Dennis Malle (aliyesimama) ni wakala maarufu wa kuleta wakenya Tanzania kwa kupata 10% bila kujali uzalendo.Picha na Gidabuday Blog |
CHAMA cha Riadha Kenya (AK),
kimesema hakina taarifa za wanariadha wake kwenda Tanzania kushiriki mashindano
mbalimbali mwaka huu.
Desemba 4 mwaka huu yalifanyika
mashindano ya Serengeti Marathon na Desemba 8 Uhuru Marathon na kushirikisha
wanariadha kadhaa kutoka Kenya ambao ilidaiwa kuwa wana barua rasmi za
utambulisho kutoka AK kama inavyotakiwa kisheria.
Suala la mawakala wa Tanzania
kuwachukua wanariadha wa Kenya katika mashindano mbalimbali bila kufuata
taratibu limekuwa likiota mizizi huku Riadha Tanzania (RT), ikishindwa
kulipatia tiba.
Katika mbio za Uhuru Marathon,
zilizagaa habari kuwa mwanariadha Emily Lagat amefariki mara baada ya kumaliza
mbio hizo, kabla ya wakala wake, Dennis Malle, kukanusha huku akibainisha kuwa
ni mzima licha ya kwamba alikuwa majeruhi.
Malle akizungumza kwa simu kutoka
Arusha, alidai kuwa Lagat aliyeshika nafasi ya nne katika mbio hizo, aliumia
katika mbio hizo na kutibiwa kwa muda kisha kuendelea na mbio na kumaliza,
ingawa alikuta zoezi la ugawaji zawadi limekwishamalizika.
Wakala huyo alidai kuwa wanariadha
aliowaleta wote wamerejea Nairobi salama na walikuwa na mialiko rasmi, jambo
ambalo AK imelikanusha.
Akizungumza na Tanzania Daima
jijini hapa jana, Ofisa Uhusiano wa AK, Evans Bosire, alisema hawana taarifa
zao kwani shirikisho hilo halijatoa ruhusa kwa mkimbiaji yeyote kutoka Kenya
kwenda kushiriki mashindano hayo.
Alisema, kama kuna mkimbiaji
amekwenda Tanzania kukimbia, hilo hawalitambui, kwani atakuwa ameenda kwa
mapenzi yake mwenyewe na si kwa ruhusa ya shirikisho. Aliongeza kuwa, endapo mchezaji
atapata tatizo lolote, itakuwa ngumu kwa wao kujua, kwani hawana taarifa zozote
juu yao.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa RT,
Suleiman Nyambui, alidai kuwa, kuna udanganyifu unaofanyika wa barua za ruhusa
na kwamba watalifanyia kazi.
SOURCE: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment