Makamanda wa bavicha walipo mtembelea Mjane wa Marehemu Kamanda Mbwambo, Ephata Nanyaro (wa pili Kushoto). Picha na MAKTABA |
Ephata Nanyaro ni miongoni mwa vijana wanaojitanabaisha kuwa
wanachama na viongozi waaminifu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) mkoani Arusha.
Ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema
(Bavicha) Mkoa, na vilevile ni mwenyekiti wa chama hicho wa Wilaya ya
Arusha Mjini. Nanyaro ambaye anajulikana kimsimamo ndani ya chama hicho,
pia ni Diwani wa Kata ya Levolosi kupitia chama hicho cha upinzani
nchini.
Wiki iliyopita nilipata wasaa wa kuzungumza naye
mambo mbalimbali kuhusu yeye na siasa ambapo pamoja na mambo mengine
anaeleza malengo na mikakati yake katika siasa kuwa ni kutetea wananchi
wanaoonewa na kukandamizwa na mfumo kandamizi.
Swali: Ni lini hasa ulianza kujishughulisha na masuala ya siasa, na je, ni kitu gani kilikusukuma?
Jibu: Nilianza rasmi kushiriki shughuli za kisiasa
mwaka 2005, ingawa kabla ya hapo nilikuwa mfuatiliaji wa siasa za
upinzani tangu mwaka 1995. Nilijikuta nikivutiwa na jinsi viongozi
walivyokuwa wakiibua hoja nzito za kuukosoa utawala kwa lengo la kutetea
wananchi.
Hii ilinifurahisha sana na nikajikuta nikivutiwa
na kupenda kufuatilia habari mbalimbali za siasa. Niliendelea kuwa
karibu na shughuli za siasa hadi mwaka 2005 nilipojiunga rasmi Chadema.
Pia niliamua kuingia kwenye siasa ili kupata uwanja wa kupigania
mabadiliko katika Taifa langu.
Swali: Kwa nini ulichagua Chadema na siyo chama kingine?
Jibu: Nilichagua Chadema kwa kuwa ni chama pekee
chenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania. Misingi ya kuanzishwa
kwa Chadema ndiyo iliyonivutia, hasa demokrasia. Taifa letu lilikuwa na
bado linapita katika kipindi kigumu ambacho hakuna demokrasia ya kweli
wala maendeleo.
Swali: Vipi umejipangaje kukabiliana na changamoto za kisiasa ndani na nje ya chama chako.
Jibu: Changamoto kwenye siasa ni nyingi lakini
ukiongozwa na dhamira ya kweli, huwezi kushindwa. Nimekuwa nikiongozwa
na maslahi ya taifa kuliko maslahi madogo madogo ya watu au vikundi
fulani.
Hii ndiyo imani yangu kwa kuamini kuwa maana taifa
litaendelea kuwepo lakini watu watapita. Kwa upande wa siasa za ndani
ya chama Mkoa wa Arusha hususani Wilaya ya Arusha Mjini ina changamoto
nyingi mno, hivyo chama tunashirikiana pamoja na jamii kukabiliana na
changamoto za kisiasa na kiuchumi.
Bahati mbaya chama tawala ambacho kimsingi hakipo
tena, kimeshindwa kutatua changamoto za kiuchumi badala yake Serikali
inawekeza zaidi katika kukihujumu chama chetu, hivyo sisi tuna uongozi
shirikishi, kwa maana ya kushirikisha jamii kwa ujumla ili kutatua
changamoto hizo.
Swali: Kwa nini uligombea udiwani?
Jibu: Niligombea ili niweze kubadilisha sheria
kandamizi zinazotungwa na watendaji wa halmashauri na ambazo zinawaumiza
wananchi wanyonge wasio na mitaji wala uwezo.
Kwa mfano katika mtaa ninaoishi mwaka 2006
nilihamasisha wananchi wenzangu tukajenga barabara kwa kiwango cha
changarawe, baadaye nikaja kukamatwa na maofisa wa manispaa kwa kosa la
kuboresha barabara bila kibali, nilitakiwa ama nilipe faini ya Sh50,000
au wanifungulie kesi mahakamani. Nilikubali kupelekwa mahakamani ambapo
kesi iliishia hewani.
Swali: Una malengo gani kisiasa?
Jibu: Malengo yangu kisiasa ni kuwatumikia kwa
uadilifu wapigakura wa Levolosi kwa kipindi hiki kilichobaki, bado tuna
kazi kubwa ya kufanya kwenye maeneo ya miundombinu
Malengo yangu vilevile ni kutetea wananchi
walioonewa na kukandamizwa na mfumo kandamizi. Unajua katika Serikali
kuna mifumo ya kiuongozi ambayo inakandamiza haki za watu. Kuna mifumo
ambayo siyo shirikishi, na hii inasababishwa na kukosekana kwa
wawakilishi wa wananchi katika vyombo vya kutolea uamuzi.
Ukiangalia Bunge, kwa mfano, halina wawakilishi wa
kijamii na badala yake wote waliopo ni wawakilishi wanasiasa. Hakuna
mbunge anayewawakilisha wakulima, wanafunzi wa vyuo vikuu, wafugaji…Hii
inasababisha hata sheria zinazotungwa na Bunge zinakuwa hazina maslahi
ya kijamii. Maana Bunge halina wawakilishi mbalimbali wa kijamii.
Mfano mdogo ni ile sheria ya fao la kujitoa ambalo
wabunge wote waliipitisha, kwa mtazamo wangu hii sheria ilipita bila
kupingwa kutokana na kukosekana kwa wawakilishi wa wananchi ndani ya
Bunge wanaoumizwa na sheria ile.
Swali: Ni mwanasiasa gani wa nje au ndani ya nchi
ambaye unavutiwa naye na ambaye ndiye aliyekuhamasisha kujiingiza katika
siasa?
Jibu: Kwa kweli mtu aliyenivutia na
aliyenishawishi kujiunga na siasa ni Freeman Mbowe. Nimekuwa nikivutiwa
na jinsi kiongozi huyu anavyojenga na kusimamia hoja zake, anavyoibua
vitu na kutetea maslahi ya wananchi na kwa kweli naweza kukiri kuwa
nimejifunza sana kupitia kiongozi huyu.
Swali: Ungepewa nafasi ya kuongoza nchi ungeanza na lipi unaloona limezorota?
Jibu: Kama ningepata nafasi ya uongozi wa nchi
eneo ambalo ningeanza nalo ni katika sekta ya elimu. Ni imani yangu kuwa
elimu ndiyo msingi wa maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa kwa
ujumla.
Yapo mambo mengi yanayolalamikiwa na ambayo yanasababisha elimu
yetu iendelee kudidimia. Masuala kama ya kutokuwepo kwa mitalaa, hili
limepigiwa kelele na wabunge lakini inashangaza hakuna marekebisho
yoyote yaliyofanywa.
Nikipata fursa ya kuongoza ambayo naamini siku
moja nitaipata, nitalimulika eneo hilo na kuhakikisha upungufu wote
unaotajwa unarekebishwa na elimu inaimarika. Elimu ndiyo msingi wa kila
kitu na hakuna Taifa lolote duniani ambalo limeendelea bila elimu.
Swali: Nielezee historia fupi ya maisha yako.
Jibu: Kwanza nina umri wa miaka 30, nina mke na
watoto wawili – Ethan na Ethana. Nimekuwa kiongozi wa ngazi mbalimbali
ndani ya Chadema na hadi sasa nashikilia nafasi ya Uenyekiti wa Baraza
la Vijana (Bavicha) Mkoa wa Arusha. Vilevile mimi ni Mwenyekiti wa Chama
wa Wilaya ya Arusha Mjini na kama nilivyoeleza huko juu mimi ni Diwani
wa Levolosi. CHANZO : MWANANCHI
No comments:
Post a Comment