Matukio : Zulmira Ataka kazi kwa pamoja kuhami maeneo ya urithi wa Dunia - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


27 Jun 2016

Matukio : Zulmira Ataka kazi kwa pamoja kuhami maeneo ya urithi wa Dunia


Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues amewakumbusha wadau wa urithi wa dunia na maeneo ya hifadhi kufanyakazi kwa pamoja kwa lengo la kuhifadhi na kuyaendeleza maeneo hayo bila kuondoa ushiriki wa wananchi wanayozunguka.

Kauli hiyo ameitoa katika mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika lake kwa wadau wa mazingira ya hifadhi na urithi wa dunia mjini Marangu Moshi, kufuatia makubaliano na serikali ya Tanzania.

Alisema akizungumza na washiriki kwamba UNESCO inachofanya ni kuanzisha safari ambayo inaweza kuwa ngumu na ndefu lakini washiriki wake ni lazima kutambua namna ya kuendelea kufanya menejimenti ya maeneo ya hifadhi na urithi wa dunia kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akifungua mafunzo hayo ambayo wataalamu ni washiriki wenyewe wakitumia njia ya kuelewa ya methodolojia ya uchambuzi wa vikwazo (Bottleneck Analysis Methodology) alisema safari ya kufanikisha menejimenti ya maeneo hayo duniani na hasa hapa nchini ni yenye changamoto nyingi na kwamba wadau wote wanatakiwa kuwa pamoja kuvishinda vikwazo hivyo na kuifanikisha safari.

Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akizungumza katika warsha ya siku tatu iliyoandaliwa na shirika lake kwa wadau wa mazingira ya hifadhi na urithi wa dunia iliyomalizika mwishoni mwa wiki mjini Marangu, mkoani Kilimanjaro.(Picha zote na Zainul Mzige)

Akizungumza katika warsha hiyo ambayo imechukua wadau mbalimbali wa masuala ya urithi na menejimenti zake kutoka serikalini, taasisi zisizo za kiserikali na wananchi wengine, alisema kwamba maeneo hayo yamezungukwa na wananchi na pamoja na kuwawekea sheria za kutoharibu na kuyachakaza ipo haja ya kushirikiana nao namna ya kupanga kuyaendeleza maeneo hayo huku yakiwa yamebaki katika hali inayotakiwa.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wa kupanga maendeleo katika maeneo ambayo ni ya urithi wa dunia, binadamu na maeneo ambayo uhai unaweza kuwepo.

Aidha akifafanua zaidi mtawala huyo wa UNESCO nchini Tanzania amesema mafunzo hayo yamelenga kuwapa wahusika nadharia zinazofaa katika safari ndefu ambayo UNESCO nayo itashiriki na isingelipenda kumwacha hata mtu mmoja nyuma.

Mafunzo hayo yanatolewa kufuatia mpango wa UNESCO wa kutaka kuwa na uhakika na kuhami maeneo hayo ya urithi; huku mamlaka zikitoa ushirikiano ili kuwezesha malengo ya maendeleo endelevu, ambayo ndiyo ajenda ya dunia kuelekea 2030, yanafikiwa bila kuathiri maeneo tajwa.
Ofisa anayeshughulikia watu na maeneo yenye uhakika wa uhai: Biashara zinazozingatia mazingira na uchumi unaombatana nao kutoka Sekta ya Sayansi Ofisi ya Unesco, Dar es salaam, Myoung Su Ko akiwasilisha mada kwa washiriki wa warsha hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Kilimanjaro Resort mjini Marangu, mkoani Kilimanjaro.

Alisema kwa kuwa kitaifa, serikali imeshatoa matamko ya kisera na kuweka mikakati ya utekelezaji wa taratibu za kuhami maeneo ya kiutamaduni na ya asili ipo haja ya wadau wengine kuona namna ya kufanyakazi kama timu katika safari ambayo kila mmoja anastahili kuwaijibika kwa namna yake hata kama kunatokea changamoto.

