Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.
Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
amevitaka vyama kurekebisha katiba zao kwenye kipengele kinachoruhusu
kuanzishwa kwa vikosi vya ulinzi na usalama.
Vyama vyenye vikosi cha ulinzi na usalama ni Chadema chenye Red Brigade,
CCM (Green Guard), CUF (Blue Guard) na sasa ACT-Wazalendo (ACT Amani).
Mutungi alisema uanzishwaji wa vikundi hivyo unakwenda kinyume na Katiba
ya nchi inayolipa jeshi la polisi mamlaka ya kulinda usalama wa raia na
mali zao.
Akizungumza baada ya mkutano wake na vyama hivyo jana, Jaji Mutungi
alisema katiba za vyama vingi vilivyosajiliwa kabla hajaingia ofisini
vilikuwa na kifungu kinachoruhusu kuanzishwa kwa vikosi vya ulinzi na
usalama wa mali za chama au viongozi wao wawapo katika mikutano.
“Haturuhusu kifungu hicho kuwapo kwenye katiba za vyama vinavyosajiliwa
sasa (hakugusia ACT - Wazalendo). Hatuvifundishi vyama vya siasa namna
ya kuandaa katiba zao lakini tunasimamia kifungu hiki kwa vile
kinapingana na sheria.”
Jaji Mutungi alisisitiza kuwa vyama vya siasa nchini havina uelewa wa
sheria ya vyama vya siasa ambayo ndiyo inayovisimamia, ndiyo maana
vinashindwa kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria hiyo.
Kauli ya polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Ernest Mangu alisema watapambana
na vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vya siasa wakati wa
Uchaguzi Mkuu endapo vitaingilia majukumu ya jeshi la polisi.
Alisema uanzishwaji wa vikundi hivyo ni kinyume cha sheria inayolipa
Jeshi la Polisi dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
Alisema vikundi hivi vilianzishwa kama chipukizi au halaiki lakini
baadaye vilikuwa na kubadili malengo na kuanza kuingilia majukumu ya
polisi na kuhatarisha amani.
Maoni ya wadau
Hata hivyo, kauli za Msajili na Mangu zilipokewa kwa hisia tofauti na
viongozi wa vyama hivyo na baadhi vikiweka wazi kuwa havipo tayari
kuachana na vikundi hivyo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema vijana wa
Green Guard hawaandaliwi kijeshi na kuwa tishio kama vyama vingine, bali
kuwafanya wawe vijana bora, wakakamavu na kuwajengea uzalendo ndani ya
nchi yao.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema chama chake hakipo tayari
kuivunja Red Brigade huku akiilaumu CCM kuwa kikundi chake cha Green
Guard kimepata mafunzo ya kijeshi kikifundishwa na askari tofauti na wao
ambao wanafundishwa na raia.
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Nzega jana, Mbowe alisema suluhisho
la tatizo hilo haliwezi kuwa sheria bali kuhakikisha haki inatendeka na
inaonekana kutendeka kwa kila chama, akitolea mfano jinsi viongozi wa
chama hicho walivyopigwa na Green guard bila polisi kuchukua hatua.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment