THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Mheshimiwa Said Meck Sadik kufuatia vifo vya watu tisa wa familia moja
ya Bwana Masoud Matal vilivyotokea alfajiri ya tarehe 27 Agosti, 2015
kwa ajali ya moto.
Wanafamilia
hao wakiwemo watoto watano walipoteza maisha baada ya nyumba yao
iliyoko katika Mtaa wa Gulam, eneo la Buguruni Malapa katika Wilaya ya
Ilala Jijini Dar es Salaam kuungua na kuteketea kabisa kwa moto. Baba
wa familia, Bwana Masoud Matal alisalimika kwa vile hakuwamo katika
nyumba hiyo wakati ikiungua.
“Nimepokea
kwa mshtuko mkubwa na nimesikitishwa mno kutokana na taarifa za
kupoteza maisha kwa watu tisa wa familia moja ya Bwana Masoud Matal
baada ya nyumba yao kuunguzwa na kuteketezwa kabisa na moto alfajiri ya
tarehe 27 Agosti, 2015”, amesema kwa huzuni Rais Kikwete akiomboleza
vifo vya wanafamilia hao.
“Kwa
hakika hili ni pigo kubwa kwa Bwana Masoud Matal, lakini namuomba awe
mvumilivu kwa machungu yote ya kupotelewa ghafla na familia nzima,
lakini yote amwachie Mwenyezi Mungu muweza wa yote”, ameongeza kusema
Rais Kikwete.
Katika
salamu zake hizo, Rais Kikwete amemwomba Mheshimiwa Sadik kumfikishia
Salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa Bwana Masoud Matal kutokana
na msiba huo mkubwa uliompata, na amesema anamuomba Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za
Marehemu wote, Amina.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
28 Agosti,2015
No comments:
Post a Comment