Mhandisi
wa Baraza la Manispaa Mzee Juma Khamis wa kwanza kutoka kulia akimpatia
maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefanya ziara
kuangalia baadhi ya Mitaro iliyosababisha mafuriko kufuatia mvua kubwa
zinazoendelea kunyesha hapa nchini.
Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed na Kaimu Mkurugenzi wa Baraza
la Manispaa Nd. Said Juma Ahmada.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili a Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Abdoud
Mohammed akimueleza Balozi Seif hatua zilizokwisha chukuliwa na
watendaji wa Kamati ya Maafa katika kunusuru maafa yaliyojitokeza ndani
ya kipindi cha mvua zilizoleta athari kubwa.
Balozi
Seif akiwafariji Baadhi ya Wananchi wa Mitaa ya Kwahani, Kwawazee na
Sebleni ambao nyumba zao zimeathirika kwa mvua zilizonyesha usiku wa
kuamkia Jumapili.
Skuli
ya Nyerere Sekondari ni miongoni mwa skuli zinazotoa huduma ya muda ya
kuwahifadhi watu walioathirika na mvua kubwa za juzi ambapo Balozi Seif
alipata wasaa wa kuwatembelea kwa kuwapa pole.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajiandaa rasmi kutoa viwanja vya ujenzi
wa nyumba za kudumu kwa Wananchi wanaoendelea kukumbwa na maafa ya
mafuriko wakati wa kipindi cha msimu wa mvua za masika hapa Nchini.
Kauli
hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alipofanya ziara katika maeneo mbali mbali yaliyoathirika na mvua
kubwa zilizofurika usiku wa kuamkia Jumapili na kuleta athari kubwa kwa
Wananchi hasa katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Balozi
Seif ambae aliambatana na Viongozi wa Kamati ya Taifa ya kukabiliana na
Maafa Zanzibar kwa kuangalia mitaro wa uwanja wa Mnazi Mmoja, Kwa
Binti Hamrani Mpendae pamoja na Bwawa na Sebleni Kwawazee hata hivyo
alisema baadhi ya wananchi wanaopewa viwanja huamua kuviuza na baadae
kurejea katika maeneo wanayohamishwa bila ya kuzingatia usalama wao.
Alisema
kutokana na athari za mara kwa mara zinazoendelea kuwakumba wananchi
katika maeneo mbali mbali nchini kutokana na majanga ya mafuriko ya mvua
wakati umefika kwa wanaopewa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
kudumu kuzingatia mipango miji ili kujikinga na athari zinazoweza
kuepukika.
Balozi
Seif alitanabahisha kwamba ujenzi usiozingatia mipango miji matokeo
yake huleta adha, hasara na mashaka, na si vyema tabia hiyo ikaendelezwa
wakati jamii inatambua athari inayoweza kujitokeza.
Mapema
Mhandisi wa Baraza la Manispaa Zanzibar Nd. Mzee Juma Khamis alimueleza
Balozi Seif kwamba maji yaliyotuwama katika mtaro wa Uwanja wa Mnazi
Mmoja yataondoshwa mara baada ya kupunguwa kwa kina cha maji ya bahari.
Mhandisi
Mzee alisema maji ya bahari hivi sasa yako juu hali iliyopelekea
kufungwa kwa mlango wa kutolewa maji ya mvua yaliopo kwenye Uwanja huo
kuelekezwa pwani jambao ambalo limekwamisha utoaji wa maji hayo.
Akizungumzia
mtaro wa Kwa binti Hamrani Mhandisi huyo wa Baraza la Manispaa
alimueleza Balozi Seif kwamba kazi za uendelezaji wa mtaro huo
zimesimama kutokana na tatizo la baadhi ya nyumba zilizopo kwenye eneo
linalokusudiwa kupitishwa mtaro huo.
Alisema
kazi hiyo inaweza kuendelea tena baada ya wananchi wanaomiliki nyumba
hizo kufanyiwa tathmini ya nyumba zao ili walipwe fidia na baadae
kupisha ujenzi huo.
Katika
ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata wasaa
wa kuwafariji Wananchi wa Mitaa ya Kwahani, Kwawazee na Nyerere ambao
wamehifadhiwa kwa muda katika skuli ya Sekondari ya Nyerere kwa Wazee.
Akiwapa
pole wahanga hao Balozi Seif aliwaomba wananchi hao kuzingatia usafi wa
mazingira kwa kulinda afya zao na hasa watoto wao wadogo ili kujiepusha
na maambukizo ya maradhi kama kipindi pindu.
Naye
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed
Aboud Mohammed alisema taratibu za kuwahifadhi wananchi walioathirika na
mvua hizo zimeshakamilishwa na Serikali Kuu.
Mh.
Aboud alisema Kamati ya Kukabiliana na Maafa tayari imeanza kupokea
wananchi waliopata maafa ya mvua kwa kuwahifadhi katika skuli ya
Sekondari ya Mwanakwerekwe “C ” ambapo eneo hilo liko salama kwa
maazingira na afya zao.
Mwakilishi
wa Timu ya Msalaba mwekundu { Action Team }inayotoa huduma kwa wahanga
waliopo katika skuli hiyo ya Nyerere Shaaban Ali Iddi alisema timu yao
inaendelea kutoa elimu ili kuwasaidia wananchi hao kujiepusha na
maradhi ya matumbo.
Wakati
huo huo Balozi Seif alikabidhi msaada wa vyakula mbali mbali ili
kuwasaidia wahanga wa mafuriko hao wanaopata hifadhi ya muda katika
skuli ya Sekondari Nyerere.
Msaada
huo wa maji, maharage, mchele, sukari, sembe pamoja na mafuta ya
kupikia umetolewa kwa pamoja na Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Amani
Mwalimu Mussa Hassan Mussa na Mh. Rashid Ali Juma.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
18/4/2016.
No comments:
Post a Comment