Mfululizo
mpya wa makala zilizochapishwa na The Lancet unatoa ushahidi kuwa
kuboresha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kunaweza kuokoa maisha ya zaidi
ya watoto 820,000 kila mwaka duniani na Dola za Kimarekani bilioni 300
kila mwaka.
“Katika
kipindi cha miaka iliyopita kumekuwa na maendeleo katika kupunguza vifo
vya watoto na utapiamlo nchini Tanzania. Hata hivyo, watoto 270 chini
ya miaka mitano wanakufa kila siku na karibu asilimia 40 ya watoto hao
wanakufa ndani ya mwezi mmoja wa kuishi. Kati ya watoto wanaonusurika,
mtoto mmoja kati ya watatu wanadumaa kwa sababu ya utapiamlo sugu.
Watoto
hawa wanakosa fursa zao katika maisha. Hali duni ya lishe inaathiri
uwezo wa mtoto kujifunza na pia uwezekano wa mtoto huyo kutengeneza
kipato akiwa mtu mzima. Lakini kuna afua zinazojulikana zinazoweza
kusababisha mabadiliko makubwa na kuhamasisha kunyonyesha maziwa ya
mama. ” amesema Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Bibi Maniza Zaman,
wakati akiongea na vyombo vya habari Dar es Salaam. “Mfululizo wa
makala ya “The Lancet” unatoa ushahidi wenye ushawishi kuhusu faida
mbalimbali za kunyonyesha. Uwekezaji kwenye kulinda, kukuza, na kusaidia
unyonyeshaji maziwa ya mama kunaweza kuokoa maisha ya watoto wa
Tanzania, na hatimaye, kusaidia kukuza uchumi.”
Makala
za “The Lancet” zinaonyesha kuwa kuna faida nyingi za kiafya za
kunyonyesha maziwa ya mama. Unyonyeshaji maziwa ya mama kwa kiasi
kikubwa sana kunaweza kuzuia karibu nusu ya matukio ya kuhara na
theluthi moja ya maambukizo ya njia ya hewa– zikiwa ni sababu mbili
zinazoongoza kupelekea vifo kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama kwa kawaida wanahitaji kupelekwa
hospitali mara chache zaidi na kuwa na uwezekano mdogo wa kupata
maambukizo na magonjwa, pia wana uwezekano mdogo zaidi wa kuwa na uzito
mkubwa na kupata kisukari baadaye maishani mwao.
Kuna
faida za kiafya kwa mama pia. Kwa kila mwaka ambao mama ananyonyesha,
uwezekano wa kupata saratani ya matiti ya hatua ya pili unapungua kwa
asilimia 6. Viwango vya sasa vya kunyonyesha maziwa ya mama tayari
vinazuia vifo karibu 20,000 vinavyotokana na saratani ya matiti kila
mwaka duniani – idadi hii inaweza kuwa kubwa zaidi kwa kuboresha mbinu
za unyonyeshaji wa maziwa ya mama. Pia kunyonyesha kwa muda mrefu zaidi
kumehusishwa na kupungua kwa saratani ya mfuko wa mayai.
Kuongeza
viwango vya unyonyeshaji maziwa ya mama katika jamii kuna faida za
kiuchumi. Watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama wanapata matokeo mazuri
zaidi kwenye vipimo vya upeo wa kiakili. Kimataifa, imekadiriwa kuwa
gharama zinazotokana na kuwepo na watoto wenye upeo mdogo zaidi wa
kikakili unaohusishwa na kutonyonyeshwa maziwa ya mama ni jumla ya
takriban dola za kimarekani bilioni 300 kwa mwaka. Nchi zenye kipato cha
chini na kipato cha wastani zinapoteza zaidi ya dola za kimarekani
bilioni 70 kila mwaka. Nchi zenye kipato cha juu zinapoteza zaidi ya
dola za kimarekani bilioni 230 kila mwaka.
Hata
hivyo, hapa Tanzania kuna mikoa inayooyesha mwelekeo unaotia moyo. Kwa
mfano, mkoa wa Kilimanjaro, Tanga na Iringa ina asilimia 75 ya watoto
wananyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa. Zaidi
ya nusu ya watoto wenye umri wa miezi 0-5 wananyonyeshwa maziwa ya mama
pekee katika miezi 6 ya mwanzo wako katika mikoa ya Iringa, Kigoma,
Morogoro, Singida, Katavi na Geita, huku Kagera ikiwa na kiwango kikubwa
zaidi cha asilimia 70.
Ili
kuimarisha jitihada za kitaifa za kuboresha unyonyeshaji maziwa ya mama,
vikwazo vinavyowakabili wanawake wengi duniani kote pia vinapaswa
kushughulikiwa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na:
• Mapungufu kwenye uelewa wa watoa huduma ya afya ambayo yanawaacha wanawake bila taarifa au msaada sahihi;
• Kukosekana
kwa mifumo imara ya msaada kwenye familia na jamii, pamoja na mila na
tamaduni zisizounga mkono kunyonyesha maziwa ya mama; na
• Likizo
ya uzazi ya muda mfupi au kutokuwepo kabisa kwa likizo hiyo. Likizo ya
uzazi ya muda mfupi inaweza kuongeza uwezekano wa kutonyonyesha maziwa
ya mama au kuacha kunyonyesha maziwa ya mama mapema kwa asilimia 400;
Jambo
lingine ni uuzaji usiofaa wa vyakula mbadala vya maziwa ya mama (ikiwa
na pamoja na maziwa ya kopo kwa ajili ya watoto wachanga) na
watengenezaji na wasambazaji ambao hutoa matangazo yanayohusiana na
ulishaji wa watoto wachanga hali inayodhoofisha unyonyeshaji maziwa ya
mama kama njia yenye ufanisi ya kuboresha afya katika siku za kwanza za
maisha ya mtoto. Hapa Tanzania, Kanuni ya Uuzaji wa Chakula (Udhibiti
wa Ubora) cha Mbadala wa maziwa ya Mama na Bidhaa Teule ya mwaka 2013,
inalinda unyonyeshaji. – ufuatiliaji na utekelezaji imara zaidi wa
Kanuni hiyo unahitajika.
Wanawake
wanaofanya kazi wanahitaji kusaidiwa kupitia sheria zinazolinda uzazi
zinazotosheleza. Kwa wanawake waliopo kwenye sekta isiyo rasmi, kuna
haja ya kuboresha mifumo ya misaada ya kifamilia na kijamii, na kuandaa
mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi, ili kuokoa muda na nguvu za
wanawake waweze kufanikisha unyonyeshaji maziwa ya mama.
“Kunyonyesha
maziwa ya mama ni njia ya asili zaidi, yenye ufanisi zaidi wa gharama,
iliyo rafiki zaidi kwa mazingira na rahisi zaidi tunayoijua ya kuwapa
watoto wote, tajiri au maskini, mwanzo mzuri zaidi kiafya wa maisha,”
alimalizia kusema Bibi Zaman. “Kuweka vipaumbele kwenye kuwekeza katika
kukuza unyonyeshaji maziwa ya mama ni pendekezo bora.”
No comments:
Post a Comment