WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda anaondoka Dar es Salaam Oktoba
15, 2013 kwenda China kwa ziara ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa
Serikali ya nchi hiyo inayotarajiwa kuanza Oktoba 16.
Lengo
la ziara ya Waziri Mkuu ni kutangaza fursa za uwekezaji hapa nchini,
fursa za biashara, za utalii na kutafuta mitaji kwa ajili ya sekta
zilizo chini mpango wa matokeo makubwa ya haraka (Big Results Now
Initiative).
Kwa
mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi
hiyo, Mhe. Li Keqiang na viongozi wa Serikali ya China katika katika
sekta za uchukuzi, mawasiliano, viwanda, madini na nishati.
Atatembelea
mji wa Beijing na majimbo ya Shenzen, Chengdu na Guangzhou ambako
atakutana na Makamu wa Rais wa China, Rais wa Benki ya Exim ya China,
Rais wa Benki ya Maendeleo ya China, wakuu wa mashirika makubwa na
kampuni kubwa nchini China na kufanya nao mazungumzo.
Waziri
Mkuu Pinda ataungana na Wakuu wa Nchi watano kwenye ufunguzi wa
maonyesho ya kibiashara ya magharibi mwa China (Western China
International Fair – WCIF) ambako atahutubia washiriki wa maonyesho
hayo. Pia atatembelea maeneo kadhaa ya uwekezaji na kufungua Kongamano
la Uwekezaji baina ya Tanzania na China litakalofanyika Guangzhou.
Vilevile, Waziri
Mkuu anatarajiwa kufungua mafunzo ya siku 10 kwa maafisa 20 kutoka
idara na taasisi za serikali za hapa nchini yanayoendeshwa kwa pamoja
baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha utendaji
wa Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ).
Waziri
Mkuu ambaye anafuatana na Mawaziri wanne, wabunge wawili, wakuu wa
mikoa watatu, wakuu wa taasisi wa Serikali na wawakilishi kutoka sekta
binafsi, anatarajiwa kukutana na Watanzania waishia China huko Beijing
na Guangzhou.
Tanzania imekuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na China, nchi kubwa ya Bara la Asia, tangu mwaka 1964.
China yenye ukubwa wa kilometa za mraba 9,596,961 ina wakazi wapatao 1,349,585,838. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika Fedha la Kimataifa (IMF) nchi hiyo ni ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.
No comments:
Post a Comment