Mtendaji
Mkuu wa Mahakama Bw. Hussein Katanga (katikati) akisisitiza jambo
wakati wa kikao cha Mrejesho wa Wadau walioshiriki katika utoaji wa
Elimu ya Sheria kwa wananchi Februari 1 hadi 3, 2016 katika viwanja vya
Mnazi mmoja, jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu Mahakama
Kuu, Solanus Nyimbi na Kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John
Lugalema Kahyoza.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho akitoa mchango wake kuhusu uboreshaji wa huduma ya Mahakama.
Msajili
wa Mahakama ya Rufaa, John Lugalema Kahyoza akizungumza na Wadau
walioshiriki katika utoaji wa Elimu ya Sheria kwa wananchi Februari 1
hadi 3, 2016 katika viwanja vya Mnazi mmoja, jijini Dar es salaam.
Washiriki
wa kikao cha Mrejesho wa Wadau walioshiriki katika utoaji wa Elimu ya
Sheria kwa wananchi Februari 1 hadi 3, 2016 katika viwanja vya Mnazi
mmoja, wakifuatilia kikao hicho leo jijini Dar es salaam.
Na Aron Msigwa – Dar es salaam.
Mahakama
ya Tanzania imesema kuwa inaendelea na mkakati wa kufanya maboresho ya
miundombinu yake ili kurahisisha utoaji wa huduma ya mahakama kwa wadau
na wananchi kwa wakati.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mtendaji Mkuu Mahakama ya
Tanzania Bw. Hussein Katanga wakati wa kikao cha Mrejesho wa Wadau
walioshiriki katika utoaji wa Elimu ya Sheria kwa wananchi Februari 1
hadi 3 mwaka huu katika viwanja vya Mnazi mmoja, jijini Dar es salaam.
Bw.
Katanga amewaambia wadau hao kuwa Mahakama ya Tanzania inaendelea
kufanya mabadiliko ya huduma zake kutokana na ushirikiano mkubwa
inaoupata kutoka Serikalini pia kutoka kwa wadau wa Haki wanaoiwezesha
Mahakama kufanya maboresho hayo kwa lengo la kukuza Utoaji wa Haki
nchini.
Amesema
ili kusogeza huduma karibu na wananchi Mahakama itatekeleza Mpango
mkakati wa miaka 5 wa kuiwezesha kushirikiana kwa karibu zaidi na wadau
na Taasisi za utoaji Haki katika masuala yanayohusu shughuli za kila
siku za utendaji wa Mahakama nchini.
“
Mahakama tutaanzisha mpango wa miaka 5 ambao utaanzisha mfumo wa wa
kushirikiana na wadau wetu kwa karibu katika mambo yanayohusu shughuli
zetu ili kuwaondolea wananchi usumbufu na upotevu wa muda pindi
wanapofuatilia huduma” Amesema.
Amefafanua
kuwa Mahakama imeshaanza kujenga majengo mapya ya kisasa ya Mahakama za
Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mahakama ya mwanzo
Kigamboni jijini na Kawe zote za jijini Dar es salaam, Mahakama ya
Wilaya ya Mkuranga na Kibaha mkoani Pwani ili kurahisisha utoaji wa
Haki.
“
Mahakama sasa tuko katika mwelekeo mzuri wa kufanya mabadiliko, kwa
kushirikiana na wataalam wetu wa ndani wakiwemo Chuo Kikuu Ardhi ,
tunaendelea kujenga majengo mapya ya Mahakama katika maeneo mbalimbali
nchini ikiwemo Mahakama ya Mwanzo Kigamboni, Mkuranga, Kibaha na Kawe
ambayo yatakamilika ifikapo Juni mwaka huu” Amesisitiza.
Bw.
Katanga ameongeza kuwa mpango uliopo ni kuhakikisha kuwa majengo
yaliyopo yanakarabatiwa sanjali na ujenzi wa majengo mapya katika
Mahakama zote 133 nchi nzima.
Aidha,
amebainisha kuwa Mahakama inaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa
watumishi wake ikiwemo ununuzi wa mabasi ya kusafirishia watumishi,
magari madogo na Pikipiki ili kuwawesha watumishi wa Mahakama kutekeleza
majukumu yao ipasavyo.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu Solanus Nyimbi akizungumza na
wadau hao amewataka wafanye kazi kwa kushirikiana katika kuwahudumia
wananchi ili kuongeza imani yao kwa Mahakama.
Amezitaka
Taasisi na wadau wanaohusika na utoaji wa Haki kujikita katika
kushughulikia matatizo ya wananchi ili kufanikisha dhana ya Utoaji Haki
kwa Wakati ili kwenda na mpango uliowekwa na Mahakama wa kuondoa
mrundikano wa mashauri mahakamani na ule wa kuzifuta kesi zilizokaa muda
mrefu.
Naye
Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John Lugalema Kahyoza ametoa wito kwa
Taasisi za Utoaji wa Haki kukutana mara kwa mara ili kujdili na kutatua
changamoto zinazoukabili Utoaji wa Haki nchini.
No comments:
Post a Comment