Kaimu
Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi
amezungumza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini kuhusu
shughuli za upasuaji wa moyo zinazofanywa na taasisi hiyo. Profesa
Janabi amezungunza na mabalozi hao katika Hoteli ya Serena jijini Dar es
Salaam leo.
Balozi
wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Thami Mseleku (kushoto) na Balozi wa
Rwanda hapa nchini, Eugene Kayihura (kulia) wanamsikiliza Profesa
Mohamed Janabi wakati akieleza mambo ambayo watu wanapaswa kuzingatia
ili kuepuka shinikizo la damu kwenye mkutano uliofanyika Hoteli leo
Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Balozi
wa Zambia nchini Tanzania, Judith Kangoma (kulia) na mwenzake wa
Malawi, Hawa Ndilowe wakimsikiliza Profesa Mohamed Janabi leo.
Picha zote kwa Hisani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
MABALOZI
wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania wameipongeza Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa
kuanzisha huduma ya upasuaji wa moyo.
Mabalozi hao wamefurahishwa na huduma hiyo na kueleza kwamba watawashauri raia wao kwenda kupatiwa matibabu kwenye taasisi hiyo.
Balozi
wa Zimbabwe nchini Tanzania, Balozi Edzai Chimonyo amesema kwamba
wamefurahishwa na juhudi za taasisi hiyo na kwamba wanapenda kujua jinsi
ya kuzuia matatizo ya moyo.
“Napenda kujua ni vipi mtu anaweza kuzuia matatizo ya moyo,” amesema Balozi Chimonyo.
Naye
Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Thami Mseleku amesema kwamba
ataitumia taasisi hiyo kupima afya yake na kwamba endapo atatozwa fedha
kwa ajili kupatiwa matibabu yupo tayari kutoa ili kusaidia wagonjwa wa
kawaida wanaopatiwa matibabu hapo.
Akizungumza
na mabalozi hao, Kaimu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi
amesema ili watu wasipate shinikizo la damu wanapaswa kufanya mazoezi,
kupima afya mara kwa mara na kuchunguza endapo familia ina tatizo la
shinikizo la damu.
Profesa Janabi amesema kwamba endamba mabalozi hao watazingatia hayo wataepuka kupata shinikizo la damu.
Awali
Profesa Janabi amewaeleza mabalozi hao huduma zinazotolewa na taasisi
hiyo ikiwamo kufanya upasuaji kwa watoto 37 hivi karibuni wakimo watoto
wawili kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
Profesa
Janabi amesema upasuaji wa moyo unaofanywa na hospitali hiyo unasaidia
kupunguza gharama za matibabu endapo wangekwenda kutibiwa India.
Amesema
gharama za mgonjwa kufanyiwa upasuaji wa moyo India ni kuanzia Dola
10,000 hadi 12,000 wakiwamo ndugu wanaomsindikiza mgonjwa nchini humo.
No comments:
Post a Comment