Wafanyakazi wa uwanja wa Ndege wa Arusha wakiangalia ajali ilivyokuwa na watu kunusurika kufa. |
Arusha.Abiria 213 waliokuwa wakisafiri na ndege
ya Shirika la Ndege la Ethiopia jana walinusurika kifo baada ya ndege
hiyo kutua kwa dharura katika uwanja mdogo wa Arusha.
Ndege hiyo aina ya Boeing 767, ilitua saa 6.45
mchana katika uwanja huo baada ya kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kutokana na kupata pancha kwa ndege
nyingine inayomilikiwa Shirika la Ndege la Tanganyika (TFC), kwenye njia
ya uwanja huo.
Ndege ya Ethiopia ililazimika kuelekea Arusha na
kutua kwenye uwanja huo mdogo kuweza kupokea ndege kubwa kutokana na
kuishiwa mafuta.
Ndege hiyo iliyokuwa inatokea Addis Ababa,
Ethiopia ikiwa pia na wahudumu 23, baada ya kutua kwenye Uwanja wa
Arusha, ilinasa kwenye tope baada ya tairi lake la mbele kuvuka sehemu
ambayo lami inaishia kutokana na ufupi wa njia zinazotumiwa na ndege
zinapotua kwenye uwanja huo.
Jitihada za kuiondoa ndege hiyo zilishindikana
jana. Ndege hiyo ilikuwa ikielekea Johannesburg, Afrika Kusini kwa
kupitia Kia na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es
Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alisema: “Rubani amejitahidi kutua katika uwanja huu japo ni mdogo ili
kuokoa maisha ya abiria kwani walikuwa hawana mafuta ya kutosha kwenda
uwanja mwingine.”
Tukio la ndege hiyo kutua kwa dharura limekuja
siku chache tangu ndege ya Shirika la Ndege la Precision iliyokuwa na
abiria 37 kupasuka matairi manne ilipokuwa ikitua kwenye Uwanja wa KIA
Jumamosi iliyopita.
No comments:
Post a Comment