<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<>>>>>>>>>>>>>>>>>>
Na Pamela Chilongola - Mwananchi
Dar es Salaam. Mfanyabiashara wa magari, Gabriel Munisi (35), jana alijiua baada ya kumuua mtu mmoja na kujeruhi wengine watatu jijini Dar es Salaam katika tukio linalohusishwa na wivu wa mapenzi.
Na Pamela Chilongola - Mwananchi
Dar es Salaam. Mfanyabiashara wa magari, Gabriel Munisi (35), jana alijiua baada ya kumuua mtu mmoja na kujeruhi wengine watatu jijini Dar es Salaam katika tukio linalohusishwa na wivu wa mapenzi.
Munisi, ambaye alikuwa mkazi wa Mwanza, aliwapiga
risasi watu watatu akiwamo mchumba wake, Christina Alfred katika Mtaa wa
Bungoni Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Baada ya kumpiga risasi mchumba wake huyo na
kudhania kwamba amemuua, inadaiwa kwamba Munisi aliendelea kuwamiminia
risasi watu wengine na kumuua mdogo wake Christina, Alpha (22).
Katika tukio hilo, Christina na mtu anayedaiwa
kuwa mchumba wake mpya, Francis Shumila wamelazwa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili baada ya kujeruhiwa. Mama yake Christina, Helen
Alfred amelazwa katika Hospitali ya Amana baada ya kujeruhiwa pia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marieta Minangi
alisema Munisi alikutwa na bastola moja, magazini mbili na yalikutwa
maganda 14 ya risasi zilizotumika na risasi mbili ambazo zilikuwa
hazijatumika.
Tukio hili limetokea mwezi mmoja baada ya
mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro kujeruhiwa kwa risasi na mzazi
mwenzake, Anthery Mushi.
Katika tukio hilo, Mushi alijiua baada ya kumuua
mama mzazi wa Ufoo na inaaminika pia tukio hilo lilisababishwa na
masuala ya mapenzi.
Lilivyotokea
Mashuhuda waliokuwapo katika tukio hilo walisema
mauaji hayo yalitokea saa 1.15 asubuhi baada ya Munisi kufika Ilala
Bungoni na kwenda katika Klabu ya Wazee iliyo jirani na eneo yalipotokea
mauaji na kunywa supu kabla ya kusogea karibu na lango la nyumba
anakoishi mchumba wake.
Mmoja wa majirani, Noel Gerald alisema alimuona Munisi akiwa amesimama karibu na lango la nyumbani kwa kina Christina.
Alisema baadaye waliona gari aina ya Toyota Hilux,
Surf, likitoka katika lango la nyumba hiyo na mara walimuona Munisi
akimwamuru dereva ashushe kioo lakini alikataa na kudai kwamba ndipo
alipoamua kuwapiga risasi waliokuwamo kwenye gari hilo.
Alidai kuwa Munisi alipiga risasi nane mfululizo huku akiwa
analizunguka gari hilo na kwamba alimpiga dereva ambaye baadaye
alifahamika kuwa ni Shimula. Imeelezwa kuwa majeruhi huyo ni raia wa
Kenya na ni rubani wa ndege.
“Katika gari lile walikuwemo watu watatu ambao ni
Christina, Helen na Shimula, ambaye alikuwa ndio dereva huku marehemu
Alpha akiwa getini na Munisi alimpiga risasi ya kifua,” alidai Gerald.
Shuhuda huyo alidai kwamba Munisi aliendelea na
mashambulizi yake kwani magazini ya kwanza ilipomaliza risasi katika
bastola yake, aliongeza nyingine na kumfuata mama yake Christina ambaye
pia alikuwa ndani ya gari hilo, na kumpiga risasi mkononi. Alidai kwamba
alipona baada kutoka na kukimbilia uvunguni mwa gari.
Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, Munisi
aliamua kujipiga risasi ya kifuani na kufariki papo hapo akiwa amekaa
karibu na lango hilo.
Ilidaiwa kwamba Shimula na Christina walikuwa wanaelekea Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kuelekea Visiwa vya Cyprus.
Uhusiano wa Christina na Munisi
Rafiki wa Munisi aliyejitambulisha kwa jina la
Samwel Alex alisema Christian alikuwa mchumba wa Munisi na walikuwa
wamepanga kuoana.
Alisema Munisi baada ya kuwa na wasiwasi na
mchumba wake ndipo alipoamua kumpigia simu mama mzazi wa Christina na
kumwambia kuwa amesikia mwanaye yupo hapo Dar es Salaam lakini alikataa
na kumweleza kuwa amesafiri kwenda Moshi.
“Ninawafahamu kwa muda mrefu, Christina alikuwa
anafanya kazi Barclays Bank na Munisi ni mchumba wake wa muda mrefu
kwani alikuwa anajulikana hata kwa ndugu zake wote,” alisema Alex.
Hospitali ya Amana
Mkuu wa Kitengo cha Dharura Hospitali ya Amana, Dk
Christopher Mzava alisema wamepokea majeruhi watatu wanawake wawili na
mwanamume mmoja pamoja na maiti mbili ya mwanamke na mwanamume.
Dk Mzava alisema kati ya majeruhi hao mmoja amelazwa Hospitali
ya Amana na wawili walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Msemaji
wa Aminiel Eligaesha alisema hospitali hiyo ilipokea maiti mbili moja ya
mwanaume ambaye jina lake halikufahamika na nyingine ya mwanamke,
aliyefahamika kwa jina la Alpha.
Pia alisema walipokea majeruhi wawili, Helen na
Shimula, ambaye amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili
(Moi), wote wakiwa na majeraha makubwa ya risasi.
No comments:
Post a Comment