Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, alipofika
eneo la Vikunguni kwa ajili ya kuzindua mradi wa maji safi na salama
katika eneo hilo.
Bango la mradi wa maji Vikunguni baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mradi huo.
Baadhi
ya wananchi pamoja na wakandarasi wa kampuni ya SINO-HYDRO LTD ya
China, wakimsikiliza Maalim Seif wakati akiwahutubia wakati wa uzinduzi
wa mradi huo.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama
katika eneo la Vikunguni.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiagana
na wananchi baada ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama katika
eneo la Vikunguni. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad (OMKR).
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema
kuimarika kwa huduma za maji safi na salama nchini kutasaidia harakati
za uzalishaji pamoja na shughuli za kiuchumi.
Umesema
huduma hiyo pia husaidia kuokoa muda hasa kwa akinamama ambao mara
nyingi hukabiliwa na jukumu la kutafuta maji kwa matumizi ya nyumbani.
Maalim
Seif ametoa kauli hiyo wakati akifungua mradi wa maji safi na usafi wa
mazingira katika eneo la Vikunguni jimbo la Wawi katika Wilaya ya Chake
Chake, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Ameelezea kufarajika kwake kutokana na mradi huo kuanza kuwanufaisha wananchi wengi wa eneo hilo pamoja na vijiji jirani.
Amefahamisha
kupatikana kwa huduma hiyo ya uhakika, pia kutasaidia kujikinga na
maradhi ya miripuko yakiwemo kipindupindu ambayo mara nyingi
husababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.
Amewasisitiza wananchi kuulinda na kuutunza mradi huo, ili uweze kuwa endelevu na kuweza kutumika kwa muda mrefu.
Sambamba
na hilo Maalim Seif amewataka wananchi hao kuepukana na uharibifu wa
mazingira, ili kujikinga na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni
pamoja na kusababisha kukauka na kuchafuka kwa vyanzo vya maji.
Ameeleza
kuwa tayari vijiji kadhaa vya Zanzibar kikiwemo kijiji cha Nungwi,
tayari kimekumbwa na athari hizo kwa visima vyao kuingiliwa na maji ya
chumvi, na kuvitaka vijiji vyengine kuchukua tahadhari juu ya athari
kama hizo.
Mapema
akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na
Nishati Mhe. Ramadhan Abdallah Shaaban, amesema lengo la Serikali ni
kuhakikisha kuwa wananchi wa Zanzibar wanapata maji kwa asilimia 85
ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Amesema tayari ujenzi wa miradi ya maji mijini na vijijini umeshafikia asilimia 90 ambapo kazi ya usambazaji inaendelea vizuri.
Akisoma
taarifa ya kitaalamu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Mustafa
Aboud Jumbe, amesema zaidi ya shilingi bilioni mbili nukta tatu
zimetumika kukamilisha mradi huo wa maji Vitongoji.
Amesema
mradi huo ulioanzishwa mwaka 2011 ulijengwa chini ya ukandarasi wa
kampuni ya SINO- HYDRO ya China, na uligharamiwa kwa pamoja na Benki ya
Maendeleo ya Afrika (ADB), UN-Habitat na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Amefahamisha kuwa Serikali imo katika utaratibu wa kulipatia ufumbuzi
tatizo la umeme katika visima na matangi ya maji ili kuhakikisha kuwa
huduma hiyo inapatikana kwa uhakika.
Katika
risala yao wananchi hao wa Vikunguni wameishukuru Serikali na washirika
wa maendeleo kwa kuwapelekea mradi huo ambao umeondosha kero ya
upatikanaji wa maji safi na salama iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment