KUTOKA MAGAZETINI: CHADEMA YASEMA MHE. ZITTO KABWE ALIPONZWA NA WARAKA TU - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


28 Nov 2013

KUTOKA MAGAZETINI: CHADEMA YASEMA MHE. ZITTO KABWE ALIPONZWA NA WARAKA TU

 
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika. Picha na Edwin Mjwahuzi   

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema kimesema kwamba kilifikia uamuzi wa kumvua nyadhifa zake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kutokana na sababu moja tu ya kuhusika katika Waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba waraka huo unaeleza mbinu za uasi ambazo zililenga kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho jambo ambalo ni kinyume na katiba, sheria na itifaki za Chadema.
Hivi karibuni, Kamati Kuu ya Chadema iliwavua nyadhifa zao, Zitto, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kutokana na madai hayo.
Siku tatu zilizopita, Zitto na Dk Kitila waliitisha mkutano wa wanahabari na kueleza sababu mbalimbali za kung’olewa kwao ikiwamo suala la posho na ruzuku za vyama vya siasa.
“Wamefukuzwa katika uongozi kutokana na kuandaa mpango wa mapinduzi uliopo katika waraka wa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013,” alisema Lissu na kuongeza:
“Hawa wote hawakuvuliwa madaraka kwa sababu ya taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu ukaguzi wa hesabu za chama, suala la posho kwa wabunge wala kuuza majimbo ya uchaguzi mwaka 2010.”
Alisema kutokana na kosa hilo, Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chadema ilikutana juzi kupitia uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu na kuridhika nao, “Leo (jana) wahusika wote watapatiwa barua zao zilizoorodhesha makosa yao kumi na moja wanayotakiwa kujibu ndani ya siku 14.” Bila ya kuyataja, Lissu alisema makosa hayo yote yamejikita katika waraka huo.
Mnyika pia alijibu hoja zilizotolewa na Wakili wa kujitegemea na Diwani wa Kata ya Mabogini mkoani Kilimanjaro (Chadema), Albert Msando juu ya kasoro wakati wa kutoa hukumu kwa makosa ya Zitto na Dk Kitila,  ikiwa ni pamoja na kukiukwa kwa katiba ya chama inayoeleza kuwa mtu hatachukuliwa hatua za kinidhamu kabla ya kupewa mashtaka kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kuyajibu kwa maandishi.
Mnyika alisema, “Zitto na Dk Kitila hawakumwambia wakili wao ukweli kwamba kanuni hii ya chama ilishafanyiwa marekebisho muda mrefu na Baraza Kuu la chama na kuongezwa kifungu (d), ambacho kinasema: “Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura kama inaona masilahi ya chama yanaathiriwa.”
Waraka
Mnyika alisema waraka uliowang’oa Zitto na Dk Kitila ambao umechapishwa katika magazeti mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii, siyo ule uliowasilishwa katika Kikao cha Kamati Kuu.
“Waraka utakaotumika katika mashtaka yao siyo huo. Sisi tutautumia ule ambao uliwasilishwa katika Kamati Kuu ambao una mambo makubwa na mengi zaidi kuliko huo unaochapishwa sehemu mbalimbali, ikibidi tutautoa huo waraka halisi,” alisema.
Naye Lissu alisema kuwa kitendo cha kuandaa mkakati huo ni kinyume na utaratibu na kanuni za chama hicho, kufafanua kuwa ndiyo maana Chadema mwaka jana kilitengeneza mwongozo wa wanachama kutangaza kusudio la kuwania uongozi ndani ya chama, mabaraza yake na Serikali.
Alisema ni makosa kupanga mkakati wa kutaka kumweka mtu madarakani bila kutangaza au kumwambia mtu yeyote.
Kuhusu PAC
Lissu alisema masuala ya PAC yalizungumzwa katika kikao cha Kamati Kuu, lakini hayakuwa miongoni mwa hoja za kumng’oa Zitto.
Alisisitiza kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alishindwa kuvikagua vyama vya siasa kwa sababu hakuwa na fedha za kufanya hivyo, kwamba jambo hilo alilieleza wazi na vyama pamoja na Msajili wa Vyama vya Siasa walilipinga.
 “Leo hii, mwaka mmoja baadaye Zitto anaibuka na badala ya kusema CAG ameshindwa kukagua hesabu za vyama, anasema vyama vimekataa kukaguliwa.
Alisema kuna nyaraka ambazo Zitto akiwa Naibu Katibu Mkuu alitakiwa kuzifahamu.
Alisema Oktoba 15 mwaka huu, siku ambayo Zitto aliibua tuhuma za vyama kutokaguliwa, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alimwandikia barua CAG akimweleza kuwa wajibu wa kukagua vyama vya siasa ni wa kwake na hatakiwi kulipwa na vyama hivyo, wala Ofisi ya Msajili wa Vyama.
Mnyika alisema matukio yaliyotokea mkoani Kigoma baada ya Zitto kuvuliwa uongozi, ikiwa ni pamoja na kuchomwa moto bendera za chama hicho na kuharibiwa kwa baadhi ya majengo ni mchezo wa kuigiza na uhuni uliofanywa na watu ambao si wanachama wa Chadema.
Ratiba ya Uchaguzi
Awali, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema hicho, Benson Kigaila alieleza maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu kujipanga kuanzia ngazi ya chini mpaka taifa.
Pia aligusia suala la kugatua madaraka kutoka makao makuu kwenda katika Kanda 10 pamoja na Progamu ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), ambayo utekelezaji wake ulikuwa na awamu nne unaombatana na mafunzo mbalimbali.
Kuhusu uchaguzi, alisema kuanzia Novemba 22 hadi 14 Desemba, mwaka huu ni kipindi cha kukamilisha usajili wanachama kuanzia ngazi ya chini.
“Tarehe 15 Desemba mpaka 15 Januari, 2014 utafanyika uchaguzi katika ngazi za vitongoji. Kuanzia tarehe 16 Januari  hadi 30 Januari, 2014 kitakuwa kipindi cha kukata rufaa na kukagua ukamilifu wa uchaguzi wa ngazi hiyo,” alisema Kigaila na kuongeza:
“Februari 1 hadi 15 mwaka 2014, utafanyika uchaguzi ngazi za matawi (vijiji kwa vijijini na mitaa kwa mjini), kuanzia Februari 16 hadi 29, itakuwa kipindi cha kukata rufaa na ukaguzi kwa ngazi hiyo.”
Alisema kuwa kuanzia Aprili Mosi hadi 10, 2014 utafanyika uchaguzi ngazi ya majimbo ya uchaguzi ambayo yapo 236 na kuanzia Aprili 25 mpaka Mei 5, 2014 utafanyika uchaguzi ngazi ya wilaya.
Alisema kuanzia Mei 20 mpaka 25, 2014 utafanyika uchaguzi ngazi za mkoa na Juni 6 hadi 9, 2014 utafanyika uchaguzi katika Kanda zote 10 na Juni 23 mpaka 30, 2014 utafanyika uchaguzi ngazi ya taifa. Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad