Matukio : Mkuu wa Mkoa Arusha , Mhe. Mrisho Gambo Arejesha Posho - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Thursday, 13 October 2016

Matukio : Mkuu wa Mkoa Arusha , Mhe. Mrisho Gambo Arejesha Posho


Na Woinde Shizza wa 

Globu ya Jamii, Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo leo ametekeleza agizo la Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Joseph Pombe Magufuli la kusitisha safari ya kwenda Mkoani Simiyu kwenye sherehe za kwenda kuhitimisha kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru kwa kurejesha kiasi cha Jumla ya Shilingi 1,389,300 ambayo yalikuwa ni malipo kwa ajili ya Mkuu wa Mkoa, Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa , Dereva wa Mkuu wa Mkoa na gharama za mafuta.

Kwa mujibu wa mchakato wa malipo ya posho kwa safari hiyo ya kwenda mkoani Simiyu kwa siku tatu, posho ya RC ilikuwa ni  Sh 360,000, Msaidizi wa RC Sh 240,000, posho ya dereva 24,000 na Sh 549,300 kwa ajili ya Mafuta ya gari.

Akiongea na mwandishi huyu ofisini kwake leo, Mkuu huyo  wa Mkoa wa Arusha amesema wakati agizo hilo linatolewa yeye alikuwa bado hajaanza safari ya kuelekea Mkoani Simiyu, na kwamba amelipokea bila kinyongo na mara moja akaamua kurejesha posho hiyo, akionesha stakabadhi ya kuthibitisha hilo (pichani).
Pia Rc Gambo ameahidi kusimamia zoezi hilo kwa wahusika wote mkoani Arusha na  kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo kwa wakati na fedha hizo zielekezwe kwenye ujenzi wa madarasa kama sehemu ya maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na darasa la awali kwa mwaka 2017.
Rais Dkt. Magufuli  jana aliagiza viongozi wote wa Serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao walishalipwa fedha ya posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.
Rais Magufuli alitoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Viongozi waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na Wakuu wote wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameya na Wenyeviti wote wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.
Kwa kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.
Aidha, Rais Magufuli aliagiza kuwa Wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha Mbio za Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.

Hata hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na Wilaya zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016.

Mgeni Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein

No comments:

Post a Comment