Matukio :Watanzania 18 warejeshwa nchini kutokea Yemen - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Wednesday, 22 April 2015

Matukio :Watanzania 18 warejeshwa nchini kutokea Yemen


Kiongozi wa Msafara wa Watanzania waliorejeshwa nchini kutokea Yemen Bw. Abdul Twahid Said akizungumza na Waandishi wa Habari  kwa niaba ya wenzake mara baada ya kuwasili leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere  jijini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Emirates. Bw. Said alitoa shukrani kwa jitihada za Serikali za kuwarejesha nchini Watanzania wote kufuatia machafuko yanayoendelea nchini Yemen.
 Bw. Sabri Hery Omari ambaye ni miongoni mwa Watanzania waliorejea nae  akizungumza na Waandishi wa Habari huku sehemu nyingine ya Watanzania hao wakionekana kwa nyuma.
Watanzania waliurudishwa Nchini wakitokea nchini Yemeni kutokana na machafuko yanayoendelea huko wakifurahi kuwa nyumbani salama
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi. Mindi Kasiga akizungumza mara baada ya Watanzania hao kuwasili nchini. Anayeonekana pembeni mwenye miwani ni Bw. Elibariki Maleko, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye alikuwepo wakati wa mapokezi hayo Picha na Reginald Philip
============================================
Na. Reuben Mchome
Watanzania kumi na nane warejea kutoka Yemen.
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuwarejesha nyumbani jumla ya Watanzania kumi na nane kutoka nchini Yemen kufuatia mapigano yanayoendelea nchini humo ya wenyewe kwa wenyewe.
Watanzania hao ambao wamewasili nchini leo kwa ndege ya shirika la emirates namba EK 725 wameishukuru serikali kutokana na jitihada za haraka zilizofanywa kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Oman na kufanikiwa kuwarejesha salama pasipo gharama zozote .
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Watanzania hao Bw. Sabri Abeid Almaghi ambaye alikua anafanya biashara nchini Yemen amesema kuwa anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa namna ya pekee kwa kuwajali wananchi wake bila kujali wapo nchini au nje ya nchi na kutoa msaada  kwa wakati.
“Tunaishukuru sana serikali yetu ya Tanzania kwa jinsi ambavyo wanajali wananchi wake bila kujali wapo ndani au nje ya nchi,  kweli kama sio jitihada za ubalozi wetu pale mjini Muscat, sijui leo tungekua katika hali gani, tunaomba shukrani zetu mzifikishe kwa Rais Kikwete, Waziri Membe na wahusika wengine wote waliofanikisha kuturejesha nyumbani” alisema Mzee Saleh Mbaraka Jabri mmoja wa watanzania hao waliorejea kutoka Yemen.
Aidha, akizungumzia hali ya usalama ilivyo nchini Yemen, Bw. Almaghi amesema kuwa hali ni mbaya sana kufuatia mapigano ya anga yanayoendelea hivi sasa na muda wowote yataanza mapigano ya ardhini. Aidha amesema kuwa kufuatia hali hiyo huduma zote za kijamii pamoja na biashara zimesimama.
Akizungumza mara baada ya kuwapokea watanzania hao Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini Bi. Mindi Kasiga amesema mpaka hivi sasa watanzania ambao wamesharejeshwa nchini kutoka Yemen ni 23, kati ya   Watanzania 69 ambao wamejiandikisha  na jitihada  zinaendelea.
“Awamu ya kwanza ya Watanzania waliorejeshwa na serikali kutoka nchini Yemen ni familia moja ya watu watano ambao walirudi wiki chache zilizopita” alimalizia Bi. Mindi Kasiga.
Hivi karibuni Serikali kupitia Waziri wa Mambo  na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe ilitangaza kuwarejesha nchini Watanzania waliopo Yemen kufuatia machafuko yanayoendelea nchini humo.

No comments:

Post a Comment