Matukio : Skimu ya Mpunga Kiroka Yapata Ugeni Mkubwa - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Friday, 13 March 2015

Matukio : Skimu ya Mpunga Kiroka Yapata Ugeni Mkubwa


Msimamizi wa mradi wa FAO kijiji cha Kiroka mkoani Morogoro, Ajuaye Sigalla, akitoa muhtasari wa maendeleo ya mradi FAO unaotekelezwa na wanakikundi wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI) mbele ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto) na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi walipofanya ziara ya kugagua miradi yao ya maendeleo mkoani Morogoro.(Picha na Zainul Mzige wa modewjiblog)

Na Mwandishi wetu, Morogoro

BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Filiberto Sebregondi  ametembelea skimu ya umwagiliaji ya Kiroka na kusema kwamba atahakikisha kwamba kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo serikali wataendelea kusaidia wananchi kujiinua kiuchumi.

Akiwa katika skimu hiyo inayosaidiwa na Shirika la Chakula duniani (FAO) ametaka miradi ya maendeleo nchini kutowaacha nyuma wanawake na watoto kwani wao ndio msingi wa maendeleo ya kijamii kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.

Balozi huyo ambaye anatarajiwa kurejea Ulaya mwaka huu baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini amesema kwamba kuwapo kwa asilimia 60 ya wafaidika na mradi huo wa Mpunga kuwa wanawake kumesaidia sana kuamsha maendeleo ambayo yanatakiwa kuendelea kusimamiwa.

"Wanawake  wamefanikiwa kupeleka watoto wao shuleni. kuwapatia chakula kinachostahiki na kupata kipato na katika hili ni vyema wasiachwe nyuma kimaendeleo" alisema balozi huyo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi akizungumza na wanakikundi wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI) wanaofadhiliwa na FAO wakati wa ziara ya kutembelea miradi  inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo ambapo mradi wa Kiroka unafadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la FAO huku mradi wa makazi mapya kwa waathirika wa mafuriko Kilosa ukifadhiwa na Ubalozi wa Umoja wa Ulaya. Kushoto kwake ni Msimamizi wa mradi wa FAO kijiji cha Kiroka mkoani Morogoro, Ajuaye Sigalla.

Alisema kwamba amefurahishwa sana na mradi huo na kusema kwamba Umoja wake utaendelea kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa na serikali katika kuhakikisha kwamba mwananchi wa kawaida wa Tanzania anapata maisha bora.

Mradi wa Kiroka ambao unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya FAO na benki ya NMB ikishirikiana na RaboBank umelenga kuboresha kilimo cha Mpunga na pia kuwawezesha wakulima hao kuwa na nafasi ya kupata fedha za kuendeleza majukumu yao.

Ili kufanikisha hilo wakulima wanapatiwa elimu ya fedha na pia utunzaji wa nafaka wa pamoja na mikakati ya mauzo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi akifafanua jambo wakati akitoa salamu kwa wanakikundi wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI). Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kiroka, Mbaraka Mnebe, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez pamoja na Msimamizi wa mradi wa FAO kijiji cha Kiroka mkoani Morogoro, Ajuaye Sigalla.

Mradi huo ulioanza 2004 na kutarajiwa kuisha Juni mwakani unatekelezwa 2018 umelenga kufungua fursa kwa wanawake na wanaume na kuongeza uzalishaji, kusaka masoko, kupata  njia ya kupata  mikopo na kujenga uwezo wa kufanikisha shughuli za maendeleo kwenye skimu.

Mradi huo unatarajiwa kutumia dola za Marekani 737,000 hadi utakapokamilika.

Wakizungumza na  balozi huyo  kuelezea mazingira yao wakulima walishukuru msaada unaotoka katika mashirika ya kimataifa na kuwaomba kusaidia kuwapatia fursa zaidi za maendeleo kwa elimu wanayoipata.

Wamesema mabadiliko yaliyosababishwa na elimu yamewafanya wazalishe Mpunga kwa wingi katika eneo dogo na kufungua fursa za masoko kwa hifadhi na utafutaji masoko wa pamoja.

Katibu wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI), Muhidin Kigadu akielezea mafanikio waliyoyapata tangu walipoanza kupewa mafunzo ya kilimo bora yanayofadhiliwa na Shirika la FAO mbele ya ugeni huo.

Mradi huo ambao ulianza na Watu wa Sua kama watoa elimu sasa wanapigwa msasa na Taasisi ya maendeleo mjini na Vijijini (RUDI) kwa lengo la kuhakikisha kwamba wanatumia mfumo wa Asia wa ulimaji wa Mpunga kwa kutumia maji kidogo huku wakihifadhi ghalani kusubiri bei nzuri.

Katika ziara hiyo ya karibuni ya Balozi huyo akiambatana na  Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez,  viongozi hao walipata nafasi ya kusikiliza changamoto za wakulima katika mradi huo ambapo uzalishaji sasa umeongezeka kutoka gunia tano kwa eka kufikia gunia 25 kwa kulima kitaalamu.

Katibu wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI), Muhidin Kigadu alisema mradi huo ambao ulianza Februari 21,2012 umewajengea uwezo wakulima wa mlimani kutengeneza makinga maji  huku wakulima wa kwenye skimu wakilima kilimo cha mashadidi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kiroka, Mbaraka Mnebe akielezea jinsi skimu ilivyowasaidia kuinua maisha ya wananchi kwa kuwapatia elimu iliyowaletea mafanikio  makubwa yaliyowezesha kulima kisasa na kubadilisha maisha yao hasa katika makazi na huduma za jamii na kuwapeleka watoto shule.

Alisema wanawashukuru wahisani kwa kuwawezesha kurejesha uoto wa kijani ikiwa na pamoja na kuwa na kilimo cha matunda.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Kiroka, Mbaraka Mnebe amesema skimu imewasaidia kuinua maisha ya wananchi kwa kuwapatia elimu iliyowaletea mafanikio  makubwa yaliyowezesha kulima kisasa na kubadilisha maisha yao hasa katika makazi na huduma za jamii na kuwapeleka watoto shule.

Aidha wakulima wamefanikiwa kununua vyombo vya usafiri vya moto kama Pikipiki na kuachana na Baiskeli.

Mwanachama wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI), mkoani Morogoro, Bi. Asha Bogasi akitoa ushuhuda jinsi maisha yao yalivyobadilika mpaka wanaweza kusaidia na waume zao kusomesha watoto wao kutokana na skimu ya mradi huo.

Hata hivyo amesema  pamoja mafanikio hayo wanachangamoto hasa ya masoko na elimu ambayo wanadhani wanaihitaji zaidi huku akisisitiza zaidi kwamba elimu inatakiwa hata kama wamemaliza mradi  na wahisani kuondoka.

Mradi bado ambao haujakamilika kwani kati ya hekta 147 za mradi ni kama hekta 40 zinazotumuka kwa kuwa miundombinu haijatawanyika vya  kutosha katika hekta zote.

Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na kuwapa pongezi za kuweza kubadilisha maisha yao kupitia kilimo cha kisasa kinachofadhiliwa na FAO kwa wanachama wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI) alipofanya ziara ya kukagua mradi huo kijijini hapo.

Wanachama wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI) wakiwa wamekusanyika kwenye shule ya msingi Kiroka wakati wa ugeni wa Shirika la Umoja wa mataifa na Ubalozi wa Umoja wa Ulaya ulipowatembelea kukagua miradi yao.

 Mratibu mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na Balozi wa Umoja wa Ulaya wakiondoka kijijini hapo mara baada ya kukutana na kuzungumza na Wanachama wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI).

No comments:

Post a Comment