Gari
aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T.589 AZS likiwa limebeba
magunia ya madawa ya kulevya aina ya bhangi mara baada ya kukamatwa
eneo la Sanawari jijini Arusha na askari wa kitengo cha kuzuia Madawa ya
Kulevya mkoani hapa
Jeshi la Polisi Mkoani
Arusha limewakamata watu watano wakiwa
na magunia saba ya madawa ya kulevya aina ya bhangi wakiwemo mke na mume. Awali
askari wa Kitengo cha Kuzuia Madawa ya Kulevya Mkoani hapa wakiwa doria
walipata taarifa toka kwa raia wema iliyoeleza kuwepo kwa watu wanaosafirisha
madawa hayo.
Mara baada ya kupata
taarifa hiyo askari hao waliweka mtego maeneo ya Sanawari ambapo muda wa saa
3:30 usiku walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Hussein Rashid
(35) mkazi wa Sakina, dereva pamoja na mwenzake Sebastian Wilbert (37) Fundi
magari, mkazi wa Ilboru wakiwa wanasafirisha magunia matano ya madawa ya kulevya
aina ya bhangi yenye uzito wa kilogramu 171 kuelekea nchi jirani ya Kenya kwa
kutumia gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T. 589 AZS.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba, mara baada ya
watuhumiwa hao kuhojiwa walikiri kosa hilo na kumtaja mwanamke aitwaye Flora
John (38) Mkazi wa Ekenywa- Ngaramtoni kuwa ndio aliyewauzia.
Kamanda Sabas
aliendelea kwa kusema kwamba, askari hao walianza kumfutilia mwanamke huyo ambapo
jana Jumanne tarehe 05.08.2014 walikwenda nyumbani kwake na kumkuta mtuhumiwa ambaye ni muuzaji
akiwa na mume wake aitwaye John Meleji (45) Mkazi wa Ekenywa na mara baada ya kufanya
upekuzi walikuta gunia moja la madawa ya kulevya aina bhangi ndani ya nyumba
hiyo.
Mbali na kuwakamata watuhumiwa
hao ambao ni mke na mume pia askari hao walimkamata jirani yao aitwaye
Loseriani Metelami (21) Mkulima mkazi wa Ekenywa baada ya yeye pia kukutwa na
gunia moja la madawa ya kulevya aina ya bhangi hivyo kufanya jumla ya magunia
yaliyokamatwa kuwa saba.
Watuhumiwa hao watano wanatarajiwa kufikishwa
mahakamani hivi karibuni mara baada ya upelelezi kukamilika. Kwa hisani ya Woinde Shizza Blog
No comments:
Post a Comment