Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda - Washington
Imeelezwa
kwamba kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa wa saratani ya
mlango wa kizazi, upungufu wa upatikanaji wa huduma za afya, na vitendea
kazi, utungaji wa sera zisizo rafiki, pamoja na ukosefu wa takwimu za
magonjwa ni moja ya sababu zinazosababisha wanawake wengi kupoteza
maisha kutokana na ugonjwa huo.
Hayo
yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akitoa neno la
shukrani kwa niaba ya wake wa marais wa Afrika waliohudhuria hafla fupi
ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na kituo cha Marais wa Afrika
(African Presidential Centre) cha chuo kikuu cha Boston iliyofanyika
mjini Washington.
Mama
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)
alisema kwa kiasi kikubwa kuna mahusiano kati ya ugonjwa wa Ukimwi na
Saratani ya mlango wa kizazi ambao kama mgonjwa atapata matibabu mapema
atapona lakini kutokana na uelewa mdogo baadhi ya wanawake wanapoteza
maisha.
“Kutokana
na utaalamu uliopo sasa ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi
unazuilika na kutibika lakini bado kuna uelewa mdogo katika jamii kuhusu
uhusiano uliopo kati ya ugonjwa huu na ule wa Ukimwi; kama
zitapatikana fedha za kutosha asasi zisizo za kiserikali ambao ni
wawezeshashi wataweza kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na magonjwa haya”,
alisema Mama Kikwete.
Akiongelea
kuhusu maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi Mama Kikwete alisema ugonjwa huo
unasababisha vifo vya watu wengi lakini bado kuna magonjwa mengine
ambayo ni tishio nchini kama Malaria na Kifua kikuu ambayo nayo yanaua
watu wengi.
Alisema,
“Ugonjwa wa Ukimwi unasababisha vifo vya wanawake wengi nchini kwa
upande wa vijana watoto wa kike wanaathirika zaidi ukilinganisha na
watoto wa kiume na kwa watu wazima wanawake wengi wanapata maambukizi
zaidi ukilinganisha na wanaume.
“Maambukizi
ya ugonjwa wa Ukimwi yamepungua kutoka asilimia 7 kwa mwaka 2004 hadi
kufikia asilimia 5.1 mwaka 2012 kwa upande wa Tanzania Bara na kwa
upande wa Zanzibar maambukizi ni asilimia 0.6% kwa miaka yote hiyo”.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema vituo vya kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi
(VVU) vimeongezeka kwa sababu vituo vilivyokuwa vinatoa huduma ya
uzazi na watoto wachanga hivi sasa vinatoa huduma ya upimaji wa
maambukizi ya VVU lakini bado jitihada kubwa zaidi zinahitajika
kufanyika ili kuwe na vituo vingi vya kutoa huduma hiyo.
Kwa
upande wa vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vimepungua
kutoka 147 kwa kila vizazi hai 1000 kwa mwaka 1999 hadi kufikia vifo
81 kwa mwaka 2010. Vifo vya watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja
vimepungua kutoka 99 na kufikia 51 kwa kila vizazi hai 1000 ingawa
tatizo limepungua hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa ili kuimarisha afya
ya watoto.
Kuhusu
vifo vya kina mama wajawazito alisema vimepungua kutoka 578 kati ya
vizazi hai 100,000 mwaka 1996 hadi kufikia 454 kati ya vizazi hai
100,000 kwa mwaka 2010 hii inatokana na jamii kuwa na uelewa juu ya
umuhimu wa mwanamke kuhudhuria kliniki mapema pindi apatapo ujauzito na
kujifungulia katika vituo vya afya .
Mama
Kikwete alisema, “Vifo vingi vya kina mama wajawazito vinatokana na
kutofuata uzazi wa mpango na uchumi mdogo wa wanawake, utoaji wa mimba
usio salama, kuvunja damu nyingi wakati wa kujifungua, kifafa cha mimba,
kushindwa kujifungua, uhaba wa huduma za haraka za uzazi na huduma za
mtoto mchanga na uhaba wa watoa huduma za afya waliobobea,”.
Aliendelea
kusema vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua vinahusiana na afya ya
mama wakati wa ujauzito, hali ya kujifungua na jinsi ya kumjali mtoto
wakati wa kujifungua. Mwanamke atakayejifungua mtoto akiwa na umri mdogo
atakuwa na watoto wengi ambao umri wao haujapishana hayo yote yana
madhara kwa afya ya mama na mtoto .
“Ili
kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga, ugonjwa wa
saratani ya matiti na mlango wa kizazi na Ukimwi hasa kuzuia maambukizi
ya ugonjwa huu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto Taasisi ya WAMA inafanya
kazi ya uraghibishi kwa kutoa vifaa tiba na elimu ya uzazi kwa vijana.
Tunawakaribisha ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja ya kuokoa maisha ya
mama na mtoto wa Tanzania”, alisisitiza Mama Kikwete.
Akiwakaribisha
wake hao wa Marais Mkurugenzi wa Kituo cha Marais wa Afrika Balozi
Charles Stith aliwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya katika nchi zao
ya kujali afya ya mama na mtoto na kuwataka waendee na kazi hiyo bila ya
kukata tamaa kwani wao kama viongozi wanahitajika katika kutatua
changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii inayowazunguka.
Balozi
Stith alisema kituo chake kinatambua mchango wao na kazi wanayoifanya
hasa katika kushughulikia afya ya mama na mtoto na upatikanaji wa elimu
ya mtoto wa kike na kuhahidi kuwa kituo hicho kitaendelea kushirikiana
nao ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Mama
Kikwete anauhudhuria mkutano wa wake wa Marais wa Afrika ulioandaliwa
na Mke wa Rais wa Marekani Mama Michelle Obama kwa kushirikiana na
Taasisi ya George W. Bush ambao unajadili matatizo ya vifo vya kina
mama wajawazito na watoto, ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi na
matiti na elimu ya mtoto wa kike.
No comments:
Post a Comment