Matukio : Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa ataka watoto wenye ulemavu kupatiwa elimu - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


23 Apr 2016

Matukio : Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa ataka watoto wenye ulemavu kupatiwa elimu

Habari na picha na  John Nditi, Morogoro
WAZAZI na walezi wenye watoto wenye ulemavu wilayani Mvomero , mkoa wa  Morogoro wametakiwa kuwapeleka shule ili waweze kupata elimu itakayokuwa ni mkombozi wao kwa maisha yao ya baadaye katika kujiletea maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi,  imeelezwa.

Rai hiyo ilitolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, George Jackson Mbijima ,Aprili 20, 2016  wakati wa uzinduzi wa Darasa la watoto wenye ulemavu , katika kijiji cha Changarawe, Kata ya Mzumbe , wilayani humo. 
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru , Mbijima , alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi na jamii kwa ujumla, kuwapeleka watoto wenye ulemavu katika shule hiyo kwa kuwa elimu pekee ndiyo itakayowakomboa.
“ Serikali ya Tanzania imeweka mazingira mazuri ya kusoma kwa watoto wa makundi yote wakiwemo wenye ulemavu wa aina mbalimbali , kwani elimu pekee ndiyo mkombozi wao katika suala la kujitegemea siku za usoni...hivyo jamii itambua hilo na kuwajali watoto wenye ulemavu na si kuwaficha majumbani” alisema Mbijima.
Naye Mwalimu wa  darasa la  watoto wenye ulemavu katika shule ya Msingi ya Changarawe ,  Doreen Msuya, aliiomba serikali ya Wilaya, mkoa na Serikali kuu, kuona uwezekano wa kujenga hosteli ya watoto wenye ulemavu katika eneo la shule hiyo.

Msuya alisema , hatua hiyo itawezesha watoto wengi wanaoshindwa kufika kutokana na ulemavu wao waweze kuishi karibu na shule na kunufaika na elimu ambayo itawasaidia katika maisha yao baadae.
Hivyo alisema , mradi huo wa darasa la wanafunzi wenye mahitaji maalumu ulianzishwa mwaka 2013 baada ya kufanyika sense ya watoto wenye mahitaji maalumu na kubaini watoto 26 ambao kwa kipindi hicho walikauwa majumbani ingawa umri wa kuanza shule ulikuwa umefika.
 Msuya alisema , mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana kati ya halmashauri ya wilaya ya Mvomero na wanajamii wa kijiji cha Changarawe ambao hadi sasa wanafunzi 42 wapo darasani , kati ya hao wavulana 27 na wasichana 15.
“ Kupitia mradi wa darasa hili umeweza  kuibua watoto sita waliokuwa wamefichwa  nyumbani  ambao ni wenye ulemavu wa aina mbalimbali” alisema Msuya.

“ Kuazishwa kwa darasa la watoto wenye ulemavu katika shule hii ya Changarawe  kumesaidia  kuibuliwa ndani ya jamii watoto wa aina hiyo waliokuwa  mitaani na nyumbani bila ya matumaini yeyote ya baadaye “ alisisitiza Mwalimu Msuya.

Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake , mwanafunzi wenye ulemavu , Steven Petro (14) wa darasa la tano shuleni hapo, kuanzishwa kwa darasa hilo kumewawezewa wao kupata elimu na hivyo kuwa na matarajio mazuri ya siku za usoni.
Naye mkuu wa wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa, alihimiza wazazi kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kuandikishwa shule ya awali na msingi ikiwa na kuwandeleza hadi elimu ya juu kwa vile elimu ndiyo ufunguo wa maisha.
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika wilaya ya Mvomero  ulipitia, kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kuonwa  miradi  mitano ya maendeleo yenye thamani zaidi ya Sh  milioni 688.6 ukiwemo  wa  darasa la watoto wenye mahitaji maalumu.
Tayari Mwenge wa Uhuru umemaliza mbio zake katika Manispaa ya Morogoro, halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Mvomero , Ulanga na Kilombero tangu ulipozinduliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan , Aprili 18, mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri wa Morogoro.

 Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Ulanga , mkoa wa Morogoro wakifuatilia jambo wakati wa ugeni wa Mwenge wa Uhuru .
 Kikundi cha Wanawake cha Mvomero kikionesha bidhaa zao.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa , George Jackson Mbijima akifuatana na Mkuu wa wilaya ya Mvomero, mkoa wa Morogoro, Betty Mkwasa  kuangalia bidhaa za kikundi cha wanawawake.
 Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Jackson Mbijima akimkabidhi hati kwa klabu ya wapinga rushwa ya Twikale wose  Lugono, Mwenyekiti wa klabu , Kondo Mahawa.
 Mgangazaji wa TBC Swedi Mwinyi , ( kati kati ) akiwa pamoja na mshereheshaji mwenzake ( kushoto) wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge  wa Uhuru 2016, uwanja wa Jamhuri wa Morogoro.  
 Mjasilimali wa Kimasai  akiwa na  Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa pamoja  na mkuu wa wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa.
 Mkuu wa Takukuru wilaya ya Mvomero, mkoa wa Morogoro, Eufrasia Kayombo ( kushoto) akisaini hati ya uzinduzi wa klabu ya wapinga rushwa Twikale wose , Lugono kilichopo wilaya ya Mvomero.
 Mkuu wa wilaya ya Mvomero, mkoa wa Morogoro, Betty Mkwasa akiwa ameushika Mwenge wa Uhuru , baaada ya kukabidhiwa na Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Muhingo Rweyemamu ( hayupo pichani).
 Mkuu wa wilaya ya Ulanga, mkoa wa Morogoro, Christina Mndeme, ( kulia) akimkabidhi Mwenge wa Uhuru mkuu wa wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe ( kushoto),kuanza mbio zake Aprili 22, 2016
Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa , wakitoka  kuweka  jiwe la msingi jengo la kuhifadhia dawa na vifaa tiba katika hospitali ya wilaya ya Ulanga.
 Mmoja wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa akiwa ameubeba Mwenge wa Uhuru, baada ya kuvuka katika kivuko cha Mv Kilombero 11 kutokea wilaya ya Ulanga. (1)
Mwanafunzi mwenye ulemavu wa viungo, Steven Petro  wa darasa la tano shule ya Msingi Changarawe, wilaya ya Mvomero akisoma risala.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad