TUTUNZE UTALII WETU :NEW YORK YAMJADILI TENA TEMBO, CHELSEA CLINTON AONGOZA MAJADILIANO, TANZANIA YASHIRIKI - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


26 Feb 2014

TUTUNZE UTALII WETU :NEW YORK YAMJADILI TENA TEMBO, CHELSEA CLINTON AONGOZA MAJADILIANO, TANZANIA YASHIRIKI


Moja ya picha mbalimbli za Tembo zilipamba ukumbi yalipofanyika majadiliano kuhusu tembo, picha hizo na ambazo zilikuwa kivutio kwa washiriki wa majadiliano hayo ziliandaliwa na National Geograpy.
Chelsea Clinton, Makamu Mwenyekiti wa Clinton Foundation, na ambaye aliongoza majadiliano hayo akiwatambulisha wanajopo, kutoka kushoto ni Bw. John Heminway, Balozi Tuvako Manongi, kati kati ni Chelsea Bint wa Rais Bill na Hilary Clinton, kulia kwa Chelsea ni Bw. Bryan Christy na anayefuatia ni Bw. Josh Ginsberg kutoka Wildlife Conservation Society. Heminway na Christy ni waandishi na watunga filamu na kwa pamoja wametengeneza filamu ijulikanayo kama "The Battle for Elephants". Filamu hiyo itaonyeshwa February 27 kupitia Channel ya National Geograpy.
Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Manongi, akielezea jambo wakati wa majadiliano kuhusu tembo na changamoto zinazomkabili. Balozi Manongi alitumia fursa hiyo kuelezea juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya ujangili na udhibiti wa biashara haramu ya pembe za tembo.
Bw. Bryan Christy naye akieleza jambo, Bw. Christy ameshiriki katika kutengeneza filamu ya The Battle for Elephants, habari zaidi zinaonyesha kwamba sehemu ya filamu hiyo inahusu Tanzania, na Bw. Christy anaonekana kwenye filamu hiyo akipozi kama mnunuzi wa meno ya tembo.
Sehemu ya washiriki waliohudhuria majadiliano hayo ambapo pia walipata fursa ya kuuliza maswali kwa wanajopo.
Hapana shaka kwamba Hatari ya kutoweka kwa tembo barani afrika, ni jambo linalowagusa wengi, washiriki wa majadiliano hayo walitumia fursa hiyo kujifunza siyo tu hatari ya kutoweka kwa mnyama huyo, lakini pia uzuri na sifa zake, na namna gani wanaweza kuchangia kuhakikisha hatoweki kabisa.
Waandishi pia walikuwepo nao walipewa changamoto ya kuandika habari zenye kuelimisha jamii kuhusu athari za mauaji holela ya tembo pamoja na kuihamasisha kutambua wajibu na nafasi yao katika uhifadhi wa wanyama walio katika hatari ya kutoweka.
Pichani ni sehemu ya washiriki wa majadiliano hayo

Na Mwandishi Maalum

Zikiwa zimepita wiki chache tangu kufanyika kwa Mkutano uliojadili kwa kina kuhusu ujangili dhidi ya tembo na biashara haramu ya pembe za tembo uliofanyika Jijini London, Uingereza. Jana Jumanne, hapa Jijini New York, Marekani, palifanyika majadiliano mengine yakihusu pia sifa na uzuri wa mnyama tembo na hatari inayomkabili.

Majadiliano hayo na ambayo yaliwavutia washiriki wengi, yaliandaliwa kwa ushirikiano kati ya National Geograpy na ABC na yalifanyika katika jengo lijulikanalo kama ABC HOME lilipo Broadway, jijini New York.

Balozi Tuvako Manongi, Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alikuwa kati ya wanajopo wanne walioalikwa kushiriki majadaliano hayo ambayo yaliongozwa na Chelsea Clinton, Makamu Mwenyekiti wa Clinton Foudantion.

Wanajopo wengine walikuwa ni Bw. Josh Ginsberg kutoka Wildlife Conservation Society, Bw. John Heminway mwandishi na mtengeneza filamu ambaye pamoja na mwanajopo mwingine Bryan Christy wameshiriki katika kutengeneza filamu ijulikanayo kama “The Battle for Elephants” filamu hii inatarajiwa kuonyeshwa february 27 kupitia Channel ya National Geograpy.

Wanajopo hao wakiongozwa na Chelsea Clinton, walipata fursa ya kila mmoja wao kuelezea nini yeyé kama mtu binafsi au kupitia taasisi anayoiwakilisha ametoa mchango gani katika suala zima la uhifadhi wa Tembo na uthibiti wa mauaji holela ya Tembo na biashara haramu ya pembe za tembo.

Balozi Manongi kwa upande wake, alielezea juhudi mbalimbali ambazo serikali inafanya katika kukabiliana na ujangili dhidi ya tembo, pamoja na biashara haramu ya pembe , aidha alielezea dhamira na nia ya serikali ya kuendeleza mapambano ya kuwanusuru tembo kupitia awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza.

Balozi pia alijibu maswali mbalimbali na kutolea ufafanuzi hoja zikiwamo kuhusu kwanini operesheni tokomeza ilisitishwa, na je serikali ilikuwa na mpango gani kuhusu shehena ya pembe za ndovu ambayo iko katika maghala.

Kwa ujumla wanajopo wote walikubaliana kwamba, mapambano dhidi ya ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu ni vita ngumu hasa ikizingatiwa kwamba mtandao unaohusika na biashara ya pembe za tembo ni mpana sana na unaohusisha watu wengi.

Na kwa sababu hiyo wamehimiza mambo kadhaa yakiwamo, ushiriki wa wadau kutoka makundi mbalimbali ya kijamii kitaifa na kimataifa, udhibiti wa soko na hitajio la pembe za ndovu, utoaji wa elimu kwa umma, uwezeshwaji wa watendaji katika ngazi mbalimbali, na uimarishaji wa sheria.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad