Matukio : Uchaguzi Arusha Mjini kuahirishwa - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Saturday, 10 October 2015

Matukio : Uchaguzi Arusha Mjini kuahirishwa


JIMBO la Arusha Mjini na Chama cha ACT-Wazalendo, wamepata msiba wa aliyekuwa mgombea wa ubunge wa jimbo hilo, Estomih Mallah na kusababisha kuwa jimbo la tatu ambalo kura ya mbunge haitapigwa katika Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa Oktoba 25 mwaka huu.

Majimbo mengine ambayo kura ya kuchagua wabunge haitapigwa ni Lushoto, baada ya kufariki kwa mgombea ubunge wa Chadema, Mohamed Mtoi mwanzoni mwa Septemba mwaka huu.

Lingine ni Ulanga Mashariki, baada ya mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani kufariki dunia mwishoni mwa Septemba mwaka huu.

Taarifa za msiba wa Mallah uliosababishwa na shinikizo la damu, zilianza kusambaa katika mitandao ya simu jana asubuhi na ilipofika mchana, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba, alitoa taarifa ya Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, akitoa pole kwa familia na wanachama kutokana na msiba huo.

“Kiongozi wa chama, Zitto Zuberi Kabwe anatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wanachama kwa ujumla kwa kuondokewa na kiongozi mchapakazi, mwadilifu, mzalendo na aliyekuwa na mapenzi mema na nchi yake,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kuugua, kazi zake

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kabla ya kufikwa na mauti usiku wa kuamkia jana, Mallah alishindwa kupanda jukwaani Jumanne Oktoba 6 mwaka huu, katika mkutano wa kampeni za mgombea urais wa chama hicho, Anna Mghwira, uliofanyika katika eneo la Ngaramtoni baada ya kujihisi kizunguzungu na kichwa kumuuma.

Baada ya hali hiyo, taarifa hiyo ilieleza kuwa Mallah alipelekwa katika Hospitali ya St. Thomas alikopata mapumziko hadi Alhamisi Oktoba 8, alipohamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro, alikofariki dunia saa 7 usiku wa kuamkia jana wakati madaktari na wauguzi wakiendelea kumpatia huduma.

Mbali na kuwa mgombea ubunge wa Arusha Mjini, Mallah alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Raslimali ngazi ya Taifa, Mwenyekiti wa Kwanza wa Ngome ya Wazee Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACTWazalendo.

Kutokana na msiba huo, taarifa hiyo ilieleza kuwa Kamati ya Uongozi Taifa, imeagiza kusimama kwa kampeni za ACT-Wazalendo kwa siku tatu kuanzia jana hadi kesho Jumapili na bendera za chama hicho nchi nzima, zipepee nusu mlingoti kwa siku tano kuanzia jana hadi Jumanne Oktoba 13, mwaka huu.

Zitto aomboleza

Akimuelezea Mallah, Zitto alisema; “nilimtambua Mzee Estomih Mallah kwa misimamo yake ya kupigania usawa na amani tangu akiwa Chadema na hakuogopa kupoteza nafasi ya udiwani aliyokuwa akiishikilia kwa sababu ya kukataa kuyumbishwa.”

Alisema Mallah amefariki akipigania ukombozi wa watu wa Jimbo la Arusha Mjini na ACT-Wazalendo itamuenzi kwa kukemea maovu yote, aliyoanza kukemea na kuendeleza mema yote aliyoacha.

“ACT-Wazalendo itaendelea kumkumbuka daima kwa busara zake na uongozi wake uliotukuka, alijitoa kutumikia Taifa bila ubaguzi wala upendeleo wowote, hivyo chama kitamuenzi kwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali aliyoshiriki kuiasisi wakati wa uhai wake,” alisema Zitto.

NEC yaarifiwa

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Msimamizi wa Jimbo hilo la Uchaguzi, Juma Idd alisema tayari ametoa taarifa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili wapange tarehe mpya ya uchaguzi wa mbunge katika jimbo hilo.

“Kweli mgombea amefariki na nimepata taarifa za kifo hiki leo (jana) saa 12:00 alfajiri, kutoka kwa Katibu wa ACT Wazalendo Jimbo la Arusha, Eliamam Motivo kuwa mgombea ubunge kafariki katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo mkoani Kilimanjaro,” alisema.

Idd alisema kampeni ambazo zitaendelea katika jimbo hilo ni za urais na udiwani tu. Alifafanua kuwa kampeni za ubunge zimesitishwa mpaka Tume itakapopanga upya kwa mujibu wa ratiba zao. Msimamizi huyo wa uchaguzi, alitoa pole kwa wafuasi wa chama hicho kwa kuondokewa na mpendwa wao na kuongeza kuwa wapo pamoja katika kipindi hiki kigumu.
HABARI LEO

No comments:

Post a Comment