Alisema wadau wanatakiwa kuangalia namna ya safari zao zinavyostahili kufanywa na kuwa, kwa lengo la kutumia raslimali zilizopo kutekeleza mipango ya maendeleo na ya kuhami maeneo hayo bila kutegemea msaada wa wafadhili au wahisani.

Awali katika ujengaji wa wazo la mafunzo ilielezwa kuwa pamoja na kuwapo na juhudi kubwa za kuhami maeneo ya urithi wa dunia na kuyasajili maeneo ambayo uhai unaweza kuwapo na wanadamu, kumekuwepo na changamoto kubwa za maendeleo ambazo zinatishia kuvuruga mfumo tete wa ikolojia uliopo.

Katika kufanikisha hifadhi ya maeneo hayo kumeonekana changamoto za upungufu wa rasilimali watu wenye uwezo na vifaa vya kushughulikia uharibifu, ukosefu wa uwezo wa kuhifadhi maeneo hayo kwa kuoanisha na uwapo wa watu.
Mtaalamu wa programu na utamaduni kutoka Ofisi za Unesco Afrika Mashariki Bi. Karalyn Monteil akiwasilisha mada kuhusu makubaliano ya ulinzi katika maeneo ya urithi na utamaduni wa dunia katika warsha hiyo iliyomalizika mwishoni mwa juma mjini Marangu, Moshi.

Mathalani eneo la Urithi la Kilimanjaro lina changamoto kubwa ya uwezo kiasi ya kwamba mazingira yanaharibiwa huku wakazi wa maeneo hayo wakiwa hawashirikishwi katika maamuzi ya kulinda eneo hilo na hivyo kutojitambua kwamba wao ni kiungo muhimu katika maendeleo na utalii ambao ungewaingizia mapato.

Kutokana na kutoshirikishwa baadhi ya mambo wanayofanya wananchi yanakwenda kinyume na nadharia nzima ya uhifadhi wa maeneo hayo.

Inatarajiwa baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo washiriki watakuwa wamepata uelewa wa mbinu zinazostahili kutumika katika kuwashirikisha na kuhifadhi maeneo hayo huku ajenda za kidunia za maendeleo endelevu zikiendelea kufanywa.
Aidha watakuwa wameelewa mbinu mbalimbali zinazoweza kutumika kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya urithi na yale ambayo yamehifadhiwa kwa kuwa uhai unaonekana kuwapo. Aidha mameneja watakuwa na uwezo wa kutambua haja ya ushiriki na ushirikishi katika mipango ya maendeleo na hifadhi pale walipo.Warsha hiyo imemalizika Juni 25.
Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akiendelea kuwapiga msasa wadau na mameneja wa mazingira ya hifadhi na urithi wa dunia katika warsha ya siku tatu iliyofanyika mkoani KIlimanjaro.
Pichani juu na chini ni washiriki wakitoa maoni katika warsha ya siku tatu kwa wadau wa mazingira ya hifadhi na urithi wa dunia iliyomalizika mwishoni mwa juma mjini Marangu, Moshi.

Ofisa Utamaduni wa Shirika la UNESCO, Dar es Salaam, Michaela Konopikova (kulia) akiteta jambo na Mtaalamu wa programu na utamaduni kutoka Ofisi za Unesco Afrika Mashariki Bi. Karalyn Monteil wakati warsha ya siku tatu kwa wadau wa mazingira ya hifadhi na urithi wa dunia iliyoandaliwa na UNESCO, mjini Marangu, mkoani Kilimanjaro.
Sehemu ya wadau wa mazingira ya hifadhi na urithi wa dunia waliohudhuria warsha ya siku tatu iliyoandaliwa na UNESCO, mjini Marangu, mkoani Kilimanjaro.

Mtaalamu wa programu na utamaduni kutoka Ofisi za Unesco Afrika Mashariki Bi. Karalyn Monteil akifafanua jambo kwa washiriki wa warsha hiyo. Kulia ni Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues
Ofisa Maliasili wa Mkoa waKilimanjaro, Emanuel Kiyengi akipitia moja ya makabrasha yanayoonesha maeneo ya urithi wa dunia katika washa hiyo ya siku tatu iliyomalizika mwishoni mwa juma mjini Marangu, mkoani Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad