Na Mwandishi Wetu
“Suala
la maadili si jipya, Watanzania watakumbuka tangu enzi la Azimio la
Arusha misingi ya maadili imekuwa ikisisitizwa kama kijenzi muhimu cha
ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma,” ni kauli ya Tixon Nzunda,
Naibu Kamishna wa Maadili aliyoitoa siku ya uzinduzi wa Ahadi ya
Uadilifu, Agosti 14, 2015, Ikulu Dar es Salaam.
Kauli
hii inasadifu ninachotaka kukieleza hapa katika makala haya na kwa
hakika kumpa kongole Rais anayemaliza muda wake, Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete kwa kuamua kuhuisha suala la maadili kama kijenzi muhimu cha
ufanisi katika utendaji wa sekta za umma na binafsi.
Itakumbukwa
kuwa Ijumaa iliyopita Reais Kikwete alizindua kile kinachoitwa Ahadi ya
Uadilifu ambapo viongozi kadhaa wa umma na kutoka sekta binafsi walitia
saini hadharani ahadi za kuendesha shughuli zao kimaadili zaidi.
Ahadi
ya Uadilifu kimsingi ni tamko rasmi na bayana la dhamira ya kuwa na
mwenendo wa kimaadili na kuunga mkono Kampeni ya Kitaifa ya Maadili na
Mapambano dhidi ya Rushwa. Kwa kusaini tamko hilo mhusika au taasisi
inakuwa vimejipambanua kwa umma kuwa hawatajiingiza katika masuala
yasiyo ya kimaadili katika utoaji wa huduma na uzalishaji.
Wazo
la kuwa na Ahadi ya Uadilifu ni ubunifu kutoka maabara ya Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN) iliyokuwa ikiangalia mbinu za kuboresha sekta
ya mazingira ya biashara nchini.
Kwa
mujibu wa wataalamu kutoka sekta za umma na binafsi waliokusanyika
katika kufanya uchambuzi huo, ilionekana dhahiri kuwa rushwa bado ni
tatizo katika uendeshaji wa shughuli za umma na binafsi.
Pamoja
na kuwepo sheria, kanuni, miongozo na mikakati ya kukuza maadili na
kupambana na rushwa bado matokeo ya kuridhisha hasa katika kuinua
utendaji na maadili katika uendeshaji wa biashara yavikupatikana.
Wananchi
bado wanalalamika kuwepo kwa urasimu usio wa lazima wenye lengo la
kutengeneza mazingira ya rushwa na huduma zisizoridhisha katika utumishi
wa umma. Wafanyabishara binafsi nao wapo baadhi hawana maadili na hata
kufikia hatua ya kuchochea utoajiwa rushwa au kuzalisha bidhaa zisizo na
viwango.
Vile
vile Sekta Binafsi haijashirikishwa vya kutosha katika Mkakati wa
Kupambana na Rushwa na utamaduni umekuwa ni watu kuamini kuwa Rushwa iko
katika sekta ya umma tu wakati wanaotoa rushwa kubwa wako katika Sekta
Binafsi.
Ni
dhahiri kuwa Sheria, Kanuni, Miongozo na Mikakati iliyopo pekee haiwezi
kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la rushwa na maadili. Hivyo kuhitaji
mkakati wa ziada ambao utajenga mwitikio na dhamira kwa viongozi wa
umma na kuishirikisha Sekta Binafsi katika mapambano dhidi ya rushwa na
utovu wa maadili.
Hivyo
kusainiwa kwa tamko la ahadi ya uaminifu kutasaidia kukuza maadili na
kupambana na vitendo vya rushwa katika sekta ya umma na binafsi; ahadi
au tamko hili linashawishi viongozi, watumishi wa umma na makampuni
binafsi kuwa tayari kufanya kazi kwa kufuata misingi ya maadili na
kupambana na rushwa kwa hiari yao wenyewe.
Katika
tamko hilo kunawekwa kauli thabiti ya kimaadili ambayo inaonesha nia ya
kufanyabiashara au kutekeleza majukumu ya umma kwa uadilifu na
inakumbushwa Makampuni, Viongozi na Watumishi wa Umma juu ya wajibu wao
wa kuzingatia Kanuni za Maadili na Mapambano dhidi ya rushwa.
Misingi
ya tamko hili imebebwa katika kukuza Uwazi, Uadilifu, Uwajibikaji na
Utaalamu katika uendeshaji shughuli za umma; Kukuza mwitikio wa
kupambana na rushwa kwa kuimarisha taratibu za udhibiti wa ndani.
Misingi
mingine ni pamoja na kusimamia masharti ya Sheria ya Maadili ya
Viongozi na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kanuni za Maadili
ya Utendaji katika Utumishi wa Umma, na Kanuni za Maadili ya Kitaaluma;
Pia
ipo hoja ya kuimarisha mahusiano ya viongozi wa umma, watumishi wa umma
au wamiliki na watendaji wa makampuni na wananchi au wateja wengine;
Kudhibiti vitendo vya utovu wa maadili mahali pa kazi na kukuza
uzalendo.
Ili
kufikia malengo ya ahadi hii Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Miradi (PDB)
inayoratibu BRN ndiye mwangalizi mkuu wa kuona suala hili linaleta tija
katika kufikiwa malengo mapana ya BRN.
Hata
hivyo Sekretarieti ya Maadili ndiyo imepewa jukumu la kusimamia
utekelezaji wa kila siku wa ahadi hizi ambapo Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma itakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa Ahadi
ya Uadilifu kwa Watumishi wa Umma kwa kuwashirikisha Watendaji Wakuu wa
Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mashirika ya Umma na
Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ili
kuhakikisha utekelezaji unakuwa wa mafanikio kwa upande wa sekta binafsi
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) itakuwa na jukumu la
kusimamia utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa Makampuni binafsi.
Inategemewa
kuwa utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu utajenga mwitikio na dhamira ya
uadilifu, uwazi, uwajibikaji, ari ya kupambana na rushwa na utoaji wa
huduma bora katika Sekta ya Umma na Binafsi.
Pia,
utahamasisha Viongozi, Watumishi wa Umma na kuzingatia misingi ya
maadili na Mapambano dhidi ya Rushwa. Aidha, kuwashirikisha wananchi
kufuatilia vitendo vya utovu wa maadili miongoni mwa Watumishi wa Umma,
Viongozi wa Umma na Sekta Binafsi na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Kwa
namna hii hususani katika eneo la utoaji wa huduma na uzalishaji wa
bidhaa watanzania watarajie kuimarika sana kwa uadilifu katika utendaji
wa wahusika na kusaidia kufikia malengo ya BRN.
No comments:
Post a Comment