Mkurugenzi
Msaidizi wa Upimaji na Ramani vijijini wa Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Bw. Huruma Lugalla (kushoto) akitoa maelekezo kwa
wataalam wa Upimaji na Ramani wa wizara hiyo wakati wa uhakiki wa moja
ya ramani ya eneo linalopaswa kuwa la makazi ya watu na taasisi nje
kidogo ya mji wa Chalinze, Bagamoyo mkoani Pwani iliyopimwa na Kampuni
ya Intergrated Property Consultancy and Services (IPCS) ya Morogoro na
kubainika kuwa chini ya kiwango.
Wataalam
wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
wakifanya uhakiki wa moja ya ramani ya eneo linalopaswa kuwa la makazi
ya watu na taasisi nje kidogo ya mji wa Chalinze, Bagamoyo mkoani Pwani
lililopimwa chini ya kiwango. Katikati (aliyesimama) ni Bw. Bernard
Malugu, Mkurugenzi wa Kampuni ya Intergrated Property Consultancy and
Services (IPCS) ya Morogoro iliyoifanya kazi hiyo chini ya kiwango.
Mkurugenzi
Msaidizi wa Upimaji na Ramani vijijini wa Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Bw. Huruma Lugalla (kushoto) akifuatilia moja ya
eneo ambalo lilitakiwa kuwa na alama ya mpaka ambalo halikuwa na alama
yoyote wakati wa uhakiki wa moja ya ramani ya eneo linalopaswa kuwa la
makazi ya watu na taasisi nje kidogo ya mji wa Chalinze, Bagamoyo mkoani
Pwani iliyopimwa na Kampuni ya Intergrated Property Consultancy and
Services (IPCS) ya Morogoro ambayo ilibainika kuwa chini ya kiwango.
Kulia ni Bw.Allex Kachoka Mpima Ardhi wa wizara hiyo.
Moja
ya alama ya mpaka ya ambayo iligundulika kujengwa chini ya kiwango
wakati wa uhakiki uliofanywa na wataalam wa Wizara ya Ardhi kwenye moja
ya ramani ya eneo linalopaswa kuwa la makazi ya watu na taasisi nje
kidogo ya mji wa Chalinze, Bagamoyo mkoani Pwani.Kampuni ya Intergrated
Property Consultancy and Services (IPCS) ya Morogoro ambayo ilipewa
kazi ya Upimaji wa eneo hilo imeifanya kazi hiyo chini ya kiwango.
Wapima
Ardhi na Mipaka wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
wakiendelea na zoezi la uhakiki wa alama za mipaka kwa kutumia kifaa
kiitwacho Hand Heled GPS kwenye moja ya ramani ya eneo linalopaswa kuwa
la makazi ya watu na taasisi nje kidogo ya mji wa Chalinze,Bagamoyo
Pwani.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeto tahadhari kwa Taasisi na
wananchi wanaotaka kupimiwa maeneo yao ya ardhi kuhakikisha kuwa
wanafuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia masuala ya upimaji wa
ardhi ili kuepuka kupata hasara na kuingia kwenye migogoro ya ardhi
isiyo ya lazima kutokana na kutumia watu au makampuni yasiyosajiliwa
kishera.
Hatua
hiyo imekuja kufuatia baadhi ya makampuni yanayojishughulisha na upimaji
wa Ardhi na ramani kugundulika kufanya kazi za wateja wao chini ya
viwango kufuatia ramani zilizowasilishwa na makampuni hayo wizarani
hapo kwa ajili ya kuidhinishwa kukosa sifa pindi zinapofanyiwa uhakiki
na wataalam wa wizara hiyo.
Mkurugenzi
Msaidizi wa Upimaji na Ramani vijijini wa wizara hiyo Bw. Huruma
Lugalla akizungumza mara baada ya timu ya wataalam wa wizara hiyo
kufanya uhakiki wa moja ya ramani ya eneo linalopaswa kuwa la makazi ya
watu na taasisi nje kidogo ya mji wa Chalinze, Bagamoyo mkoani Pwani
ambalo upimaji wake umekiuka kanuni na taratibu amesema Serikali
haitayafumbia macho makampuni yote yanayochukua fedha za wananchi na
Taasisi na kisha kufanya upimaji usiokidhi viwango vilivyowekwa na
wizara hiyo kwa mujibu wa Sheria.
Amesema
wizara hiyo itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuyafungia
makampuni yote yanayobainika kufanya kazi chini ya kiwango, kukiuka kwa
makusudi taratibu za upimaji wa ardhi na kufanya uzembe wa kushindwa
kuweka mipaka na alama sahihi za maeneo wanayoyapima jambo linalochangia
mivutano na migogoro pindi maeneo husika yanapogawiwa kwa wananchi.
“Nawaomba
wananchi na Taasisi mbalimbali zinazotaka kupimiwa maeneo yao kwa
kutumia makampuni kuwa makini na kuchukua tahadhari ili kuepuka hasara
ya kulipa gharama za upimaji mara mbili, msichukue watu wa kati au
kampuni zisizosajiliwa kisheria ambazo haziko kwenye orodha ya Katibu
wa Baraza la Taifa la Wapima Ardhi” Amesisitiza.
Bw.
Lugalla ameeleza kuwa Kampuni ya Intergrated Property Consultancy and
Services (IPCS) kutoka Morogoro iliyohusika na zoezi la upimaji na
ramani katika eneo hilo haikufuata sheria, kanuni na taratibu
zilizowekwa kwa mujibu wa sheria kufuatia ramani iliyowasilishwa na
Mkurugenzi wake Bw. Bernard Malugu wizarani hapo kushindwa kukidhi
vigezo vya ubora unaotakiwa mara baada ya kuhakikiwa na wataalam wa
Upimaji na ramani wa Wizara.
Amesema
wataalam wa upimaji na ramani wa Wizara hiyo mara baada ya kufanya
uhakiki wa eneo hilo wamebaini ukosefu wa alama (bikoni) za baadhi
viwanja, kukosekana kwa pini za kugawa viwanja na tofauti umbali wa eneo
la kiwanja kimoja hadi kingine iliyokuwepo kwenye ramani ambayo
haikuendana na uhalisia wa eneo husika wakati wa zoezi la uhakiki.
Aidha,
amebainisha kuwa ramani ya eneo hilo ilisainiwa kimakosa na Mkurugenzi
wa Kampuni hiyo kufuatia kampuni yake ambayo imesajiliwa kisheria
dhamana kuamua kumtafuta mtu wa kati wa kuifanya kazi hiyo badala yake
na kisha Mkurugenzi wake Bw. Bernard Malugu kuidhinisha ramani hiyo kwa
kuisaini huku ili ipelekwe wizarani kupatiwa kibali huku akijua wazi
kanuni na taratibu zinazosimamia sekta hiyo hazimruhusu kutoa kazi kwa
mtu au kampuni nyingine.
“Ili
kuepusha migogoro ya ardhi inayoweza kutokea katika eneo lile taratibu
zitafuatwa ili kampuni hiyo iifanye kazi ile upya kwa gharama zake na
kisha kuwaita wataalam wa wizara kufanya uhakiki upya ili kujiridhisha
kabla ya kutoa kibali cha viwanja hivi, Sisi kama wizara hatutakubali
kuendelea kulaumiwa na wananchi kwa uzembe unaofanywa na makampuni haya”
Amesisitiza.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya IPCS iliyopewa kazi ya kupima eneo
hilo akitoa utetezi kwa kampuni yake mara baada ya kufanyika kwa uhakiki
huo alikiri kuwa kampuni yake imefanya makosa na kukiuka sheria, miiko
na maadili yanayosimamia shughuli za upimaji na ramani nchini.
Amesema
yeye kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo alisaini ramani ya eneo hilo
Machi 19, 2015 kimakosa hivyo kampuni yake imeonyesha uzembe na udhaifu
wa usimamizi ikiwemo yeye mwenyewe kutomfahamu mtu wa kati aliyeifanya
kazi hiyo.
Aidha,
amesema kampuni yake iko tayari kuyabeba mapungufu yote yaliyojitokeza
na kukubali kurudia kazi ya kupima na kuweka mipaka iliyokosekana endapo
itaruhusiwa na wizara hiyo kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment