Veronica Mheta, Arusha
WAKANDARASI wameaswa kuacha tabia ya kujenga majengo ya serikali
pamoja na wananchi chini ya viwango kwalengo la kupata faida kubwa na
kuleta hasara kubwa katika nchi.
Aidha serikali inafanya kila linalowezekana ili kulipa madeni ya
wakandarasi wazalendo ikiwemo kupata mikopo ya riba nafuu kwaajili ya
kuwezesha wakandarasi kupata zabuni za ujenzi wa majengo makubwa zaidi
yanayojengwa na wageni kutoka nchi za nje.
Kauli hiyo ilitolewa jana Jijini hapa na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi, Mhandisi Mussa Iyombe wakati alipokuwa akifungua mkutano mkuu
wa nne wa mwaka wa Chama cha Makandarasi Wazalendo Tanzania (ACCT)
unaofanyika kwa siku mbili .
Alisema si vyema wakandarasi kufanya kazi kwa kutaka faida kubwa na
kupelekea hasara kwa wananchi pamoja na serikali kwani ufanyaji kazi
kwa kulipua unashusha heshima katika fani hiyo sambamba na kuleta
hasara kwa serikali kwani baadhi ya majengo yanajengwa chini ya
viwango.
Pia alisema hivi sasa serikali imefanya mazungumzo na Gavana wa Benki
Kuu (BoT) kwaajili ya kuwasaidia wakandarasi waweze kupata mikopo
yenye riba nafuu kutoka serikalini itakayowasaidia kupata fedha na
kujenga majengo makubwa zaidi badala ya wageni kutoka nje ya nchi
kupata zabuni za kujenga majengo hayo huku wakandarasi wazalengo
wakiambulia asilimia 40 tu ya ujenzi.
“Naomba msibabaike na faida kubwa na kuleta hasara kwa Taifa angalieni
uzalendo lakini najua mnaidai serikali fedha nyingi ila tuko mbioni
kuwalipa madeni yenu na pia hivi sasa serikali itatoa mikopo yenye
unafuu ili muweze kujenga majengo makubwa ya kisasa badala ya wageni
kujenga maana wakipata faida wanarudisha kwao huku wakandarasi
wazalendo wakiambulia kazi za matengenezo madogo madogo”.
Naye Mwenyekiti wa ACCT, Mhandisi Milton Nyerere alisema kuwa chama
hicho kipo katika hatua ya kuanzisha chuo cha ufundi kwaajili ya
kukuza uwezo kwa kuendesha mafunzo ya fani mbalimbali za kikandarasi
kwa mafundi wa makampuni ya makandarasi ili kupunguza changamoto ya
wataalam wanayokumbana nayo kwenye utekelezaji wa miradi.
No comments:
Post a Comment