UTALII WETU : JUHUDI ZA UONGOZI WA MKOA WA RUKWA KUENDELEZA UTALII WA MAPOROMOKO YA KALAMBO (KALAMBO FALLS) ZAENDELEA - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Thursday, 7 August 2014

UTALII WETU : JUHUDI ZA UONGOZI WA MKOA WA RUKWA KUENDELEZA UTALII WA MAPOROMOKO YA KALAMBO (KALAMBO FALLS) ZAENDELEA

Kaimu Afisa Ardhi na Maliasili Wilaya ya Kalambo Ndugu Makwasa Biswalo (katikati) akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya eneo lililopimwa katika kijiji cha Kapozwa kwa ajili ya kuendeleza Utalii katika Kijiji hicho ambacho kina maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls), maporomoko ambayo ni ya pili kwa urefu barani Afrika yakiwa na urefu wa mita 235. 

Zipo jitihada kadhaa zilizokwishafanywa na uongozi wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Eng. Stella Manyanya katika kuhakikisha eneo la maporomoko hayo linaimarishwa na kuwa kivutio kikubwa cha utalii na chanzo cha mapato kwa halmashauri husika na taifa kwa ujumla. 

Jitihada hizo ni pamoja kuwahamasisha wananchi wa kijiji cha Kapozwa na wadau wengine katika kutambua umuhimu wa maporomoko hayo ambapo mpaka hivi sasa wananchi hao wameshashiriki kufyatua matofali kwa ajili ya kujenga kituo cha utalii katika eneo hilo.

 Jitihada zingine ni zile za kupima viwanja na kuandaa michoro katika eneo hilo ambapo ramani imeshaidhinishwa na tathmini ya kuwafidia wananchi maeneo yao imeshafanyika. 

Aidha zimekuwepo jitihada za kutafuta fedha kutoka Serikalini na kwa wahisani mbalimbali katika kusaidia kujenga na kuimarisha utalii katika maporomoko hayo (Kalambo Falls). Wakala wa Misitu Taznania (TFS) wamesaidia upatikanaji wa kiasi cha fedha (Tsh. Mil. 10) ambazo zitasaidia kufungua baadhi ya mitaa katika eneo liliopimwa na shughuli zingine zitakazohitajika katika eneo hilo.  

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya anawaomba wadau wote wa utalii nchini ikiwemo Serikali, Mashirika binafsi, Wawekezaji na Wahisani mbalimbali kuwa na jicho la pamoja katika kuona Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls) yanachukuliwa umuhimu wa pekee wa kuendelezwa na kutangazwa kwa nguvu kwani ni miongoni mwa kivutio kikubwa cha utalii nchini na barani Afrika kwa ujumla. 

Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls) yenye urefu wa mita 235 yapo Mkoani Rukwa katika Wilaya ya Kalambo na ni sehemu ya mpaka kati ya Nchi ya Tanzania na Zambia. Nchi ya Zambia imekuwa ikitumia fursa ya mpaka huo kuendeleza eneo lao la mpakani na kuitangaza Kalambo Falls jambo ambalo likiachwa kwa muda mrefu bila Tanzania kuchukua hatua kama hiyo itapelekea dunia kubaki na picha isiyo sahihi kuwa maporomoko hayo yapo nchini Zambia wakati sehemu kubwa ipo Tanzania na hata muonekano mzuri unapatikana kutokea Tanzania na maji ya mto huo yanatokea Tanzania. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akiangalia ramani ya viwanja vilivyopimwa katika kijiji cha Kapozwa kwa ajili ya kuendeleza utalii katika kijiji hicho cha mpakani na nchi ya Zambia yalipo maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls). Mkuu huyo wa Mkoa alikabidhiwa ramani hiyo na Kaimu Afisa Ardhi na Maliasili Wilaya ya Kalambo Ndugu Makwasa Biswalo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya na Meneja wa Misitu Wilaya ya Sumbwanga na Kalambo Ndugu Martin Hamis wakipanda mti wa kumbukumbu katika eneo lililopimwa la kijiji cha kapozwa kwa ajili ya kuendeleza utalii wa maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls). 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya na wapimaji wa ardhi kutoka chuo cha Ardhi Morogoro waliokuwa wakishirikiana na wataalamu wa ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kupima ardhi ya kijiji cha Kapozwa kwa ajili ya kuiendeleza kiutalii wakiangalia Maporomoko ya Moto Kalambo (Kalambo Falls).  
Sehemu ambayo ni nusu ya maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls). 
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Smythies Pangisa akiangalia bonde la maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls).
Sehemu ya jitihada za wananchi wa kijiji cha Kapozwa ambao wamefyatua matofali kwa ajili kujenga kituo cha utalii kwa ajili ya maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls).
Sehemu ya mchoro kwa ajili ya kujenga kituo na geti la utalii katika maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls). Jitihada hizi zimefanywa na uongozi wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Eng. Stella Manyanya.
Vijana wa nchi jirani ya Zambia wakiwa wanapunga upepo kandokando ya maporomoko ya mto Kalambo. Upande wa nyuma zinaonekana ngazi maalum ambazo ni sehemu ya miundombinu iliyojengwa na Serikali ya Zambia kuwavutia watalii katika eneo hilo. Serikali ya Tanzania ina changamoto kubwa ya kuhakikisha eneo hilo muhimu la utalii linaendelezwa ili kulijengea umiliki halali tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo inaonekana limetelekezwa kwa muda mrefu.
Sehemu ya bonde ambalo ni maangukio ya maji ya mto Kalambo yanapotengenezwa maporomoko (Kalambo Falls).Picha Hamza Temba - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

No comments:

Post a Comment