Rais Dkt.Jakaya mrisho Kikwete akifungua mkutano wa Viongozi wa
Kamati ya
Amani Mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere(JNICC) jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali wakimsikiliza kwa
makini Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akiwahutubia wakati wa
ufunguzi wa Mkutano wa Viongozi wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam
leo.(picha na Freddy Maro).
<<<<<<<<<<<<<<<< >>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>
RAIS Jakaya Kikwete amefafanua msimamo wa Serikali katika mjadala unaoendelea wa Mahakama ya Kadhi, na kuweka wazi kuwa Serikali haina mpango wa kuianzisha, wala kuiendesha.
<<<<<<<<<<<<<<<< >>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>
RAIS Jakaya Kikwete amefafanua msimamo wa Serikali katika mjadala unaoendelea wa Mahakama ya Kadhi, na kuweka wazi kuwa Serikali haina mpango wa kuianzisha, wala kuiendesha.
Mbali na hiyo, Rais Kikwete
ambaye jana alizungumza na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani
Dar es Salaam, pia alielezea kusikitishwa kwake na tamko la Jukwaa la
Wakristo Tanzania, lililowaelekeza waumini wao kupigia Katiba
Inayopendekezwa kura ya Hapana.
Mahakama ya Kadhi
Akifafanua suala la Mahakama ya Kadhi, Rais Kikwete alisema Serikali ina msimamo wa mambo mawili katika mahakama hiyo.
Kwanza, alisema Serikali haina mpango wa kuianzisha na kuiweka katika
Katiba na pili, haihusiki kuiendesha na badala yake, Waislamu wenyewe
ndio watakaoiendesha.
Alisema kimsingi, mahakama hiyo ilikuwepo kabla ya Uhuru na
kinachotakiwa kuzungumzwa ndani ya Bunge, ni Sheria ya Kutambua Uamuzi
Unaofanywa na Kadhi.
Alifafanua zaidi kuwa Mahakama hiyo ya Kadhi, haihusiki na mambo ya
jinai, isipokuwa mambo ya kijamii ikiwemo talaka, mirathi na mengine ya
aina hiyo.
Alitoa mfano wa Sheria ya Kiislamu, iliyokuwepo tangu zamani, ambayo
inatambua chombo hicho na kusisitiza kuwa kinazungumzwa, ni uamuzi
unaofanywa na Kadhi utambulike tu.
Katika mfano huo, alisema Muislamu ukigombana na mke wake, kuna mabaraza
ya usuluhishi ambayo huyo mwanamke atapaswa kwenda, ila wakishindwa na
ataomba talaka ambayo inaidhinishwa na Kadhi, ambaye ndiye msajili wa
vyeti vya ndoa kwa Waislmau.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Shehe Alhad
Musa, alimshukuru Rais Kikwete kwa ufafanuzi alioutoa na kusema Wakristo
na Waislamu siku zote ni wamoja na wataendelea kuishi kwa amani, furaha
na ushirikiano.
Katika hilo, Shehe Alhad alinukuu Biblia katika Kitabu cha Mathayo tano,
mstari wa 25, ambao unasema; “Patana na mshitaki wako, mngali njiani,
asije akakupeleka kwa Kadhi na Kadhi akakukabidhi kwa Polisi na Polisi
akakutupa korokoroni.”
Katiba Pendekezwa
Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, ambayo inasubiri kupigiwa kura na
wananchi, Rais Kikwete alisema Katiba hiyo imewakilisha vitu vingi
kuliko Katiba iliyopo.
Alifafanua kwamba Katiba Inayopendekezwa, imeweka haki za makundi
mbalimbali ya jamii, kuliko iliyopo na kuongeza kuwa yeye binafsi
ameisoma na kurudia kuisoma, lakini hajaona mahali popote ambapo ina
kasoro.
Alisema isingekuwa rahisi kuweka maoni ya kila mtu katika Katiba, na
kufafanua kuwa yale ambayo hayajawekwa sasa hivi, utafika wakati wake na
yatawekwa.
Alibainisha kuwa haikuwa rahisi kwa maoni ya kila mtu kuingia katika
Katiba Inayopendekezwa, kwani hata CCM ilikuwa na mambo 60
waliyopendekeza, lakini kati ya hayo ni 12 tu yaliyoingia.
Rais Kikwete alisema Katiba sio Msahafu au Kurani, ambayo haiwezekani
kubadilishwa hata nukta. Alitoa mfano wa Zanzibar, kwamba wakati kuunda
Muungano, yapo mambo yalionekana ni muhimu kubakia katika Muungano,
lakini kadri muda ulivyokwenda yameondoka.
Jukwaa la Wakristo
Akizungumzia tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania, Rais Kikwete alisema
amehuzunishwa na kufadhaishwa na tamko hilo la viongozi wa dini la
kutaka waumini wao wajiandikishe kwa wingi, lakini wapige kura ya Hapana
kwa Katiba Inayopendekezwa.
Tamko hilo lilitolewa na jukwaa hilo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la
Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).
Rais Kikwete alisema, tamko hilo litakuwa pia limekwaza waumini, kwa
kuwawekea mipaka ya kidemokrasia na kukwaza hata viongozi wenyewe.
Alitoa mfano kwamba kwa tamko hilo, muumini hataweza kusimama na
kumwambia kiongozi wa dini asiwaingilie katika uamuzi, kwa kuwa kupiga
kura ni haki ya kikatiba ya kila mtu, na ikitokea hivyo, hata kiongozi
husika atakwazika.
Subira kwa NEC
Kuhusu uwezekano wa Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30 kama
ilivyotangazwa na Serikali, huku kazi ya kuandikisha wapigakura
ikiendelea kusuasua, Rais Kikwete alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), inayoratibu uandikishaji wa wapigakura, itazungumza kuhusu
walipofikia wakati muafaka ukifika.
Amani
Kuhusu amani ya nchi, Rais Kikwete alisema viongozi wa dini pia wa jukumu kubwa la kuimarisha amani ya nchi.
Katika utekelezaji wa jukumu hilo, Rais Kikwete aliwataka viongozi hao
wajaribu kuepuka kutumiwa na watu wenye nia mbaya, kwa sababu wanafahamu
kuwa viongozi wa dini wana ushawishi katika jamii na wana watu wengi
nyuma yao.
Alisema machafuko yatakayotokana na mvurugano wa kidini, hakuna mtu
atakayeweza kuyazuia, hivyo ni vyema viongozi hao waendeleze mshikamano.
Alitoa mwito kwa mikoa mingine nchini, kuunda kamati za amani kama
ilivyo Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment