Rais wa Namibia anayeondoka Hifikepunye Lucas Pohamba kwenye picha iliyopigwa Agosti 17, 2010 mjini Windhoek. Picha/AFP
Na JOHN NJAGI
Kwa Mukhtasari
Rais
wa Namibia anayeondoka Bw Hefikepunye Pohamba, ameibuka mshindi wa tuzo
ya 2014 ya kiongozi bora barani Afrika na kumwangusha aliyekuwa rais wa
Kenya Mwai Kibaki aliyestaafu 2013. Atapokea Sh460 milioni.
RAIS wa Namibia anayeondoka Bw Hefikepunye Pohamba, ameibuka
mshindi wa tuzo ya 2014 ya kiongozi bora barani Afrika iliyotolewa na
wakfu wa Mo Ibrahim na kumwangusha aliyekuwa rais wa Kenya Mwai Kibaki
aliyestaafu 2013.
Bila kutoa sababu zozote, mwenyekiti
wa kamati ya kusimamia tuzo hiyo ambaye alikuwa katibu wa uliokuwa
Umoja wa Afrika (OAU) kwa sasa Muungano wa Afrika (AU) Dkt Salim Ahmed
Salim alitangaza kwamba Bw Pohamba alimshinda Bw Kibaki na viongozi
wengine waliostaafu miaka mitatu iliyopita.
“Ninawahakikishia kuwa Rais Kibaki alikuwa miongoni mwa walioteuliwa kwa tuzo hiyo lakini alishindwa,” akasema.
Kwa kutoa mamlaka kwa amani,
kuanzisha mabadiliko muhimu chini ya uongozi wake kama vile elimu ya
bure katika shule za msingi na upili na miradi mikubwa ya miundo misingi
pamoja na kupanua demokrasia nchini, ilitarajiwa kuwa Rais Kibaki,
angetwaa tuzo hiyo.
Hata hivyo, aliangushwa na Bw Pohamba ambaye
licha ya kutawala moja ya nchi changa kidemokrasia barani Afrika kwa
mwongo mmoja, hakujulikana mno.
Bw Pohamba alivutia kamati kwa kuleta mageuzi katika nchi yake kwa muda mfupi, kukumbatia demokrasia na utawala bora.
Kufuatia ushindi huo, Rais huyo
atatia kibindoni zawadi ya dola 5 milioni (Ksh460 milioni) atakazolipwa
kwa kipindi cha miaka 10 na baadaye dola 200,000 (Ksh18 milioni) kila
mwaka katika maisha yake yote.
Mwanzilishi wa tuzo hiyo, Bw Mo
Ibrahim, alisema Rais Pohamba aliyeondoka mamlakani Desemba mwaka jana
lakini hajatoa mamlaka bado kwa sababu mrithi wake hajaapishwa, ni
kiongozi wa kuigwa barani Afrika.
Unyenyekevu
“Afrika sio tu kuhusu viongozi
wabaya kama Mobutu Seseseko na wengine. Kuna viongozi wanyenyekevu
wanaoendelea kujitolea mhanga kwa ajili ya watu wa nchi zao,” akasema Bw
Ibrahim.
Bw Salim Ahmed Salim alisema
Namibia imepiga hatua kwa kutoa elimu ya bure, kupunguza viwango vya
ukimwi, kuimarisha usawa wa jinsia na kadhalika kwa kuwa na asilimia 48
ya wabunge wanawake ingawa kuna changamoto za kiuchumi na usawa wa
kijamii.
Waliowahi kushinda tuzo hiyo awali ni aliyekuwa rais wa Musumbiji
Joaquim Chissano, (2007) Festus Mogae wa Botswana (2008) na Pedro Pires, Cape Verde (2011).
Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini
Nelson Mandela alitangazwa mshindi wa heshima tuzo ilipozinduliwa
2007. Hakukuwa na washindi 2009, 2010, 2012 na 2013 baada ya kamati
kusema hakuna aliyestahiki kuipata.
No comments:
Post a Comment