Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akizungumza na Rais wa Burundi Mhe. P. Nkurunziza alipomtembelea
Ofisini kwake Ikulu jijini Bujumbura jana Julai 02-2014.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akizungumza na waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali vya
Burundi Ikulu jijini Bujumbura jana ambapo alizungumzia kuhusu
kuimarisha ushirikiano kati ya Nchi mbili hizi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na baadhi ya Viongozi
wa Serikali ya Burundi kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura
jana baada ya kuhudhuria maadhimisho ya miaka 52 ya Uhuru wa nchi hiyo. Picha na OMR
*************************************
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA BURUNDI, MHESHIMIWA PIERRE NKURUNZINZA
Julai 02, 2014: Bujumbura
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
leo Jumatano Julai Pili, 2014 amekutana na Rais wa Burundi Mheshimiwa
Pierre Nkurunzinza na kufanya naye mazungumzo. Mazungumzo hayo
yamefanyika katika Ofisi ya Rais Nkurunzinza iliyopo katikati ya jiji la
Bujumbura.
Katika
mazungumzo hayo, viongozi hao walipata fursa ya kubadilishana mawazo
kuhusu uhusiano baina ya Tanzania na Burundi ambapo Mheshimiwa Makamu wa
Rais alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Nkurunzinza na watu wa
Burundi kwa sherehe zilizofana za kutimiza miaka 52 ya uhuru. Pia
alitumia nafasi hiyo kumtakia kila la heri Mheshimiwa Rais Nkurunzinza
pamoja na watu wa Burundi kufuatia kupiga hatua kubwa za kimaendeleo
sambamba na kuweza kuwafanya wananchi wa Burundi kuwa wamoja.
Pia
alimueleza Rais Nkurunzinza kuhusu umuhimu wa kuzidi kuifanya Burundi
kuwa nchi moja kwa kuwaunganisha watu wake na akaeleza kuwa, Tanzania
inafurahi kuona hatua kubwa za kimaendeleo zikipigwa nchini Burundi na
kwamba ili hatua hizo ziwe madhubuti, upo umuhimu wa kuwafanya wananchi
wa Burundi kubakia wamoja na wanaoshirikiana katika kuiendeleza nchi
yao.
“Burundi
ikifanya vizuri maana yake ni kuwa Afrika Mashariki imefanya vizuri.
Tanzania tutafurahi na nchi zote za ukanda wetu zitafurahi,” alisema
Mheshimiwa Makamu wa Rais na kuongeza kuwa lengo la Tanzania siku zote
ni kuona jirani zake wakiishi kwa utulivu na wakifanya mambo yao ya
maendeleo katika hali ya amani.
Katika
mazungumzo hayo Rais Nkurunzinza aliendelea kuishukuru Tanzania kwa
uhusiano wake wa karibu na Burundi na akaongeza kuwa wananchi wa nchi
yake wamefurahishwa sana kwa Tanzania kushiriki katika sherehe za miaka
52 ya Uhuru wa Burundi, sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Prince
Louis Rwagasore jana. Pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Tanzania,
sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Somalia na Waziri
Mkuu wa Chad.
Msafara
wa Mheshimiwa Makamu wa Rais umeondoka leo jijini Bujumbura na kurejea
jijini Dar es Salaam tayari kabisa kuendelea na majukumu mengine ya
kitaifa. Katika msafara huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais aliambatana na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman na
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa
Mahadhi Juma Maalim.
Imetolewa na:Ofisi ya Makamu wa Rais
Julai 2, 2014 Bujumbura: Burundi
No comments:
Post a Comment