Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akisalimiana na kumkaribisha Ofisini kwake Waziri wa Nchi
Maendeleo na Francophonie wa Ufaransa Mhe. Annick Girardin, wakati
alipofika Ofisini kwake Ikulu Dar es salaam April 09, 2015.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akizungumza na Waziri wa Nchi Maendeleo na Francophonie wa
Ufaransa Mhe. Annick Girardin aliyeongoza ujumbe wa watu tisa, wakati
alipofika Ofisini kwake Ikulu Dar es salaam April 09, 2015.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib
Bilal katikati, Waziri wa Nchi Maendeleo na Francophonie wa Ufaransa
Mhe. Annick Girardin kushoto na Balozi wa Ufaranza Nchini Tanzania Mhe.
Malika Barak, wakiwa kwenye picha ya pamoja nje wa Ofisi ya Makamu wa
Rais Ikulu Dar es salaam April 09, 2015.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akiagana na Waziri wa Nchi Maendeleo na Francophonie wa Ufaransa
Mhe. Annick Girardin, baada ya kumaliza Mazungumzo yao Ofisini kwake
Ikulu Dar es salaam April 09, 2015. (Picha na OMR)
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
amekutana na ujumbe kutoka serikali ya Ufaransa ambapo wamezungumzia
mchango wa Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kuhimili mabadiliko ya
tabianchi na kupunguza gesi joto.
Ujumbe
huo wa watu tisa ambao unaongozwa na Waziri wa Nchi wa Maendeleo ya
Francophonie anayeshughulika na masuala ya mazingira wa Ufaransa
Mheshimiwa Annick Girardin ulikutana na Dkt. Bilal leo ofisini kwake
Ikulu.
Waziri
Annick alimweleza Dkt. BiLal kuwa lengo la ziara yake katika nchi za
Ethiopia, Tanzania na Kenya ni kuhimiza baadhi ya nchi za Afrika ambazo
zinaweza kutoa mchango mkubwa katika kufikia makubaliano ya Mkataba Mpya
wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kupitishwa mjini Paris,
Ufaransa.
Alisema
mwaka huu Ufaransa inaandaa mkutano wa 21 wa Mkataba wa Mabadiliko ya
Tabianchi na kuiomba Tanzania iendelee kushiriki kikamilifu kwa kutoa
mchango wake katika maandalizi ya Mkataba Mpya katika mkutano huo.
Makamu
wa Rais aliuambia ujumbe huo kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na
nchi nyingine za Afrika katika kuhakikisha mkutano huo unakuwa wa
mafanikio hasa kwa sababu ya kazi kubwa Tanzania iliyofanya kama
Mwenyekiti wa Kamati ya Marais wa Afrika ya Mabadiliko ya Tabianchi
(CAHOSCC) na kusimamia kamati mbalimbali za Mkataba Mpya.
Alisema
katika maandalizi ya mkutano huo Tanzania imeanza mchakato katika
kuainisha maeneo muhimu ya mchango wake kwa juhudi za dunia za
kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (INDC) yakiwamo ya sekta za
kilimo, mifugo, maji, misitu na ardhi.
Aidha
alisema sekta za nishati, usafirishaji, udhibiti wa taka zimeainishwa
pia kama maeneo yanayoweza kuchangia kupunguza gesi joto..
Hata
hivyo, Dkt. Bilal aliiomba Ufaransa kuisaidia Tanzania kwa utaalam na
teknolojia ili nchi iweze kufanikisha azma yake ya kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi na kutoa mchango wake wa kupunguza gesi joto
bila kuathiri maendeleo jambo ambalo Waziri Annick alilikubali.
Akizungumzia
kwa upande wa Afrika kwa ujumla Makamu wa Rais alisema karibu nchi
nyingi za Afrika zimeathirika kutokana na mafuriko ya mara kwa mara na
ongezeko la kina cha bahari kiasi cha kusababisha baadhi ya visiwa
vidogo kuzama. Alisema ukame na mmomonyoko wa udongo ni tatizo kubwa
kwa nchi za Afrika.
Dkt.
Bilal alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Ufaransa kwa misaada
yake katika sekta za elimu, nishati, mabadiliko ya tabianchi na maji na
kutoa mfano wa mradi wa maji wa Musoma ambao utanufaisha wananchi wa mji
huo baada ya kukosa maji safi na salama kwa muda mrefu.
Waziri Annick na ujumbe wake wanatarajia kwenda Kenya ambapo kesho pamoja na mambo ya mengine atagusia masuala ya ugaidi.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
9/4/2015
No comments:
Post a Comment