Tanzania na Zambia, Rais Magufuli amesema Zambia ni nchi inayoongoza
kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam ambapo katika mwaka 2015
mizigo yenye uzito wa tani Milioni 1.9 ilipitishwa na kwamba kumekuwa na
ongezeko la biashara kati ya Zambia na Tanzania kutoka Shilingi Bilioni 89.2
mwaka 2010 hadi kufikia Shilingi Bilioni 152.2 mwaka 2015.
Dkt. Magufuli
amemhakikishia Rais Lungu kuwa Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya
kufanyia biashara ikiwa ni pamoja na kuboresha zaidi bandari ya Dar es Salaam,
kupunguza vizuizi vya barabarani kutoka 8 hadi 4, kushughulikia tatizo la
vizuizi vya polisi na kujenga Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa
Huduma za Mpakani (One Stop Border Post)
"Tunataka
mambo haya yote yaende haraka, wataalamu wetu ni lazima waharakishe kurekebisha
vikwazo vyote vilivyokuwa vinatuchelewa, tufanye kazi pamoja kwa manufaa ya
wananchi" amesisitiza Rais Magufuli.
Jioni ya leo Rais
Edgar Chagwa Lungu anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na
Mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam na kesho Rais
Lungu anatarajiwa kumaliza ziara yake ya siku 3 hapa nchini.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam