Waziri
wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu
akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati
ya Mpango ya Bunge Zima kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa
Mwalimu Nyerere.
Sehemu
ya Wabunge waliohudhuria uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima wakimsikiliza
Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu
kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
Baadhi
ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakifuatilia kwa
makini uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16.
viongozi
waandamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakifuatilia uwasilishaji
wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 uliokuwa ukifanywa na
Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu
katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima. Picha na Saidi Mkabakuli.
Naibu
Katibu Mtendaji (Sekta za Uzalishaji) kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bw. Maduka Kessy (Kulia) akimpongeza Waziri wa nchi (Ofisi ya
Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Kushoto) mara baada ya
kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati
ya Mpango ya Bunge Zima.
Na Saidi Mkabakuli
Serikali
imesema kuwa ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha miradi ya
kitaifa ya kimkakati iliyoibuliwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo
unaofikia kikomo mwaka ujao wa fedha wa serikali.
Hayo
yalisemwa na Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe.
Dkt. Mary Nagu wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka
2015/16 katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima kwenye Ukumbi wa Mikutano
wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Dkt.
Nagu alisema kuwa mpaka kufikia mwezi machi mwaka huu, serikali
imefanikiwa kutandika reli za uzito wa ratili 56.12 kwa yadi kwa umbali
wa km 9 kati ya stesheni za Lumbe, Mto Ugalla na Katumba; kukamilisha
malipo ya ununuzi wa mabehewa 274 ya mizigo ambapo mabehewa yameshaanza
kupokelewa Novemba 2014; kukamilika kwa matengenezo ya njia ya reli
iliyoharibiwa na mafuriko katika maeneo ya Ruvu – njia panda ya Mruazi.
Waziri
Nagu aliongeza kuwa kwa upande wa Barabara hatua iliyofikiwa ni pamoja
na kukamilika kwa ujenzi wa kilometa 502.6 za barabara kuu kwa kiwango
cha lami dhidi ya lengo la kilomita 560, na ukarabati wa kilomita 78.8
za barabara kuu kwa kiwango cha lami dhidi ya lengo la kukarabati
kilomita 131.5. Kwa upande wa madaraja hatua iliyofikiwa ni: kuendelea
na ujenzi wa madaraja ambapo daraja la Kigamboni limefikia asilimia 75,
Sibiti asilimia 22, Kilombero asilimia 26, Mbutu asilimia 99, Lukuledi
II asilimia 25 na Kavuu asilimia 36.
Katika
sekta ya Uchukuzi, Dkt. Nagu aliyataja mafanikio yaliyopatikana ni
pamoja na kuongezeka kwa shehena iliyohudumiwa katika bandari ya Dar es
Salaam kufikia tani milioni 14.3 Machi 2015 dhidi ya lengo la tani
milioni 13.0 kwa mwaka 2014/15; kuongezeka kwa ufanisi wa bandari katika
kupakua magari kwa kila shifti moja ya saa 8 kufikia magari 886 kwa
shifti kufikia Machi 2015 ikilinganishwa na lengo la magari 600 kwa
shifti katika mwaka 2014/15; kupungua kwa muda wa meli kupakia na
kupakua mizigo bandarini kutoka lengo la wastani wa siku 5 mwaka 2013/14
hadi wastani wa siku 3.7 kufikia Machi 2015; kuanza kwa utekelezaji wa
mradi wa malipo kwa njia ya mtandao mwezi Julai, 2014; na kuanza kutoa
huduma katika bandari ya Dar es Salaam kwa masaa 24 kwa siku zote za
juma. Aidha, kwa upande wa bandari ya Bagamoyo, hatua iliyofikiwa ni
kusainiwa kwa makubaliano ya ujenzi wa bandari; na kutangazwa kwa zabuni
kwa ajili ya kupata wawekezaji katika bandari za Mtwara na Mwambani
-Tanga.
“Katika
sekta ya nishati, hatua iliyofikiwa ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi
wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam (km 542) Machi 2015,
na ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi Madimba (Mtwara) na Songosongo
(Lindi) umefikia asilimia 86.9 ambapo unatarajiwa kukamilika Juni 2015.
Kwa upande wa usambazaji wa umeme vijijini, wateja wapya 2,602
wameunganishiwa umeme katika mikoa ya Simiyu, Singida, Kagera, Tanga,
Ruvuma, na Iringa,” alisema Dkt. Nagu.
Kwa
mujibu wa Waziri Nagu, shughuli nyingine zilizotekelezwa nia katika
sekta ya nishati, ni pamoja na kukamilika kwa usimikaji wa mitambo 4 ya
kufua umeme yenye uwezo wa jumla ya MW 150, kuendelea na ujenzi wa
vituo vya kupoza na njia za kusafirisha umeme, na kuendelea na ujenzi wa
karakana, majengo ya utawala, na barabara za ndani katika mradi wa
Kinyerezi I; kukamilisha ulipaji fidia kwa eneo la Makambako katika
mradi wa usafirishaji umeme wa Makambako - Songea; na kuanza ujenzi wa
nguzo za njia ya umeme katika mradi wa msongo wa kV 400 wa Iringa –
Shinyanga.
Akiwasilisha
kazi zilizotekelezwa katika sekta ya Maji, Dkt. Nagu alisema kuwa
ulazaji wa mabomba katika mradi wa maji Ruvu Chini kutoka Bagamoyo hadi
Dar es Salaam kazi ambayo imekamilika kwa kilomita 52.43 kati ya
kilomita 55.93 za mradi sawa na asilimia 93.8; kwa upande wa mradi wa
maji Ruvu Juu: mkandarasi amekamilisha utafiti wa udongo na uchunguzi wa
awali wa mahali yatakapojengwa matanki Kibamba na Kimara; na kwa upande
wa mradi wa Bwawa la Kidunda, wananchi wamelipwa fidia ya shilingi
bilioni 7 kupisha ujenzi wa barabara na eneo litakapojengwa bwawa.
“Kwa
upande wa miradi ya maji vijijini, jumla ya miradi 123 ya maji ilijengwa
na kukamilika. Idadi hii imenufaisha wananchi wapatao 463,750 na
kuongezeka kwa ufanisi katika masuala ya ununuzi wa huduma katika
mikataba kutoka siku 265 hadi siku 90. Aidha, Serikali imeendelea na
ujenzi wa mabwawa ambapo bwawa la Iguluba (Iringa) na Wegero (Mara)
yamekamilika. Vile vile, ujenzi wa bwawa la Kawa (Rukwa) umefikia
asilimia 95, bwawa la Sasajila (Dodoma) asilimia 66.09 na Mwanjoro
(Shinyanga) asilimia 45.4,” aliongeza Waziri Nagu.
Katika
sekta ya kilimo, Dkt. Nagu aliyataja mafanikio yaliyopatikana ni pamoja
na: kupatikana kwa hati za mashamba mawili ya Bagamoyo na Mkulazi;
maghala 30 yamekarabatiwa na kupatiwa watoa huduma binafsi katika Wilaya
za Mbozi na Momba. Vile vile, skimu 30 za umwagiliaji zimepatiwa watoa
huduma binafsi katika Wilaya za Mbarali, Kyela na Iringa; na mafunzo
juu ya kubaini na kudhibiti visumbufu, matumizi bora ya maji, utunzaji
na matengenezo ya miundombinu ya umwagiliaji na kutumia mwongozo wa
uendeshaji skimu za umwagiliaji yametolewa. Aidha, ujenzi wa maghala 2
katika Wilaya ya Mlele umekamilika.
Vile
vile katika sekta ya viwanda, Waziri Nagu alizitaja kazi zilizotekelezwa
ni pamoja na kukamilika kwa ukarabati wa barabara ya Itoni - Mkiu -
Liganga na Mchuchuma kwa kiwango cha changarawe ili kuwezesha mitambo
kufika maeneo ya Mchuchuma na Liganga; na kuanza uthamini wa mali za
wananchi watakaohama eneo la Mchuchuma. Vile vile, fidia shilingi
bilioni 53 imelipwa katika eneo la kujenga kituo cha Biashara na Huduma
Kurasini; na fidia ya shilingi bilioni 7 imelipwa katika eneo la
uwekezaji Bagamoyo na Serikali imesaini mkataba na kampuni ya China
Mechants Holding International kwa ajili ya kujenga bandari na eneo la
viwanda. Aidha, katika kiwanda cha kuzalisha dawa ya kuua viluwiluwi wa
mbu, Kibaha, kazi ya ufungaji wa mitambo na ujenzi wa miundombinu
inaendelea na inatarajiwa kukamilika kabla ya Julai, 2015.
Akizungumzia
upande wa maendeleo ya rasilimali watu, Dkt. Nagu alisema kuwa kazi
zilizofanyika ni pamoja na kuendelea kugharamia wanafunzi 159
wanaoendelea na mafunzo katika fani za mafuta na gesi kwa ngazi
mbalimbali za mafunzo ndani na nje ya nchi ambapo wanafunzi 124
wanagharamiwa na Serikali na wanafunzi 35 wanagharamiwa na nchi
wahisani; na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo
vikuu na vyuo vya ualimu, ufundi na ustawi wa jamii.
Kwa
upande wa utafutaji wa rasilimali fedha, Waziri Nagu alisema kuwa
Mamlaka ya Mapato Tanzania inatumia kanzidata bora inayohifadhi taarifa
inayoweza kuthaminisha bidhaa na hivyo kutoa makadirio bora zaidi ya
viwango vya kodi. Vilevile, alisema kuwa tozo kwa ajili ya uwekezaji
katika elimu umeanza Julai 2013 ikiwa asilimia 2.5 ya mapato ghafi ya
kampuni za simu.
“Katika
sekta ya fedha, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuongezea Benki ya
Maendeleo ya Kilimo mtaji wa shilingi bilioni 60; kuendelea kuongeza
mtaji wa Benki ya Rasilimali kufikia shilingi bilioni 212 ambapo mtaji
kutoka Serikalini ni shilingi bilioni 152.2 na shilingi bilioni 59.8
zimetokana na malimbikizo ya faida; na mali za Benki ya Maendeleo ya
Wanawake Tanzania ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 26.5 mwaka 2013
hadi shilingi bilioni 34.8 mwaka 2014,” alisema Dk. Nagu.
Kuhusu
eneo la huduma za utalii, Dkt. Nagu aliongeza kuwa kazi zilizofanyika
ni pamoja na usanifu wa ujenzi wa Utalii House awamu ya pili na
kuboreshwa kwa mfumo wa ukusanyaji mapato (utalii, uwindaji na upigaji
picha). Aidha, idadi ya watalii kutoka nje iliongezeka kutoka watalii
1,090,905 mwaka 2013 hadi watalii 1,102,026 mwaka 2014. Vile vile mapato
yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.81
mwaka 2013 hadi dola za Marekani bilioni 1.98 mwaka 2014.
“Kwa
upande wa Biashara, hatua iliyofikiwa ni kurekebisha sheria ya mfumo wa
stakabadhi ghalani na kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu mfumo
huo; kuanzishwa kwa kampuni ijulikanayo kama Tanzania Mechantile
Exchange plc kusimamia na kuendesha soko la mazao ya bidhaa na
kuhamasisha matumizi ya fursa za masoko ya mipakani, Kikanda na
Kimataifa,” aliongeza.
Kwa
mujibu wa Dkt. Nagu maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka
2015/16 yamezingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika malengo
ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2011/12 – 2015/16). Aidha, Mpango huu umezingatia Mkakati wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini – MKUKUTA II (2010/11 – 2014/15),
Malengo ya Milenia, Mwongozo wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2014/15;
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2014/15 yaliyojadiliwa na
Bunge Novemba, 2014; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2010 –
2015); na sera na mikakati ya kisekta.
No comments:
Post a Comment