Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka
(Katikati) akizungumza na Viongozi wa Mkoa huo na Wajumbe wa Kamati za Fedha,
Mipango na Uongozi kutoka katika Halmashauri za Mkoa huo katika kikao
kilichofanyika Mjini Bariadi, kujadili mikakati ya ujenzi wa vyumba vya
madarasa, (kushoto) Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne A. Sagini na (kulia)
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, mhe. Festo S. Kiswaga
Wakuu wa Wilaya wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu (hayupo pichani) katika kikao cha kujadili mikakati ya ujenzi wa vyumba
vya madarasa mkoani humo, mstari wa kwanza kutoka kushoto, Mhe. Benson Kilangi
(Itilima), Joseph Chilongani (Meatu), Seif Shekalaghe, Tano Mwera (Busega) na
mstari wa pili, kutoka kushoto, Mhe. Stanslaus Nyongo(Mbunge Maswa Mashariki),
Mhe. Mashimba Ndaki (Mbunge Maswa Magharibi).
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne A. Sagini
akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka
(kulia) ili azungumze na Viongozi wa Mkoa huo na Wajumbe wa Kamati za Fedha,
Mipango na Uongozi kutoka katika Halmashauri za Mkoa huo, katika kikao
kilichofanyika Mjini Bariadi, kujadili mikakati ya ujenzi wa vyumba vya
madarasa.
Viongozi na baadhi Wajumbe wa Kamati za Fedha, Mipango na Uongozi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) katika kikao cha kujadili mikakati ya ujenzi wa vyumba vya madarasa mkoani humo kilichofanyika Mjini Bariadi. |
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
Maswa, Mhe. Dila Mayeka akitoa mchango wake wa mawazo katika
kikao cha kujadili mikakati ya ujenzi wa vyumba vya madarasa mkoani humo, kilichofanyika
Mjini Bariadi
Na Stella Kalinga
Serikali Mkoani Simiyu
imesema asilimia mbili ya ushuru wa zao
la pamba inayopatikana katika Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu ielekezwe
katika ujenzi wa Miundombinu ya elimu ya msingi na sekondari,hususani vyumba
vya madarasa.
Uamuzi huo
umefikiwa kufuatia majadiliano ya pamoja kati ya Uongozi wa Mkoa na Halmashauri
zote katika kikao kilichoongozwa na Mkuu
wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka akiwa na Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa
Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala Wilaya na Wajumbe wa
Kamati za Fedha za Halmashauri ili kujadili mstakabali wa ujenzi wa vyumba vya
madarasa katika mkoa huo.
Mtaka amewaelekeza
Wakurugezi wote wakafanye uhakiki na kuainisha takwimu sahihi za mahitaji ya vyumba vya madarasa ili kupata
uhakika wa vyumba vinavyohitajika katika mkoa mzima na kupanga mkakati wa namna
vyumba hivyo vitakavyojengwa ikiwa ni pamoja na teknolojia itakayotumika katika
kufyatua matofali pamoja na gharama zake
na kuwasilisha taarifa katika Ofisi yake tarehe 9 Agosti, 2016, ambapo baada ya
kupata taarifa hiyo na kujiridhisha zoezi la ufyatuaji matofali kimkoa
litazinduliwa rasmi Wilayani Maswa tarehe itakayopangwa na mkoa.
“ Sina uhakika
sana na takwimu hizi, niwaagize tena Wakurugenzi wote mkafanye mapitio upya na uhakiki
wa kina katika maeneo yenu juu ya idadi ya vyumba vya madarasa vinavyohitajika
kwa Elimu ya Msingi na Sekondari. Mkae na wataalam wenu wa ujenzi mfanye
tathmini ya namna mtakavyojenga kama mtatumia matofali ya kuchoma, matofali ya
block au matofali yakufungamana (interlocking blocks) yanayofyatuliwa na vijana
waliopewa mafunzo na Shirika la Nyumba la Taifa,ambao wako katika kila halmashauri
pamoja na gharama zitakazotumika”, alisema Mtaka.
Kwa upande wake
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amewataka Wakurugenzi kufanya utaratibu
wa kubadilisha matumizi ya fedha haraka pale inapobidi kwa kufuata sheria kanuni na
taratibu kufanikisha zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwatengenezea
wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunzia na kuwezesha madawati yaliyotengenezwa
ambayo hayana mahali pa kuwekwa yasiharibike kwa kupigwa na jua na kunyeshewa
na mvua.
Pamoja na
kutenga asilimia mbili ya ushuru wa pamba, Mtaka amesema Mkoa unakusudia
kufanya Harambee kubwa itakayowashirikisha viongozi na wadau wengine muhimu
kutoka ndani na nje ya mkoa ambao watachangia kwa kuunga mkono jitihada za
Serikali Mkoani humo, katika kuondoa tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa kwa
Mkoa wa Simiyu.
Akichangia hoja
hiyo ya harambee Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi , Mhe.Mashimba Ndaki
amesema, hiyo itakuwa ni fursa kwa wenyeji wa Mkoa wa Simiyu walo ndani na
nje kuchangia maendeleo ya Mkoa wao na
akasisisitiza fedha zitakazokusanywa zisimamiwe vizuri na viongozi.
Katika hatua
nyingine Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amekabidhi simu tano kwa Wakuu wa Wilaya tano
za Mkoa huo zilizotolewa na idara ya mahakama kwa lengo la kutekeleza mpango
wa mapambano dhidi ya rushwa na vitendo
vinavyokwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma katika utoaji wa huduma za
Mahakama, ambazo zitagawanywa kwa maafisa wa dawati la malalamiko kwa kila
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na akaelekeza zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, Mtaka
amewataka Wakuu wa Wilaya kutenga siku maalum ya kusikiliza kero za wananchi ambayo
Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa
Halmashauri watakaa kuwasilikiliza wananchi
na kuwapatia ufumbuzi na pale inaposhindikana masuala yao yapelekwe
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya hatua zaidi.
No comments:
Post a Comment